Viongozi mbalimbali wa Ulaya wamefanya ziara nchini Marekani wiki hii ili kujaribu kuutafutia suluhu mzozo kati ya Urusi na Ukraine ambazo zimeendelea kushambuliana vikali.
Baada ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, jana ilikuwa zamu ya Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer ambaye amesema mkataba wa amani kuhusu mzozo wa Ukraine unapaswa kuwa wa kudumu:
“Mkataba huo lazima uwe wa kudumu. Lazima liwe jambo la kudumu. Na ili kulifanikisha hilo, kuna haja ya kuwa na nia ya dhati kutoka kwa Putin kwamba hawezi kukiuka mpango huo. Na ndio maana nimekuwa nikisema mara kadhaa kuwa, nadhani nchi za Ulaya, ikiwemo Uingereza, zinatakiwa kushirikishwa kikamilifu katika mchakato huo.”
Siku ya Ijumaa, Trump atampokea rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ambapo miongoni mwa mambo mengine kuhusu vita, watajadili namna ya kuiwezesha Marekani kupata madini adimu ya Ukraine.
Baadaye siku ya Jumapili, Waziri Mkuu huyo wa Uingereza ameandaa mkutano wa kilele na viongozi kadhaa wa Ulaya kutoka Ufaransa, Ujerumani, Denmark, Italia, Uholanzi, Norway, Poland, Uhispania, Finland, Sweden, Jamhuri ya Czech, Romania pamoja na Uturuki ili kuelezea aliyoyajadili na Trump na kujadili kuhusu usalama wa Ulaya.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Mark Rutte na mkuu wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen na rais wa Baraza Kuu la umoja huo Antonio Costa wamealikwa kwenye mkutano huo wa kilele mjini London.
