Kamati maalum imebuniwa kupanga kuapishwa kwa Kithure Kindiki kama Naibu Rais mpya nchini Kenya.
Mkuu wa Wafanyakazi ambaye pia ni Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Kosgei ametangaza kwenye gazeti la serikali kamati ya wanachama 23 kusimamia kuandaliwa kwa hafla ya kuapishwa kwa Naibu Rais Mteule Kithure Kindiki.
Kupitia gazeti rasmi la serikali, Ijumaa tarehe 1/11/2024, imetangazwa kuwa Sikukuu ya Kitaifa.
Hilo linawadia muda mfupi baada ya Mahakama Kuu nchini humo kuondoa amri zinazomzuia Naibu Rais Mteule Kithure Kindiki kuapishwa.
Kithure Kindiki aliteuliwa na Rais William Ruto tarehe 18 Oktoba, 2024 kama Naibu Rais Mteule, na kupitia kipengele cha 149 (1) cha katiba, Bunge la Kitaifa lilimuidhinisha.
Hata hivyo, upande wa Naibu Rais aliyeondolewa madarakani Rigathi Gachagua uliwasilisha ombi la kuzuia kuapishwa kwa Kindiki Kithure kama Naibu Rais mpya, siku moja baada ya Bunge la Seneti kupiga kura ya kumuondoa Gachagua madarakani.
Wakati wa kusikiliza kesi hiyo, jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Eric Ogola, Anthony Mrima na Fredah Mugambi walisema kuwa afisi ya kikatiba ya naibu rais haiwezi kuachwa wazi.
Vile vile, Rais William Ruto amemteua Waziri Mkuu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi kukaimu Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo ilikuwa inashikiliwa na Kithure Kindiki.