Raia anayesadikiwa wa Ubelgiji anayetafutwa na Serikali kwa ukwepaji kodi wa zaidi ya Sh bilioni 10, Marc Rene Roelandts, analindwa na baadhi ya watumishi na viongozi wa Serikali, JAMHURI imeelezwa. Kwa sasa mfanyabiashara huyo yuko mafichoni nje ya nchi kutokana na tuhuma zinazomkabili, lakini habari zinasema watumishi wake wawili wamekamatwa.
Mbelgiji huyo ni mmiliki wa kampuni ya Aureus Limited ambayo zamani ilikuwa ikiitwa Mineral Extraction Technologies Ltd (Minextech). Inajihusisha na uchenjuaji wa marudio ya dhahabu ya wachimbaji wadogo kwa kutumia teknolojia ya kemikali ya sayanaidi (vat leaching). Kampuni hiyo inamiliki leseni ya uchimbaji madini ML 384/2009. Mitambo ya uchenjuaji ipo katika Kijiji cha Nyarugusu wilayani Geita na Nyakato jijini Mwanza.
Agosti hadi Septemba 2011, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) alifanya ukaguzi wa hesabu za fedha na kodi kwa kampuni hiyo na kubaini kasoro kadhaa zilizoikosesha Serikali mapato.
Baadhi ya kasoro hizo ni kampuni ya Minextech kuficha taarifa za mauzo ya kilo 63.27 za dhahabu zenye thamani ya Sh 2,763,426,787 katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2010. Udanganyifu huo ulibainika baada ya kulinganisha takwimu za uzalishaji zinazotunzwa na kampuni hiyo na taarifa za mauzo ya dhahabu zilizowasilishwa serikalini.
Ilibainika kutolipa Sh bilioni 9.085 kama Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya mauzo ya dhahabu katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2010. Pia haikulipa Sh 252,683,678 za PAYE katika kipindi hicho. Kampuni hiyo pia haikulipa Sh milioni 371.026 za mrabaha katika kipindi hicho.
Marc Rene ni nani?
Raia huyu wa Ubelgiji anatuhumiwa kuwa na hati tano za kusafiria – tatu zikiwa za Ubelgiji. Namba za hati hizo ni EG 125092, EH 096287 na EL 590081. Pia anatuhumiwa kuwa na hati mbili za kusafiria za Burundi zenye namba EE 132212 na EF 558746.
Amekuwa akiishi nchini kwa kibali ncha Daraja A alichopewa Novemba 2011; ingawa amekuwapo hapa nchini tangu mwaka 2005. Hakuna taarifa za Uhamiaji zinazoonesha namna anavyokuwa akiishi nchini kuanzia mwaka huo.
Uraia wake kimsingi bado ni wa utata kwani kuna baadhi ya nyaraka alizojaza akionesha kuwa yeye ni mzaliwa wa Uganda, lakini nyingine zikionesha kuwa alizaliwa Barcelona, Uhispania.
Anadaiwa kuwa na kiburi, pengine kutokana na ukwasi mkubwa alionao. Amewahi kuitwa Ofisi za Madini Kanda ya Ziwa lakini akaishia kumtukana Ofisa Madini wa Kanda hiyo, Salim Salim. Aliyekuwa Kamishna wa Madini Tanzania kwa wakati huo, Dk. Dalali Kafumu, naye amewahi kutukanwa na Marc.
Utoroshaji dhahabu
Dhahabu anayoisafirisha nje ya nchi ni yeye pekee anayetoa taarifa zake, kwa kuwa kwa kipindi kirefu Ofisi za Madini Mwanza hazikuwa na mzani wa kupimia! Amekuwa akifanya hivyo kwa msaada mkubwa wa maofisa wawili katika ofisi hiyo ambayo kwa sasa JAMHURI inayahifadhi majina yao. Imebainika kuwa nyaraka za kusafirishia madini hughushiwa kwa kutumika zaidi ya mara moja.
Katika benki moja (jina tunalo) jijini Mwanza, hutakiwa kuonesha ripoti halali ya dhahabu lakini kwa kuwa hakuna anayefuatilia, hulipa dola 100 na kupatiwa nakala za karatasi za mzigo kwamba umehakikiwa wakati si kweli.
Kampuni moja (jina tunalo) inasaidia sana kuwapo kwa mchezo huo mchafu. Marc ana rafiki yake raia wa Urusi mwenye jina la Vash anayemiliki kampuni inayojihusisha na ununuzi wa dhahabu. Marc huiuzia dhahabu kampuni hiyo na wakati mwingine hutumika kusafirisha dhahabu ya Marc.
Kwenye ripoti ya Tume ya Jaji Mark Bomani ilibainika kuwa kampuni ya Marc ni kati ya kampuni mbili zinazojihusisha na biashara ya dhahabu, ambazo zimeikosesha Serikali mapato ya Sh bilioni 46.5 kati ya Julai 2009 na Juni 2010.
Mtandao wa ukwepaji kodi ni mkubwa ukimhusisha mmoja wa maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inayesemekana amekuwa akimpa mbinu za ukwepaji kodi. Ushauri wa mtumishi huyo wa TRA inasemekana ndiyo uliomwezesha Marc kufungua kampuni nyingine baada ya kuona amebanwa alipe kodi anayodaiwa.
