Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Nyasa.

WANANCHI wa Kata ya Chiwanda wilayani Nyasa mkoani Ruvuma wametakiwa kuchagua viongozi bora wa serikali za vijiji na vitongoji kwenye uchaguzi unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu ambao wataweza kuwaletea maendeleo na kutatua changamoto zinazowakabili na si vinginevyo.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya Nyasa sekondari mara baada ya kuwasha umeme kwa mara ya kwanza katika shule hiyo.

Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga akiwasha umeme wa REA katika shule ya Nyasa Sekondari mapema Jana.

Amesema kuwa ili kumuunga mkono Raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluu Hassan ni vyema kuwachaguwa viongozi wale watakao kuwa tayari kubeba shida na ajenda za maendeleo za wananchi.

” Mwaka huu ni mwaka muhimu sana wa uchaguzi wa serikali za Vijiji na vitongoji ili tuendelee kuwaunga mkono viongozi wa Chama cha mapinduzi (CCM) maendeleo haya yanapatikana kwa sababu ya viongozi mahili wa CCM kwa sababu wanaongea lugha moja mpaka kwenye serikali za mitaa kuhakikisha tunawaletea ninyi watu wa chiwanda kupata maendeleo ” alisema Naibu Waziri huyo Judith Kapinga .

Aidha amewataka wananchi hao kushiriki zoezi la kuboresha daftari na wahakikishe wanapiga kura kwa kuwachaguwa viongozi bora ambao watakuwa wachapa kazi katika kuwaletea maendeleo kwenye kata yao.

Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Chimate Kata ya Chiwanda Wilayani Nyasa.

Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga yupo kwa ziara ya siku mbili ya kikazi katika Wilaya ya Mbinga na Nyasa ambapo akiwa Nyasa kwa mara ya kwanza kupitia wakala wa Umeme vijijini (REA)amewasha umeme katika shule ya Nyasa Sekondari yenye mchepuo wa masomo ya Hati.

Awali Naibu Waziri huyo alipata fursa ya kuzungumza na wanafunzi wa kike na kuwaasa wasome kwa bidii na kuwapa zawadi ya taulo za kike ili ziweze kuwasaidia wawapo shuleni hapo.