Mahojiano kuhamasisha fursa za uwekezaji Sekta ya Madini Nchini
Na Wizara ya Madini- Bangkok
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo Septemba 7, 2023 alifanya Mahojiano na Mwakilishi Maalum wa Jarida la The New Jeweller, Anand Parameswaran katika Maonesho ya 68 ya Vito na Usonara yanayoendelea jijini Bangkok nchini Thailand.
Jarida hilo ni maalum katika kuchapisha na kutangaza masuala mbalimbali yanayohusu Sekta ya Madini katika nyanja zote zinazohusu mnyororo mzima wa shughuli za uongezaji thamani madini duniani hususan bidhaa za madini ya Vito na Usonara.
Kutokana na Tanzania kuwa kivutio katika maonesho hayo ambapo inatajwa kwa sehemu kubwa madini ya vito yanayopatikana kwenye maonesho hayo yana asili ya Tanzania, uwepo wake katika maonesho hayo umekuwa kivutio kikubwa kwa wafuatiliaji wa masuala ya madini.
Aidha, kufanyika kwa mahojiano hayo kumetoa nafasi kwa Tanzania kuendelea kuhamasisha fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya madini nchini ikiwemo azma ya Serikali ya kurejesha minada ya madini nchini lengo likiwa ni kuwavutia zaidi wanunuzi na wauzaji wakubwa wa madini kutoka maeneo mbalimbali duniani kufika Tanzania.
Akizungumza na Mwakilishi huyo, pamoja na masuala mengi yaliyozungumzwa, Mbibo amemweleza mambo kadhaa ikiwemo mazingira wezeshi ya kibiashara katika Sekta ya Madini ambayo yamekuwa moja ya kichocheo kikubwa kinachopelekea wawekezaji wakubwa kuichagua Tanzania.
Pia Mbibo amemweleza kwamba, Serikali imekuwa ikizifanyia kazi kwa karibu changamoto na mapungufu ambayo yameonekana kuwa kikwazo katika biashara ya madini ambapo imewezesha kufanyika kwa marekebisho katika Sheria ya Madini na Kanuni mbalimbali zinazosimamia Sekta ya madini nchini.
Kupitia mahojiano hayo, Mbibo amewaalika wadau mbalimbali kushiriki katika Jukwaa la Kimataifa la Uwekezaji katika Sekta ya Madini linalotarajiwa kufanyika Oktoba 25 na 26, 2023 jijini Dar es salaam.
Jarida la The New Jeweler hutolewa kila Mwezi na kusambazwa maeneo mbalimbali duniani.