Wale wanaopenda kutazama runinga wanaona kwa macho yao namna siasa za Tanzania zinavyobadilika kwa kasi kila siku.
Mwishoni mwa wiki walionekana wananchi kwenye maeneo kadhaa katika vijiji vilivyopo mikoa ya Arusha na Tanga wakichoma na wengine wakichana kadi zao za uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kilichowashitua watazamaji wengi, si matendo ya kuchana au kuchoma kadi tu, bali ni aina ya watu waliofanya matukio hayo.
Matukio ya aina hiyo yalikuwa ya kawaida kufanywa na wananchi wa mijini ambako inaaminika ndiko kwenye ngome za vyama vya siasa vya upinzani.
Mathalani, hakuna anayeweza kushangaa kuona matukio ya aina hiyo yakitokea Musoma Mjini, Mwanza mjini, Mbeya mjini, Dar es Salaam, Arusha, Moshi na katika miji mingine mikubwa ambako vyama vya upinzani vina wafuasi wengi.
Kwa miaka mingi, vijijini kumetambulika kama eneo muhimu la ushindi kwa Chama Cha Mapinduzi. Mambo yanaelekea kuwa tofauti sasa. Upinzani umeshapenya hadi huko. Hii ni habari njema na ni mfano halisi wa namna elimu ya uraia ilivyopenya na hata kuwaingia wananchi walio mbali na miji mikubwa. Kwa upande mwingine, hii si habari njema kwa Chama Cha Mapinduzi. Kuna nahau na methali za wahenga kama vile: “Mdharau mwiba, mguu huota tende”; “Bandu bandu humaliza gogo”, au “Mwanzo wa ngoma ni lele”. Mwandishi mahiri, Chinua Achebe katika riwaya yake ya Things Fall Apart, hayuko mbali na hiki kinachoendelea CCM.
Sina shaka yoyote kusema kwamba tangu kurejeshwa kwa mfumo wa siasa ya vyama vingi nchini mwaka 1992, mwaka huu wa 2015 siasa zimebadilika mno. Wananchi wanajiamini. Wamepata ujasiri wa aina yake. Wanajiona wako huru kushabikia mgombea au chama wanachokitaka bila hofu yoyote; na kwa ufupi tu ni kwamba wako huru kuchukua uamuzi wowote wa kumchangua au kutomchagua mgombea yeyote au chama chochote. Haya ni mapinduzi makubwa kwenye safari yetu ya kujenga mfumo wa demokrasi ya vyama vingi vya siasa.
Sidhani kama Chama Cha Mapinduzi na viongozi wake mahafidhina wanalitambua hilo. Na kama wanalitambua, hatuna hakika kama wanalikiri na kuwa wako tayari kubuni nguvu mpya za kisiasa za kukabiliana na mabadiliko haya.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ni wa kipekee kwa sababu wagombea wakuu wawili – Dk. John Magufuli na Edward Lowassa – wana rekodi za utendaji kazi zinazofanana kwa kiwango kikubwa. Kufanana huko kunaweza kuwa kwa manufaa kwa upande wa Ukawa kuliko CCM kwa sababu wapo wapigakura wanaoonekana kuwa na kiu ya kubadili mfumo wa uongozi wa wa Taifa letu. Wapigakura wengi, zaidi ya asilimia 60 ni vijana. Hawa ni pamoja na wale wasioijua historia ya CCM wala waasisi wake. Kwa mfano, watoto ambao walikuwa na miaka mwili au mitatu mwaka 1999 wakati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, anafariki dunia, mwaka huu watapiga kura. Hawa wanasikia tu kwamba CCM ni “Chama cha Nyerere”. Wanasikia namna wazee wengi na watu wa rika la kati wanavyomsifu Mwalimu na kushangilia uongozi wake. Wanamsikia kupitia simulizi na mara kadhaa kwenye maandishi na hotuba zake fupi fupi zinazorushwa na vituo kadhaa vya redio na runinga. Hawa vijana wapigakura wapya hawawezi kuichagua CCM au mgombea wake kwa sababu wanamjua, wanampenda na wanamheshimu Mwalimu.
