Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salam
Joto la kinyang’anyiro katika nafasi ya Mwenyekiti wa tume ya umoja wa mataifa linazidi kupanda kwa wagombea wa nafasi hiyo.
Nafasi hiyo ya uenyekiti imekuwa ikishikiliwa na Moussa Faki raia wa Chad tangu mwaka 2017 ambapo kwa sasa wagombea watatu pekee wanagombea nafasi hiyo huku mmoja wao akitegemewa kurithi kiti hicho cha juu katika ngazi za kisiasa barani Afrika.
Yafuatayo ni majina matatu ambayo yaliwekwa hadharani tangu mwishoni mwa mwaka jana 2024, yanayotajwa kati yao ndiye atakayekuwa mrithi wa mwenyekiti wa sasa Mousa Faki .
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002508690.jpg)
RAILA ODINGA(KENYA)
Raila Odinga raia wa Kenya mwenye umri wa miaka 80, alizaliwa Januari 7, mwaka 1945 anasimama kama muwakilishi pekee kutoka ukanda wa Afrika mashariki katika kiti hicho .
Jina hili si jina geni sana katika medani za kisiasa katika ukanda wa Afrika mashariki na kati kwani amekuwa miongoni mwa wakongwe wa siasa nchini Kenya.
Raila Odinga amekuwa akisifika katika kupigania mageuzi ya siasa za Kenya, harakati zilizomfanya kuingia katika misukosuko ya kukamatwa na kuachiliwa mara kwa mara tangu mwaka 1982 mpaka 1991 wakati wa utawala wa Rais pili wa Kenya, Hayati Daniel Arap Moi.
Pia mwanasiasa huyo mkongwe amewahi kuhudumu kama Waziri mkuu wa Kenya, wadhifa ulioundwa kufuatia mkataba wa kitaifa uliofikiwa kumaliza ghasia baada ya uchaguzi wa mwaka 2007-2008 ambapo aligawana mamlaka na Rais Mwai kibaki.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002508691.jpg)
MOHAMOUD ALI YOUSOF(Djibout).
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 60 , alizaliwa Septemba 2 ya mwaka 1965 . Mahmoud Ali mbali na ugombea huo ameshawahi kuhudumu kama Waziri wa mambo ya nnje wa taifa hilo lenye umuhimu wa kimkakati katika eneo la upembe wa Afrika tangu 2005.
RICHARD RANDRIAMANDRATO (Madagascar)
Richard James Randriamandrato nae alizaliwa Machi 7 ,1959 . Kiongozi ambae pia ni amewahi kuhudumu kama Waziri wa mambo nnje wa nchi ya Madagascar ambapo alifutwa kazi mwezi oktoba 2022 kwa sababu za kulipigia kura azimio la umoja wa mataifa lililolaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Huku kwa wakati huo taifa lake likidai kuwa alikuwa amekiuka msimamo wao wa kutoegemea upande wowote.
Kama msemo wa waswahili usemao “Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo.” ndivyo hali ilivyo kwa sasa kwani nchi hiyo imeamua kumuunga mkono kugombea uenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika.
Wakuu wa nchi na serikali za mataifa ya Afrika jumamosi hii watapiga kura kumchagua mwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika zoezi litakalowakutanisha viongozi mbalimbali mjini Addis Ababa, Ethiopia huku kitendawili kigumu kikibaki kuwa ni nani atakayeshinda nafasi ya kiti hicho.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002508692.jpg)