ALHAMISI ya wiki iliyopita shule za msingi zilifungwa, watoto wakabaki majumbani na wazazi wao. Kwenye shule zao na katika vituo vingine mbalimbali, kulikuwa na kazi kubwa ya kisasa ya kuchagua makamishna wa polisi na uhalifu.
Jamaa hawa watafanya kazi hiyo hadi 2016 ambapo uchaguzi mwingine utafanyika England na Wales. Hili ni jambo la kufikirisha sana, si kwa sababu ya watoto kukosa shule wala muda wa uongozi wa makamishna, bali haja ya kuwa na watu kama hao.
Kwa hapa Uingereza (isipokuwa jijini hapa) wameshaona umuhimu wa kuwa nao, na kazi yao ni kufanya kazi na polisi kuangalia jinsi askari wanavyotumikia watu na kudhibiti uhalifu.
Ni kitu kama kile cha madaraka mikoani, ambapo badala ya rais, waziri au mkuu wa polisi kuteua viongozi wote, wananchi wanapewa nao nafasi ya kuamua na kuchagua.
Makamishna hao sio mapolisi, lakini ni watu wenye uzoefu wa mambo wanayofanya polisi na kazi yao ni kuwawajibisha polisi linapotokea jambo lakini si kuendesha jeshi la polisi kwenye maeneo yao.
Kwetu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunaona Inspekta Jenerali Said Mwema anavyosimamia polisi shirikishi jamii, ambayo ni nzuri. Zamani watu walikuwa wanawaona mapolisi kama maadui, isipokuwa pale wanapokuja kumkamata mtu aliyewaibia.
Kadiri elimu ilivyosambazwa, watu wameelewa umuhimu wa polisi, japokuwa bahati mbaya ni kwamba utendaji wa baadhi ya askari umezorota, wanaua watu, hawakamati wahalifu na mwisho wake wamelitia doa jeshi zima, akiwemo mkuu wao.
Labda mfumo huu wa uchaguzi unaweza kusaidia, kama wananchi wanavyowachagua wabunge wao na kuwawajibisha wanaposhindwa kuwatumikia. Pamoja na kuwa hii ni tofauti kidogo, kwa ujumla wake ni kitu kitakachowarahisishia kusimamia vyema eneo lao kiusalama.
Kwa ukubwa wa England, makamishna waliochaguliwa ni 41, kwa hiyo Tanzania wakipatikana hawa watakuwa zaidi ya maradufu. Tukiwa na wasimamizi kama hawa, watakuwa na nafasi maridhawa ya kuweka vipaumbele katika maeneo yao, kuwachagua makonstebo wakuu wa maeneo yao nini hasa polisi wafuatilie na kudhibiti na kutoa ripoti kila baada ya kipindi juu ya mafanikio, changamoto na yaliyoshindikana.
Hili wazo lilitokana na watu kulalamika kwamba hawana sauti kwenye maeneo yao, badala yake wanamwagiwa tu polisi wanaofanya kazi wanavyojua badala ya kama wanavyotaka wananchi. Hapa ndipo tunaanza kupata uongozi wa kutoka chini kwenda juu badala ya juu kwenda chini, uwakilishi wa wananchi unakuwa mkubwa na hatimaye amani inadumishwa.
Kama hapa Uingereza, kila mahali wameweka vifaa vya kudhibiti usalama, kuna ofisi za kuratibu vifaa hivyo na hata wakiwepo wahalifu inakuwa rahisi kufuatilia kwa kushirikiana na wananchi.
Hii ndiyo demokrasia wanayoitaka wananchi na wanayoihitaji vizuri na kwa Uingereza hili si jambo la siku nyingi kiutekelezaji. Lilikuwa wazo la siku nyingi lakini kisera liliwekwa miaka mitatau minne iliyopita na utekelezaji ukaanza mwaka baadaye na sasa uchaguzi umefanyika.
Hebu tuangalie mambo muhimu kama haya, tuyatafakari na kuamua mwelekeo gani tuchukue katika kuboresha polisi wetu na utendaji wao ili amani iwe kubwa kwetu. Tushauriane pia kupitia Jamhuri.