Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Lindi

Wananchi wa Kijiji cha Nditi, Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, wameanza kuona manufaa ya vituo vya Askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), wakisema kuwa hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza uvamizi wa wanyamapori wakali na waharibifu, hususan tembo.

Wakizungumza Aprili 13, 2025 katika mkutano wa elimu kuhusu namna ya kukabiliana na wanyamapori hao, wananchi hao walieleza kuwa uwepo wa kituo cha kudumu cha askari katika eneo hilo umeleta utulivu na kuwawezesha kurejea katika shughuli za kilimo bila hofu.

“Kabla ya kituo hiki hatukuwa na amani, lakini sasa tembo wakionekana tunapata msaada kwa haraka. TAWA wametujengea kituo hapa Nditi, tunawashukuru sana,” alisema Saidi Juma Ngomo, mkazi wa kijiji hicho.

Ameongeza kuwa kwa miaka minne iliyopita, wakulima walikuwa wakikumbwa na hofu kubwa mashambani, lakini sasa hali imebadilika kwa kiasi kikubwa na jamii imeanza kuelewa umuhimu wa kuwa karibu na askari wa wanyamapori.

Wananchi hao wameiomba Serikali kuongeza idadi ya askari na vituo kama hivyo katika maeneo mengine ya wilaya ili kuhakikisha mapambano dhidi ya wanyamapori waharibifu yanakuwa endelevu na yenye tija zaidi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mhe. Mohamed Moyo, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuboresha mifumo ya ulinzi dhidi ya wanyamapori wakali.

“Kupitia baraza la madiwani tumepitisha bajeti ya kununua ndege nyuki kwa ajili ya kuimarisha jitihada za kudhibiti tembo. Hii ni dhamira ya kweli ya kuwalinda wananchi wetu na mali zao,” alisema Mhe. Moyo.

Akizungumza katika mkutano huo, Afisa Uhifadhi Mkuu wa TAWA kutoka Kanda ya Kusini Mashariki, Linus Chuwa, alisema kuwa Mamlaka hiyo imejenga vituo vitano vya kudumu katika maeneo yenye changamoto ya migogoro baina ya binadamu na tembo.

Alivitaja vituo hivyo kuwa ni pamoja na kile cha Kijiji cha Ngarambe (Rufiji), Milola (Lindi Manispaa), Nditi (Nachingwea), Chingurunguru (Tunduru), na Ngumbu (Liwale). Kila kituo kikiwa na askari waliopatiwa vifaa maalum vya kazi kama mabomu ya baridi na silaha za kisasa kwa ajili ya kutawanya wanyama bila kuwatisha wananchi.

Naye Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja, alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwapa kipaumbele wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi kwa kuhakikisha wanapata msaada wa haraka pindi wanapokumbwa na changamoto ya wanyamapori.

“Serikali haitakaa kimya kuona wananchi wake wakiteseka kwa sababu ya tembo. Tumejipanga kuhakikisha usalama wa watu na mali zao unalindwa kwa nguvu zote,” alisema Maganja.