DAR ES SALAAM
Na Regina Goyayi
Miezi michache baada ya kifo cha Mbunge wa Muhambwe (CCM), Mhandisi Atashasta Nditiye, mapendekezo yake ya namna ya kuongeza mapato ya serikali yamefanyiwa kazi.
Mhandisi Nditiye, aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, alifariki dunia Februari 12, mwaka huu kwa ajali ya gari jijini Dodoma.
Siku tatu kabla ya kifo chake, yaani Februari 9, mwaka huu, Nditiye alitoa mapendekezo kadhaa bungeni mbele ya Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, akielekeza namna sahihi ya serikali kujiongezea mapato.
Mapendekezo yake yalikuwa namna ambavyo Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inavyoweza kuongezewa fedha na kujitegemea.
Sasa mawazo ya mhandisi huyo yameisaidia serikali kupanga kukusanya zaidi ya Sh bilioni 300 kuimarisha barabara katika kila kijiji! Nditiye alipendekeza zikusanywe Sh bilioni 120 tu.
Huu hapa mchango wake wa mwisho bungeni: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwapo kwenye Bunge letu tukufu, lakini niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Muhambwe kwa kuniwezesha kurudi mara ya pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajikita kwenye kitu kimoja tu ambacho ninapenda nikichangie kama kusaidia serikali yetu katika kuinua kipato.
Hivi karibuni Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba hii ambayo mimi binafsi naiona ni nzuri sana, kumekuwa na maelezo mengi sana ya waheshimiwa wajumbe na wabunge kwa ujumla kuelezea jinsi ambavyo wamekuwa hawaridhiki na fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya TARURA na wakawa wanapendekeza kwamba sasa tuangalie uwezekano wa kuhakikisha tunachukua fedha kutoka TANROADS.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninataka nitoe ushauri. Kwanza kabisa, hakuna kosa kubwa tutakalofanya kama tutajaribu kuondoa hiki kidogo ambacho wanacho TANROADS kwa njia yoyote ile.
Isipokuwa kitu ambacho tunaweza kukifanya, Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kuhakikisha tunatafuta vyanzo vizuri na sahihi kwa ajili ya TARURA. Tunajua umuhimu wa TARURA kwa barabara zetu kuanzia vijijini mpaka barabara kuu na tunajua jinsi wanavyojitahidi. Ukweli ni kwamba, bajeti yao ni ndogo.
Mimi, Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona nije na mpango na niutoe kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, auangalie kama utafaa.
Mwaka jana kipindi kama hiki nilihudhuria Kamati ya Bunge ya Bajeti na nikaitoa kama proposal ni jinsi gani tutaitumia sekta ya mawasiliano kuhakikisha tunapata fedha za kutosha kuwasaidia TARURA kufanya shughuli zao kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi hicho ambacho bado ninasimamia kwenye wazo langu hilo, tuliwapendekezea watu wa Wizara ya Fedha kwamba, tuzungumze na kampuni za simu; tuweke tozo kidogo kabisa ambayo itawezesha TARURA kupata fedha.
Tukawapa pendekezo na nitaomba Mheshimiwa Mwenyekiti tulisikilize kwa makini.
Tuliwaelekeza, tukawaambia, bwana, tukiweka senti 25 kwa kila megabyte moja; sasa hivi Watanzania wanaosajiliwa kwa kutumia laini za simu wako milioni 50; na kati ya watu milioni 50, kati ya watu milioni 24, wamesomeka kuwa wanatumia mitandao ya internet kwa njia na shughuli mbalimbali.
Mimi nikasema, tuchukue tu sampuli ya watu milioni 10, tusichukue watu mlioni 24. Tuchukue watu milioni 10 ambao wanatumia internet.
Nikasema tuweke tozo ya senti 25. Tusifike hata senti moja! Tuweke senti 25 kwa kila megabyte moja.
Nikasema kwamba kwa gigabyte moja ambayo ni megabyte 1,000, tukiweka hapo senti 25 tutakuwa tumechangia serikali Sh 250 kwa gigabyte moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikaenda mbali zaidi na nitaleta hiki kitu kwa maandishi. Najua itaisaidia serikali.
Kwanza kabisa, niwahakikishie serikali tusiwe waoga. Hizo kampuni za simu zimekuwa na ushirikiano mkubwa sana na serikali.
Zinachangia sana kwenye serikali na hawawezi kulalamika. Isitoshe hakuna bei elekezi ya mtandao mmoja kwenda mtandao mwingine kutoa huduma kwa wateja wake!
Tukitumia watu milioni 10 ambao kila mmoja anatoa Sh 250, tunaweza kusema kwa wiki moja; tuchukulie tu kwamba wiki moja mtu atatumia gigabyte moja. Tutakuwa tumetengeneza Sh bilioni 2.5!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipiga hiyo hesabu kwa muda wa mwezi mmoja ni Sh bilioni 10. Kwa mwaka mzima, Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Sh bilioni 120.
Kwa bajeti ya Sh bilioni 273 ya TARURA tutakuwa tumewaongezea kiwango fulani cha fedha.
Kwa kufafanua, ninapendekeza mteja ndiye awe anakatwa senti 25 halafu kampuni waipeleke serikalini kama fedha ya serikali.