Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa wa Ujenzi na Uchukuzi wa Jamhuri ya Namibia Mheshimiwa John Mutorwa, amewasili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati.
Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi za Afrika utafanyika nchini tarehe 27-28 Januari 2025 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere.

Mhe. Mutorwa amepokelewa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa John Mutorwa anamwakilisha Rais wa Namibia katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati, ambao unawaleta pamoja viongozi wa Afrika, wadau wa sekta ya nishati, na washirika wa maendeleo.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati unalenga kuimarisha juhudi za pamoja katika kukabiliana na changamoto na fursa za nishati barani Afrika, sambamba na kupitisha Azimio la Dar es Salaam. Azimio hilo linasisitiza dhamira ya Viongozi wa Nchi na Serikali za Afrika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu, na endelevu kote barani.