Raia wa Sweden, Susanna Nordlund, anayejulikana kwa uchochezi katika eneo la Pori Tengefu la Loliondo (LGCA), na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA), anatumia mbinu aruhusiwe kuingia nchini.
Susanna alifukuzwa nchini kwa ‘kupigwa PI’, mwaka 2010 lakini tangu wakati huo amekuwa akiingia kinyemela kabla ya kukamatwa mwaka jana na kusekwa rumande kabla ya kufukuzwa nchini kupitia Kenya.
Akiwa Kenya na baadaye Sweden, aliandika makala mbalimbali akitukana na kutoa kashfa kwa viongozi mbalimbali wa Tanzania.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa Aprili 3, mwaka huu, Susanna, kwa ghiliba, alirusha kete ya kwanza ya kuhakikisha anamwingiza ‘mkenge’ waziri ili aruhusiwe kuingia nchini.
Alimwandikia barua aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa wakati huo, Charles Kitwanga, akitaka aondolewe PI ili aweze kuingia nchini. Nakala ya barua hiyo aliipeleka kwa ubalozi wa Sweden jijini Dar es Salaam, ubalozi wa Tanzania ulioko Stockholm, Sweden; na kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Margot Wallstrom.
“Anamdanya waziri kwenye barua yake kwa kusema yeye ni mtalii, na kwamba alifukuzwa nchini mwaka jana (2015) kwa amri ya PI na akaenda Kenya,” kinasema chanzo chetu.
Susanna anataka amri hiyo iondolewe ili aweze kuingia nchini Tanzania na kufanya shughuli zake kihalali akiwa na viza ya kitalii yenye kumwezesha kupitia Namanga, Arusha hadi Loliondo.
“Sioni hatima yangu bila kutembelea Tanzania, msaada huu utakuwa wenye manufaa makubwa,” amesema Susanna kwenye barua hiyo ambayo JAMHURI imepata nakala yake.
Alivyonaswa mwaka jana
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na Mkuu wa Wilaya (DC) ya Ngorongoro, Hashim Shaibu (ambaye sasa amehamishiwa Kigamboni, Dar es Salaam), ndiye aliyeongoza Kamati hiyo kumkamata mwanamke huyo anayetajwa kuwa mdau mkuu katika kuiharibu Loliondo na Serengeti.
Alikamatwa saa 2 usiku katika Hoteli ya Onesmo iliyopo Wasso, akiwa anakula.
Uchunguzi wa awali ulionesha kuwa alifikia katika nyumba ya kulala wageni inayomilikiwa na aliyekuwa Mbunge wa Ngorongoro, Mathew ole Timan pamoja na mkewe, Tina.
Tina ni Mkenya aliyepata uraia wa Tanzania mwaka 2010. Ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwa amepata nafasi hiyo kabla ya kuwa raia wa Tanzania.
Susanna anatajwa kuwa ni miongoni mwa wachochezi wakuu wa migogoro katika Loliondo na athari za uchochezi huo sasa zimeingia hadi katika Hifadhi ya Serengeti. Amekuwa akitumia migogoro hiyo kuomba fedha kutoka mashirika mbalimbali ya kimataifa, na hilo linathibitishwa na kauli yake ya kuomba kuondolewa PI kwa kusema: “Sioni hatima yangu bila kuitembelea Tanzania.”
Susanna amekuwa akijiamini mno, hasa kutokana na kile anachosema kwamba endapo Serikali itaendelea kumfuatafuata, atahakikisha Sweden inakata misaada yake nchini.
“Tumesema sisi si maskini kiasi cha mtu kuvuruga nchi yetu kwa kigezo kuwa atatuchongea ili tusipate misaada kutoka kwao. Ina maana tunapewa misaada kwa kigezo cha kutuvuruga?” Amesema mmoja wa viongozi walioshiriki kumkamata.
Hii si mara ya kwanza kwa Susanna kuingia nchini licha ya kuwa na PI. Kwenye mtandao wake wa Just Conservation, anatamba na kuonesha namna alivyoweza kurejea nchini, kuzunguka na kufanya kilichomleta bila kuguswa. Hiyo ilikuwa Julai, 2013.
Shaibu alizungumza mwaka jana na JAMHURI na kuthibitisha kukamatwa kwa Susanna na kusema familia ya Timan inahojiwa kwa kumhifadhi.
