Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Namtumbo
NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Marryprisca Mahundi ambaye pia ni Mbunge wa viti maalum kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), amewataka wananchi kutunza vyanzo vya maji na amewaonya baadhi ya watu wanaojihusisha na uharibifu wa mazingira kwa kukata miti ovyo sambamba na hufanyaji wa shughuli za kilimo , kuingiza mifugo kwenye vyanzo vya maji kuacha mara moja kwani vitendo hivyo vinachangia kuwepo kwa ukame na kusababisha kukosekana kwa maji.
Hayo ameyasema jana kwenye mkutano wa hadhara kwa wananchi wa kata ya Mgombasi na Kata ya Kitanda zilizopo katika halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ambapo alikuwepo mkoani humo kwa ziara ya siku 3 kutembelea na kukagua miradi ya maji katika halmashauri mbili ambazo ni Namtumbo na Tunduru.
Alisema kuwa kuna umuhimu kwa wananchi kupewa elimu juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na madhara yake hivyo ni jukumu la halmashauri husika kuendelea kuelimisha faida za utunzaji wa mazingira ili maji yaendelee kuwepo na wananchi waweze kufaidika na miradi ya maji inayotekelezwa na serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Awali akihutubia wananchi wa kata ya Kitanda ambako kuna mradi wa maji ya mtiririko ambao hadi kukamilika utagharimu kiasi cha sh. Bilioni 3.1 na utahudumia wakazi wapatao 15,000 alisema kuwa serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kwenye miradi hivyo ni vyema jumuia za maji zilizoundwa zikasimamia miradi hiyo kwa wananchi kuchangia kiasi kidogo cha fedha ambazo zitasaidia kufanyia ukarabati pindi miundombinu hiyo ya maji itakapo haribika badala ya kusubiri serikali itoe fedha kwaajiri ya kukarabati.
Aidha amewataka wananchi watambue kuwa miradi yote inayotekelezwa mijini na vijijini ni utekelezaji wa ilani wa chama cha mapinduzi hivyo ni wazi kabisa kuwa serikali yao inawajari na kuwataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali yao ya awamu ya sita ya Raisi Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwaletea maendeleo.
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa ameishukuru Serikali na amempongeza naibu waziri huyo kwa kuwaingiza kwenye mpango wa bajeti na atimaye wamepata fedha ambazo zimesaidia kupata mradi wa maji ya mtiririko katika kata mbili na kwamba utawasaidia wananchi ambao mwanzo walikuwa wakichota maji toka mtoni jambo ambalo lilikuwa ni kero kubwa.
“Ziara yako naibu Waziri ni kuja kuangalia mradi lakini kuwapa moyo wananchi, kwamba mradi huu utakamilika kama tulivyokusudia ndugu zangu ili mpate maji na nia ya Raisi wetu Dkt. Samia Suluu Hassan wote tunaijuwa ni kumtua mama ndoo kichwani na kazi hii katika Wilaya yetu Naibu Waziri mmefanya kazi kubwa sana tulikuwa na mradi hapa umekwama miaka 8 lakini kupitia wizara yako mlisema mtalitatua na mmelitatua” amesema mbunge huyo Kawawa.
Nae Diwani wa Kata ya Mgombasi Mrisho Mbawala amesema kuwa kwa sasa idadi ya watu imeongezeka kwa hiyo mahitaji ya maji ni makubwa hivyo wanaiomba serikali iwaongezee maeneo ya vichotea maji ili wananchi waweze kuondokana na usumbufu wa kufuata maji katika maeneo mengine ambapo alibainisha kuwa vichotea maji vilivyojengwa ni 21 angalau vifike 30.
Mkurugenzi wa RUWASA Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Mhandisi David Mkondya akisoma taarifa ya miradi hiyo ya maji ya mtiririko kwa Naibu waziri wa maji amesema kuwa miradi hio ya maji katika kata zote mbili ya Mgombasi na Kitanda hadi kukamilika itagharimu kiasi cha shilingi bilioni 5.8 na utahudumia wanachi zaidi ya 30000 na kwamba tayari wameshaweka mikakati ya kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu na wataendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji.
Nao baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo wakiongea na mwandishi wa gazeti hili wameishukuru serikali kwa kuwaletea mradi huo wa maji ambao wanaimani utawapunguzia kero ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji jambo ambalo lilikuwa linawakwamisha kwenye shughuli zao za kila siku za kujileta maendelao ndani ya famila zao.