Miaka mitatu iliyopita Mwanasheria maarufu nchini, Mabere Marando alitoa kauli ambayo si mimi tu, bali Watanzania wengi hatukumwelewa.
Kauli yenyewe ilikuwa hivi: “Tanzania ni nchi yenye bahati. Ni nchi pekee duniani inayojiendesha bila Rais.”
Wapo walioichukulia kama vijembe vya kisiasa, na mimi ni mmoja wao, ila kadri siku zinavyopita na hasa baada ya Rais Dk. John Pombe Magufuli kuingia madarakani, kauli ile inadhihiri usahihi wake.
Sitanii, Novemba 20, 2015 wakati anazindua Bunge, Rais Dk. Magufuli alisema baadhi ya watu wamesafiri nje ya nchi mara nyingi kuliko walivyokwenda vijijini kwao kuwaona wazazi wao.
Bila shaka alitumia diplomasia, lakini uhalisia alikuwa akimsema Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ambaye wanaharakati wanasema ametumia muda mwingi nje ya nchi katika kipindi cha uongozi wake.
Nimeamini kuwa maneno ya wahenga, si ya kubeza. Walisema sikio la kufa halisikii dawa. Wapo wanaosema Kikwete tangu ametoka madarakani amesafiri mara sita nje ya nchi, ila mimi nilizo na uhakika nazo ni nne.
Amekwenda Ethiopia, Afrika Kusini, Comoro na wiki iliyopita Uingereza. Anafanya ziara hizo, bila hata kuona aibu kutokana na agizo la Rais Magufuli, hata kama yeye si mtumishi wa umma tena.
Mbunge wa Kibamba (CHADEMA), wakati huo akiwa Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alisema Rais ni dhaifu. Ameshindwa kusimamia Serikali na watumishi wa umma wanafanya kila wapendalo.
Kilichomkuta baada ya kauli hiyo ni kufukuzwa bungeni kama adhabu ya kutoa lugha ya kukera. Hata hivyo, waliokuwa wakifuatilia hali halisi ya utendaji wa Serikali, walibaki wanasikitika.
Leo nchi yetu ina kipindupindu kila kona. Maeneo kama Mkoa wa Kagera, tangu enzi za Mkoloni hayajawahi kupata kipindupindu. Vyanzo vya maji vilikuwa vya kutosha. Usafi ulikuwa wa hali ya juu. Wenyeji walimiliki mashamba makubwa yenye kuruhusu hewa safi kusambaa na yalipaliliwa na hata wasiokuwa na choo, walitumia zana ya asili (omushote).
Ingawa maji ya bomba ni msamiati kwa maeneo mengi ya Kagera, ila maeneo kama Mlima wa Kibeta, Rugambwa, Kahororo, Ihyungo, Nshambya na Nyangoye hayakuwa makazi ya watu.
Kwa sasa watu wamejenga milimani sawa na walivyofanya Mwanza. Hawa waliojenga milima hiyo hawana mahala pa kuchimba mashimo ya vyoo au mashimo ya maji taka (septic tanks).
Wengi wanatumia mapipa au vyoo vilivyojengwa kwenye mawe. Mvua zikinyesha vinatiririsha maji taka katika mto Kanoni. Mto Kanoni unasukuma uchafu mpaka Ziwa Victoria. Pale Bakoba yanapochukuliwa maji ya bomba, ni jirani na mto Kanoni unapomwagia maji ziwani. Niulize kinachofuata. Maji ya ziwa yanavutwa na kuingizwa kwenye matangi, na sina uhakika kama yanatibiwa vyema kuua wadudu.
Sitanii, ni wakati wa Serikali ya Kikwete tumeshuhudia ujenzi holela. Kwa mji wa Bukoba kama hakuna kitakachofanyika juu ya wakazi wa Manispaa waliojenga kwenye mawe maeneo niliyoyataja ikiwamo Buyekela kwa juu, basi tujue kipindupindu imefika si mgeni wa kupita. Mkuu wa Mkoa wa Kagera asimamie ujenzi wa mfumo wa maji taka kwa gharama ya wakazi wa milimani.