Shaibu alisema mahojiano hayo yalilenga kujua sababu za kumhifadhi Susanna ambaye kina Timan wanatambua kuwa alishapewa hati ya kufukuzwa nchini (PI) tangu mwaka 2010.
“Tulimkamata Juni 23 usiku. Alipohojiwa alikutwa na vitu vingi ambavyo vingine ni hatari kwa usalama wa nchi. Alikuwa na questionnaire (maswali) mengi sana aliyopanga kuwauliza wanavijiji wa Oloipir, Mondorosi, Sukenya na kwingineko. Ni maswali ya uchochezi kabisa,” alisema DC Shaibu.
Alisema kwenye upekuzi huo, ilibainika aliingia nchini kupitia mpaka wa Namanga akiwa na hatia ya kusafiria ikimwonesha kuwa ni mtalii.
“Tulikaa naye hapa Loliondo (rumande) kwa siku tatu tukaona ni busara kumpeleka katika ngazi za juu mkoani. Mimi kama DC niliishia hapo,” alisema.
Kamishna wa Huduma za Uhamiaji na Udhibiti wa Mipaka, Abdallah Abdullah, aliiambia JAMHURI kwamba Susanna baada ya kushikiliwa Loliondo na Arusha, alifukuzwa nchini.
Alipoulizwa imekuwaje mtu aliyepewa PI akaweza kurejea nchini bila kutambuliwa kwenye mifumo ya utambuzi ya kisasa? Kamishna Abdullah alisema: “Alipofukuzwa nchini mwaka 2010 mfumo wa utambuzi wa kutumia kompyuta ulikuwa bado. Ilibidi tufukue nyaraka kuweza kutambua kuwa alishafukuzwa.
“Hivi sasa baada ya kubaini hilo taarifa zote zinazomhusu tumeshaziingiza kwenye mtandao. Akiingia tu, akigusa dole gumba kwenye mashine mara moja atatambulika.”
“Hapa tumesema hatuna huruma kwa watu wanaoshirikiana na wageni kuihujumu nchi yetu. Wananchi waendelee kutupatia taarifa za wageni na watu wanaowahifadhi.
“Mtu anajua kabisa huyu mgeni hatakiwi nchini, badala ya kumzuia yeye anamkaribisha. Mbaya zaidi hata kwenye hoteli hakuandika jina lake kwenye kitabu cha wageni. Hii ni kuonesha kwamba walijua kinachofanywa na huyo mgeni,” alisema Kamishna Abdullah.
Awali, Susanna alifanya mikutano ya siri katika maeneo ya Kertalo na Karkamoru akiwa na Tina.
Mmoja wa wananchi wanaokerwa na uchochezi unaofanywa na asasi zisizo za Serikali (NGO) amesema: “Nadhani kwa upeo wangu hizi ni harakati za kijasusi za Wazungu na ukoloni mamboleo kutikisa Serikali ya Tanzania (To destabilize Tanzania Government) wakimtumia Susanna Nordlung, wafadhili wa mataifa ya Magharibi, na mashirika ya kimataifa.
Wanazijengea uwezo NGO zote za Wamaasai wa Kenya na Tanzania ili baadaye waweze kurudisha ardhi za Wamaasai zilizochukuliwa na wakoloni wa Kiingereza na baadaye serikali za Tanzania na Kenya.
“Ardhi hizi kwa upande wa Tanzania ni Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, na Pori Tengefu la Loliondo kama sehemu za kuanzia na baadaye hifadhi za Mikumi, Tarangire, nk.
“Mikakati ni kuunganisha umoja na NGOs za Kimaasai ili wote wa Tanzania na Kenya waungane. Hawa watu (wafadhili wa Magharibi) siyo wazuri. Sasa hivi chunguza mabilioni ya fedha ambazo mashirika haya inazo pamoja na blogs. Ni hatari.”
Kwa muda sasa, Susanna na washirika wake wamekuwa wakikusanya mabilioni ya fedha kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa kile anachosema ni kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji na wenyeji “wanaonyanyaswa” na Serikali ya Tanzania katika maeneo yao.
Kupitia ufadhili wake, amekuwa akizimwagia NGOs fedha nyingi, huku silaha kuu ya kuhakikisha shughuli hiyo inaendelea ni kupandikiza migogoro ili Loliondo isitawalike.