Na Byarugaba Innocent, JamhuriMedia,Kibaha
Naibu Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Ridhiwan Kikwete ameanza ziara rasmi ya Kikazi Mkoani Pwani ambapo Julai 10,2023 ameongea na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kibaha ikiwa niwendelezo wa kuhamasisha na kuboresha utendaji wa kazi.
Kikwete amesema Utumishi mzuri ni Chachu ya Maendeleo katika eneo unalihudumia na kuwataka watumishi kuwa wabunifu na kufanyakazi kwa weledi ili kuwaletea wananchi Maendeleo ambayo ndio dira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Aidha,Kikwete amekemea vikali watumishi wanaotumia muda wa mwajiri kisemana kwa meseji za hovyo,kugombanishana,kufarakishana badala ya kufanyakazi na kwamba katika Utumishi wa umma haipendezi kwani mafanikio katika taasisi yoyote ile yanategemea watumishi walivyojipanga kufanyakazi zao kwa kushirikiana ili kuleta tija.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe.Abubakari Kunenge amempongeza Mhe.Kikwete kwa kufanyakikao kazi hicho wakati wa ziara yake kuzungumza na watumishi ambao ndio rasilimali watu muhimu za nchi na kuwataka watumishi kutambua haki na wajibu wao kwa Taifa.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe.Nickson Simon amesema Kibaha Mji Ina watumishi 2438 kati ya 2582 sawa na asilimia 94 ambao wamekuwa Chachu ya Mafanikio kisekta.
Aidha,ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwapandisha vyeo watumishi 604 na kupata watumishi wa ajira mpya 63 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na kwamba vyeo hivyo na ajira mpya vimeamsha ari ya utendaji.