Nashauri ujengwe mfereji mmoja mkubwa, hata ikibidi kwa gharama za wakazi wa milima hiyo, na mfereji huo wa maji taka utoe fursa ya wenye nyumba kuunganisha vyoo vyao kwenye mfereji huu kisha kwa chini maeneo ya Buyekela au Kashozi Road lichimbwe shimo kubwa la maji taka, mfereji huyo utumike kukusanya uchafu na ufyonzwe baadaye kupelekwa katika dampo huko Kata Nyanga. Bila kufanya hivyo, kipindupindu kitakuwa cha kudumu Bukoba.
Alipokutana na wafanyabiashara jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Rais Dk. Magufuli ametoa kauli iliyopasua moyo wangu, kwa kusema: “Sijui kama mnafahamu, lakini ukweli ni kwamba tangu Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2015/2016 ipitishwe Juni 30, mwaka huu, hakuna fedha yoyote iliyokwisha kutolewa kwenye wizara kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
“Kama kutolewa, basi tutakuwa tumeanza kuzitoa kwenye wizara kuanzia mwezi huu (Novemba 2015), Katibu Mkuu Kiongozi yuko hapa, aseme. Miezi sita tangu bajeti hiyo ipitishwe, hakuna hata senti kwa ajili ya maendeleo iliyotolewa na Hazina kwa ajili ya wizara yoyote, bali zilizokuwa zikitolewa ni zile za mishahara tu na kwenye shughuli nyingine.
“Kwa hiyo, ninapojaribu kusema haya na kusisitiza umuhimu wa ninyi kulipa kodi, hatufanyi haya kwa sababu ya jeuri, bali kwa nia njema ili malengo ya Watanzania yaweze kutimia. Kwa hiyo, niwaombe sana ndugu zangu.” Maneno haya yamenifanya nilowane mwili mzima. Nikakumbuka bajeti zilizopita na Rais aliyemaliza muda asivyoona aibu.
Zipo wizara kwa miaka mitano mfululizo zimepata asilimia 20 ya fedha zilizotengwa. Huduma za jamii zimezorota kwa kiwango kikubwa, kwa sababu kuu moja tu. Rais wetu aliyemaliza muda amekuwa akienda nje ya nchi kubembeleza tupewe misaada. Mmoja wa misaada iliyolidhalilisha taifa letu ni huu wa MCC. Kwa miaka miwili sasa Wamarekani wanasema utatolewa. Haujatolewa.
Rais Dk. Magufuli umeyaona na unayafahamu haya. Hotuba yako tumeichapisha yote kwenye gazeti letu. Hayo unayoyashuhudia ndiyo yamewafanya Watanzania wengi kuichukia CCM. Ukisema fedha za maendeleo hazijapelekwa wizarani, hii inamaanisha wakandarasi na wazabuni wote wa Serikali hawajalipwa kwa kazi walizozifanya kwa muda wa miezi sita au zaidi.
Mniwie radhi naomba niliseme hili. Hazina ya Tanzania inategemea zaidi uimara wa waziri wa fedha. Hata kama tunalenga kutoa kipaumbele kwa jinsia, tuangalie nani tunamkabidhi nini. Hii dhana ya 50 kwa 50 haikuletwa iangamize mataifa machanga. Dhana hii imeletwa kwa nia njema kuwezesha kinamama, ila si kwa mtindo aliofanya Kikwete.
Wapo waliomshambulia Profesa Ibrahim Lilpumba aliposema Waziri wa Fedha aliyemaliza muda, Saada Mkuya hakuwa ameiva kushika wadhifa kama huo ambao ni roho ya nchi. Mimi ni mmoja wa walioamini hivyo, ila hoja ya Profesa Lipumba ilipotoshwa na wanaharakati wakasema Waziri wa Fedha hakustahili kuwa Mwanamke.
Yapo mambo sikubaliani na Lipumba, lakini hili la kusema Saada Mkuya hakuwa na sifa za kushika wadhifa huu, nitakuwa wa mwisho kupingana naye. Narudia, wapo wanawake mahiri, kama Dk. Asha Rose Migiro, Samia Suluhu Hassan, Amina Salum Ali, Getrud Mongela na wengine wengi wenye sifa za kutosha kushika wadhifa mzito kama huu.