Wapigakura wengi wa aina hii kwao wanachotaka ni kuwapigia kura watu wanaowaona kwa sifa na muonekano wao. Hawa ndio wale waliojawa hasira za kuiondoa CCM madarakani, na unapowauliza kwanini wanachukua uamuzi huo, majibu yao mara zote yamekuwa haya: “CCM imetawala sana, au CCM imeiharibu nchi hii.” Kwao wao, hawawezi kuihukumu CCM kwa kulinganisha yale ya miaka ya 1960, 1970, 1980 na haya yanayoonekana leo. Kwao wao, kusafiri kwa barabara kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kwa saa zisizozidi 13 ni kero kubwa kwao; lakini kwa wale wa enzi zetu tunajua safari hiyo ilituchukua siku tatu! Kwa hiyo mtu wa zama hizo ukimweleza kuwa CCM haijafanya lolote la maana kwa miaka yote hii, hawezi kukuelewa.
CCM wanapaswa walitambue na walikiri hilo. Wajue watanyimwa kura, pengine si kwa sababu ya kushindwa kabisa kuiendeleza nchi hii, isipokuwa ni kwa sababu kizazi cha sasa hakiyajui hayo yanayoifanya ijivune. Chenyewe kinataka mabadiliko tu hata kama hayana tija. Libya walipomwondoa Muammar Gadafi, hawakufanya hivyo kwa sababu kiongozi huyo hakuwapa maendeleo. Aliwapa kila walichotaka. Walikula. Walikunywa. Aliwapa mahari wakaoa na kuolewa. Aliwapa mishahara wasio na kazi. Aliwahapa huduma zote. Pamoja na yote hayo mazuri, wananchi, kwa kushawishiwa na maadui wa Magharibi, wakamng’oa Gadafi na kumuua. Leo wanajuta. Walichotaka Walibya ni mabadiliko bila kujali matokeo ya hicho walichotaka. Kwa meneno mengine ni kwamba vitu vyote vinaweza visibadilike, lakini mabadiliko lazima yatokee.
Wapinzani wa CCM, hasa Ukawa wasibweteke na wingi wa hizi habari za kuhama kwa wanachama wa CCM na kujiunga nao. Habari za kwenye runinga, redio, magazeti na hasa hasa kwenye mitando ya kijamii ni zinaweza kuwafanya wabweteke. Watambue kuwa hao wanaoihama CCM na kujiunga nao ni sehemu ndogo tu kati ya kubwa sana ya Watanzania. Ushindi hauwezi kupatikana kwa kubweteka na taarifa za kwenye mitandao ambazo mara nyingi ni za kishabiki na za kupeana matumaini pasi na ukweli au uhalisia. Kwanza, ni wajibu wa Ukawa kujiuliza ni wapigakura wangapi wa Tanzania wenye uwezo au fursa ya kushiriki kwenye mijadala inayoendelea kwenye mitando ya kijamii. Kubweteka tu na idadi au ushabiki kwenye mitando hiyo kunaweza kuwa na athari kwa Ukawa. Wanaweza kujawa matumaini ya kushinda, lakini mwisho wa siku matokeo yakawashangaza na kubaki wakilalamikia “goli la mkono” hata kama ni “goli la kichwa”.