Hapo ndipo ukawa mwanzo wa kuzaliwa kwa kampuni ya Aureus Limited, baada ya kifo cha kampuni ya awali ya Mineral Extraction Technologies Ltd (Minextech). Kampuni ya Aureus imefunguliwa katika Kanda ya Kimapato ya Ilala jijini Dar es Salaam na “return” [mrejesho]yake kwa mwaka ni Sh 750,000 pekee.
Mgogoro wa ardhi na wanakijiji
Marc amekuwa kwenye mgogoro mkubwa na wanakijiji wa Nyarugusu. Mwenyekiti na Mtendaji wa Kijiji hicho, kwa nyakati tofauti wamewawakilisha wananchi kwenye kilio chao cha kupokwa ardhi yao bila fidia halali.
Ahadi alizotoa za kuchimba visima vya maji, ujenzi wa vyumba vya madarasa na huduma nyingine za kijamii hazijatekelezwa. Wananchi wamefungiwa barabara yao ya miaka yote kwa lengo la kuwazuia kupita karibu na eneo la mgodi. Wananchi na mifugo wameathirika kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni kemikali zinazotokana na uchenjuaji dhahabu.
Jeuri dhidi ya Waziri
Marc anajulikana kwa jeuri yake dhidi ya viongozi. Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, ni miongoni mwa walioonja joto la Mzungu huyo.
Wakati fulani ilifikishwa kesi kwake iliyomhusu Marc, na waziri akaamua kumwita yeye na mlalamikaji. Marc akalazimisha aingie kumwona Waziri bila kuwapo mlalakamikaji. Waziri akagoma. Kuona hivyo, Marc akaanza kutoa maneno ya kashfa akisema waziri hakuwa mtendaji, bali ni mwanasiasa tu, na kwa sababu hiyo hana mamlaka ya kumchukulia hatua. Maneno hayo ya kejeli aliyafikisha kwa Waziri Nahodha kupitia kwa msaidizi wake aliyejulikana kwa jina la Nelson.
Waziri alichukia, akaamua kuchukua uamuzi wa kinidhamu wa kusitisha vibali vyake vya ukazi. Akaandika barua kwenda Uhamiaji. Pamoja na hatua hiyo, wiki chache baadaye Marc alionekana akiendelea na shughuli zake bila wasiwasi wowote. Kilichotokea kwa Uhamiaji ni kwamba wasingeweza kumchukulia hatua kwa sababu hapakuwa na kosa la kisheria au kikanuni la kumwondoa nchini “mwekezaji”, na kwamba uamuzi wa kumwondoa ungeweza kuliingiza Taifa katika kesi na baadaye hasara.
Baadaye Ofisa Uhamiaji mmoja Kanda ya Mwanza anayejulikana kwa jina la Mselemu alimwezesha kupata “Certificate of Clearance”.
Katika sakata jingine la kutuhumiwa mambo mbalimbali, polisi walimfuatilia kwa ajili ya kumkamata. Wakapata taarifa kuwa amepanga katika Hoteli ya Holiday Inn, Dar es Salaam. Kabla ya kukamatwa alipewa taarifa na msiri wake. Akaamua kukodi chumba kingine ilhali kile cha awali akiwa ameandika jina lake halisi na kukitelekeza akiwa ameacha begi lenye suruali na simu.
Uchunguzi ulipofanywa ilibainika yupo katika chumba kingine juu ghorofani. Alipofuatwa aligoma kufungua mlango akisema hadi awepo mwanasheria wake. Kweli, hakutoka kutwa nzima hadi mwanasheria alipofika. Katika kuonesha kuwa ana mtandao mpana, polisi walishindwa kufanya ukaguzi kwenye nyumba anazoishi baada ya amri kutoka kwa “wakubwa”.
Lakini si polisi tu bali hata kwa upande wa Uhamiaji taarifa za nyuma za Marc hazionekani, na kuna habari kwamba faili lake ama limepotea au limefichwa kwa makusudi. Marc ana mwanasheria wake anayemtetea katika masuala mengi, hasa ya ardhi katika Kijiji cha Nyarugusu. Mmoja wa mahakimu ambao husikiliza kesi hizo ni mke wa mwanasheria huyo.
Kinachotokea hapo ni kwamba inapoandaliwa kesi, wakili (mume) huandaa utetezi kwa mteja wake na kisha huipeleka iamuriwe na hakimu (mkewe). Matokeo yake ni kwamba mara zote wananchi wamekuwa wakishindwa katika kesi zao.
Kauli ya Uhamiaji
Uhamiaji kwa upande wao wanasema kwamba hati za kusafiria za Marc zinazosemwa kuwa ni mbili zilishamalizika muda wake. Wanasema hati ya Burundi yawezekana akawa nayo kwa sababu nchi hiyo inaruhusu uraia wa nchi mbili. Hata hivyo, Uhamiaji hawajui Marc mara ya kwanza aliingia nchini akiwa na hati ya kusafiria ya taifa gani!
Wanasema hawana ushahidi wa kujitosheleza wa kumchukulia hatua za kisheria, na kwamba wao kama Uhamiaji ni wa mwisho kuchukua hatua hasa kwa mtu aliyeingia nchini na kujitanabaisha kwa vibali kama mwekezaji. Inatisha!