Nazikumbuka vyema bajeti za Basil Mramba akiwa Waziri wa Fedha katika Serikali ya Rais Benjamin Mkapa. Mramba pamoja na makosa yake ya kiubinadamu kwamba sasa hivi ‘anachezea ndoo’ lupango, lakini mtakumbuka wakati wa Rais Mkapa nchi hii uchumi ulivyosimama. Serikali ilifika mahala ikarejesha heshima kwa wafanyakazi.
Nchi ilifika mahala ikaweza kujitegemea katika mambo mengi. Hapo juu nimezungumzia kipindupindu, lakini Mkapa akiwa Rais alimshinikiza na kumwezesha Waziri wa Maji wakati huo, Edward Ngoyai Lowassa miradi mikubwa ya maji ikajengwa. Tulishuhudia mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi Shinyanga na Kahama. Maji yalipofika Shinyanga kipindupindu ikafutika.
Mkapa alikuwa akiimba sera ya maji mita 400 kutoka mlango wa kila familia kwa aliye mbali. Mramba ilikuwa ukimhoji anakwambia fedha zipo, tatizo ni watu kushindwa kuzitumia (absorption capacity). Rais Magufuli ikiwa gazeti hili litaingia mtaani kabla ya kutangaza Baraza la Mawaziri chondechonde nakusihi. Heshimu jinsia, lakini tanguliza masilahi ya taifa kwanza.
Mwanaume asiye na uwezo usimweke katika Baraza la Mawaziri. Mwanamke asiye na uwezo, usimweke katika Baraza la Mawaziri. Baraza si darasa. Si mahala pa kufundishia uongozi. Kaulimbiu yako ya HAPA KAZI TU, ianzie kwenye Baraza. Sitarajii upeleke watu kwenye semina elekezi ambazo zimefanyika nyingi katika serikali zilizopita, lakini hakuna lolote zilicholifanyia taifa.
Hivi hata kazi ya kukamata makontena ya wafanyabiashara uliowataja inahitaji semina elekezi? Hivi hata kufanya usafi lazima Rais aunde Kamati au Tume ya kuchunguza kwa nini usafi haufanyiki? Nakuhakikishia Mheshimiwa Magufuli, agizo lako la watu kufanya usafi linatelekezeka. Nimeshuhudia Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongela alivyowabana wakazi wa Kagera. Watu wamechimba vyoo wanalia!
Sitanii, hata kwenye vijiwe vya kahawa au baa, leo unaona kuwa watu wanawaza kuwa Serikali ipo. Ni masikitiko makubwa kuwa mtangulizi wako hata alipoaga kuwa angetembelea wizara, mkoa au taasisi fulani, watumishi kitu pekee waliochokuwa wanafanya ni kuandaa hotuba nzuri, chai na… Akifika, wanapiga picha, hotuba inatolewa, kisha anapongezwa kwa kazi!
Naomba kuhitimisha makala hii kwa ushauri. Kama ulikuwa unawaza hili, basi kuanzia leo lifute. Kitu kinachoitwa misaada nchi yetu haiwezi kuendelea kwa misaada. Wawezeshe Watanzania wenye nia ya kufanya biashara na kuwekeza, wafanye kazi. Watanzania wakiwekeza, watalipa kodi, wataajiri Watanzania na hata fedha zao watakazopata hizo za kigeni baada ya kuuza bidhaa na huduma nje ya nchi, zitabaki kwenye benki za hapa ndani.
Rais Dk. Magufuli wezesha wazawa, nchi ipige hatua, ukitegemea misaada, utasubiri sana. Yote hayo na mengine ninayowaza, sasa yananifanya nikubaliane na Marando, kuwa kweli inawezekana Tanzania imejiendesha miaka 10 bila Rais, ambayo ni bahati ya pekee. Je, Magufuli ungependa nawe uingie katika mkondo wa Kikwete? Kupanga ni kuchagua.