Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mlele
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geophrey Pinda amewaasa Watanzania kuhakikisha wanakuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo kwa kuwa ardhi iliyopo haiongezeki na idadi ya watu inazidi kuongezeka.
Mhe. Pinda amesema hayo tarehe 26 Desemba 2023 nyumbani kwake Kibaoni, Halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi katika hafla maalum ya chakula aliyowaandalia wananchi na viongozi wa jimbo lake kusheherekea Siku Kuu ya Chrismas.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda, Naibu Waziri huyo wa Ardhi amesema, wakati serikali ikiandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, watanzania wanatakiwa kuwa na mpango wa matumizi ya ardhi huku wakielewa changamoto kubwa iliyo mbele yao ni kuwa ardhi haiongezeki.
‘’Miaka 25 inayokuja lazima tufikirie hizi hekta na ekari tulizopopewa na Mungu ikaitwa Tanzania inatushoje itakapofika miaka hamsini ijayo, kwa hiyo ni sisi ndiyo tutakaopanga tutumiaje maeneo yetu’’ alisema Pinda.
‘’Kila mtu akikaa ajue ardhi ni yake na ndugu zake kwa hiyo tuishi kwa amani na tusigombane, hakuna namna tutakachokifanya katika eneo hili ni lazima tukubaliane namna ya kuitumia ardhi ndogo katika ongezeko kubwa la watu’’ amesema Pinda.
Akigeukia shughuli za maendeleo kwenye jimbo lake la Kavuu, Pinda amewaambia wananchi wake kuwa, jimbo hilo kwa sasa limepiga hatua kubwa ukilinganisha na miaka ya nyumba kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amewezesha utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo hata ile ambayo haikutajwa kwenye ilani ya CCM na kutolea mfano ujenzi wa zahanati, shule na miundombinu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpimbwe Shamimu Mwariko aliwapa ushauri wananchi wa Mpimbwe kuwa, kama wanataka halmashauri yao ifanane kimaendeleo na halmashauri zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo basi wahakikishe wanawashika viongozi wanaofanya maamuzi ya kimkakati.
‘’Kama kweli mna lengo la kusema sasa sisi Mpimbwe iwe inafanana na eneo fulani shikeni viongozi wanaofanya mamuzi kimkakati, utekelezaji wao, mipango yao ni kuhakikisha wanafungua njia watu waweze kupita njia hizo ndiyo kazi ya kiongozi yoyote duniani’’, alisema Shamim
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda amemtaka Mbunge wa Jimbo la Kavuu ambaye ni mdogo wake kuwa karibu na wananchi wakati wote wa juhudi mbalimbali za kuliletea maendeleo jimbo lake.
‘’Hoja kubwa ya wananchi unaowaoongoza ni mahusiano, mnaishije? Kila aliyesimama amekupa sifa ni jambo zuri kazi yako sasa ni kutoharibu sifa, kaza uzi na jishushe kadri inavyowezekana na watu wote ni wa kwako hata wale mliopingana’’ alizsema Mizengo Pinda.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda yuko jimboni kwake katika Halmashauri ya Mbimbwe mkoa wa Katavi kujumuika wananchi wa jimbo la Kavuu pamoja na mambo mengine kusheherekea Siku Kuu ya Chrismas na wananchi wa jimbo lake.