Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geophrey Pinda ametaka kuwepo upendo miongoni mwa watumishi ili waweze kutekeleza majukumu kwa ufanisi.
Aidha, amewataka watumishi hao wa sekta ya ardhi kufanya kazi kwa bidii ili serikali ione matunda na ufanisi wa kazi walizotumwa kuzitekeleza.
Pinda amesema hayo tarehe 9 Februari 2023 jijini Dodoma wakati alizingumza na viongozi na watumishi wa Wizara ya Ardhi Makao makuu.
Amesema, akiwa kama Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi asingependa watumishi wa sekta hiyo kuishi bila upendo ndiyo maana ameamua kukutana na kada zote za sekta ya ardhi kwa lengo la kujua changamoto za watumishi wa kada hizo.
Ameongeza kwa kusema, upendo miomgoni mwa watumishi siyo tu unatoa faraja kwa watumishi bali unarahisisha kazi za wizara kwa kuwa watumishi hao watakuwa wakifanya kazi kwa furaha na amani.
Aidha, amebainisha kuwa, uamuzi wa kukutana na watumishi unalenga pia kuwafunda na kuwaweka karibu watumishi ili wizara ya ardhi ifanye kazi kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya.
“Nimeona nikae na watumishi kwa hekima na busara ili nifahamu changamoto zinazowakabili na kuzitatua ili mwisho wa siku kuondoa malalamiko yanayotolewa kwa wizara” alisema Mhe. Pinda.
“Shati letu limejaa madoa, ukipita mtaani wakiona mtumishi wa ardhi wanasema ni wale wale na sauti za kulaumu ni kali kweli kweli” amesema Pinda.
Vile vile, mhe Pinda ametaka watumishi wa sekta hiyo kupewa stahiki zao kwa mujibu wa sheŕia, taratibu na miongozo iliyopo ili wafanye kazi kwa bidii bila manung’uniko.
“Watumishi wakipewa posho stahiki utaona jinsi wanavyokimbiza mambo na ugumu utaisha” amesema Pinda.