Na Lusungu Helela, JamhuriMedia, Iringa
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amefungua mafunzo ya mfumo mpya wa usimamizi wa utendaji kazi wa mtumishi na taasisi katika utumishi wa umma (PEPMIS & PIPMIS) mkoani Iringa ambapo amesema mfumo huo utakuwa mwarobaini kwa watumishi wasiotekeleza wajibu wao.
Aidha, Kikwete amefungua pia mafunzo ya mfumo wa tathmini ya mahitaji ya rasilimaliwatu utakaowezesha kubainisha mahitaji ya rasilimaliwatu katika Taasisi husika.
Akizungumza leo Mkoani Iringa na watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizopo mkoani Iringa pamoja na Taasisi na Mashirika ya umma, Mhe. Kikwete amesema mifumo hiyo imelenga katika kuboresha utendaji kazi unaojali matokeo na tija katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
‘’Tumetuma watalaamu nchi nzima kwa ajili ya kujenga uelewa wa namna ya kutumia mifumo hiyo ya kidigitali ambayo tunaamini itasaidia watumishi wa umma kuwahudumia wananchi kwa viwango vya juu’’ amesema Kikwete.
Hata hivyo, Kikwete amesema mwanzo Serikali ilikuwa ikitumia mfumo wa wazi wa mapitio na upimaji wa utendaji kazi (OPRAS) kusimamia utendaji kazi wa watumishi wa umma lakini kutokana na changamoto zake imeamua kuja na mfumo mpya ambao utajibu changamoto za mfumo wa OPRAS.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amesema Mkoa ameishukuru Ofisi ya Rais, UTUMISHI kwa kufika Iringa kwa ajili ya kutoa mafunzo ya namna ya kutumia mifumo hiyo ya kidigitali kwa ajili ya kupima utendaji kazi wa watumishi wake ambapo ameihakikishia ofisi hiyo kupata ushirikiano wa kutosha .
Timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Rais, UTUMISHI ikiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Mikataba ya Utendaji Kazi, Bi. Zainab Kutengezah ipo mkoani Iringa kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa watumishi ya namna bora ya kutumia mifumo hiyo.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizopo mkoani Iringa pamoja na Taasisi na Mashirika ya umma wakati akifungua mafunzo ya mfumo mpya wa usimamizi wa utendaji kazi wa mtumishi na taasisi katika utumishi wa umma (PEPMIS & PIPMIS/ HRA
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akisoma taarifa ya hali ya watumishi Mkoani Iringa kabla ya kufungua mafunzo ya mfumo mpya wa usimamizi wa utendaji kazi wa mtumishi na taasisi katika utumishi wa umma (PEPMIS & PIPMIS/ HRA