Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limeelezea dhamira yake kuhakikisha kuwa mafunzo ya ufundi na yale ya amali yanayotolewa kwenye vyuo na shule za sekondari za ufundi nchini yanazingatia viwango na ubora ili kuzalisha wahitimu wanaokubalika katika soko la ajira.
Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Lingwanda, ameeleza hayo Machi 19, 2025, wakati akichangia mada kuhusu mchango wa wahitimu wa ufundi stadi katika maendeleo ya jamii na uchumi, kwenye kongamano la maadhimisho ya miaka 30 ya VETA, linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mwajuma amesema matarajio ya Serikali ni kuwa na wahitimu wa ufundi na amali watakaochangia kikamilifu katika shughuli za uzalishaji kupitia ujuzi walioupata.
Amesisitiza umuhimu wa kufanyika tafiti za mara kwa mara katika sekta ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, ili kuwezesha uandaaji wa mikakati madhubuti ya kuboresha utoaji mafunzo kulingana na mahitaji ya viwanda na soko la ajira kwa ujumla.
“Tafiti za mara kwa mara zitasaidia kutoa taarifa sahihi kuhusu mahitaji ya soko la ajira na kutoa mrejesho kuhusu wahitimu wa ufundi, hivyo kuboresha utoaji mafunzo kwenye vyuo vyetu,” amesema Dkt. Mwajuma.
Dkt. Mwajuma amewahakikishia wadau kuwa NACTVET itaendelea kushirikiana nao katika kuimarisha utoaji mafunzo ya ufundi na kuzalisha wahitimu wenye sifa watakaoweza kuajirika na kuchangia katika maendeleo ya Taifa.
Aidha NACTVET inatarajia kuja na mfumo maalum wa kieletroniki utakaochakata takwimu na taarifa mbalimbali zinazotoka katika Vyuo vya Ufundi na Ufundi Stadi,Wahitimu,Waajili na wale wanaojiajili.

Amesema awali walikuwa wakitumia njia ya kawaida katika kukusanya takwimu na taarifa hizo hivyo baada ya mfumo huo utaweza kuwarahisishia kazi yao kwa urahisi na ufanisi.
“Sasa hivi tunataka kutengeneza mfumo utakaokuwa unakusanya taarifa kutoka kwa wahitimu wa taasisi za ufundi na Ufundi stadi kwa njia rahisi zaidi. Tunaishukuru Serikali kwa kutupatia bajeti ya nyongeza mwaka huu.
“Jukumu letu kama baraza ni kuhakikisha tunakuwa na taarifa au takwimu ambazo ni sawa ambazo zitaweza kufanyiwa kazi na watafiti pindi wanataka kujua mambo mbalimbali ya wahitimu ikiwemo walioajiriwa au waliojiajiri wapo wangapi hadi sasa,” amesema.