Pamoja na hayo yote, ukweli unabaki pale pale kuwa mwaka 2015 ni mwaka wenye changamoto nyingi na kubwa mno kwa Chama Cha Mapinduzi. Ni mwaka ambao kwa mara ya kwanza CCM inashuhudia ikiwapoteza baadhi ya makada wake wenye nafasi kubwa ndani ya chama. Kwa mara ya kwanza mtu aliyefikia wadhifa wa Waziri Mkuu amekihama chama hicho. Wenyeviti wa CCM wa Mikoa wamehama. Waliokuwa wakuu wa mikoa wamejiengua na kwenda upinzani. Watu mashuhuri kama kina Juma Mwapachu, wameonekana wazi wakiyataka mabadiliko. Hawa ni tone tu. Idadi ya watu wanaoushabikia upinzani isiyotaka kujitokeza wazi wazi ni kubwa mno kuliko wakati mwingine uliopita.
Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba endapo uchaguzi utakuwa huru na wa haki, Chama Cha Mapinduzi kwa mara ya kwanza kipoteza viti vingi vya udiwani, uwakilishi na ubunge. Sina hakika kwenye urais, lakini huko kwingine, CCM ijiandae kisaikolojia, ikiwezekana hata ianze kufikiria namna ya kuunda Serikali ya Mseto.
Dalili kwamba CCM itakuwa na wakati mgumu ni kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwishoni mwa mwaka jana. Kama CCM ina wataalamu wa siasa wakweli na wanaoitakia mema, matokeo yale yalitosha kuwafanya watafute njia za kukifanya chama kiendelee kuaminiwa na wapigakura kabla ya Oktoba, mwaka huu.
Lakini kama ni kuendesha chama kwa mazoea, au kwa ndoto za kutumia vyombo vya dola kujitwalia ushindi, nchi inaweza kuingia kwenye ukurasa mbaya wa kihistoria. Hapa ni wajibu wa CCM na Ukawa kutambua na kuheshimu kuwa bila haki, hakuna amani.
Kama nilivyogusia hapo awali, bado naona nafasi ya CCM kuendelea kushikilia nafasi ya urais ipo. Hilo litawezekana tu endapo watu waliopewa dhima ya kulifanikisha hawapeana maneno ya kufarijiana au kupeana matumaini hewa. Wala wasidhani kuwa Watanzania hawajui wanachotaka. Timu ya kampeni iwe timu makini yenye watu wenye ushawishi wa hali ya juu. Ndani ya CCM kuna watu ambao wakipanda jukwaani kumnadi mgombea, basi hapo hapo CCM ihesabu maumivu.
CCM watambue kuwa Ukawa wana rasilimali watu na vitendea kazi vya kutosha. Kama tatizo lilikuwa fedha kwa uchaguzi wa miaka iliyopita, mwaka huu hilo si tatizo kwao. Kwenye suala la vitendea kazi, sioni CCM- kama chama watakuwa na usafiri au zana ambazo Ukawa watakuwa hawana. Kama ni magari wote wanayo. Kama ni helikopta, wote wanazo. Kama ni ndege, kila upande uko sawa sawa.
Kwenye vyombo vya habari kumeshaonekana. Kila unaposoma habari ya Ukawa, pembeni ipo ya CCM.
Ukichukua maandalizi haya ya rasilimali fedha na watu; ukijumlisha na sifa za wagombea ambazo zinakaribiana mno, unaona wazi kabisa kuwa mwaka huu mchuano ni mkali. Hii ni kama mechi ya Simba na Yanga ambayo mara nyingi matokeo hujulikana baada ya kipyenga cha mwisho. Kama Ukawa walikuwa wanyonge dhidi ya CCM, basi unyonge huo mwaka huu umepungua sana. CCM wanachoweza kutamba nacho zaidi ya Ukawa ni nguvu za dola walizonazo.
Lililo muhimu ni kwamba Watanzania wanapenda kuona kampeni za kiungwana na hatimaye washiriki Uchaguzi Mkuu ulio huru na wa haki. Siasa na wanasiasa watapita, lakini Tanzania na Watanzania wataendelea kuwapo milele. Ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunadumisha amani, utulivu, upendo na mshikamano. Ili haya yawezekane, ebu sasa tuanze kufikiria kuundwa kwa Serikali ya Mseto.