Wakati Taifa likifikisha miaka 16 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, watu mbalimbali wanaendelea kumkumbuka Rais huyo wa kwanza na muasisi wa Taifa letu, kulingana na kila mmoja alivyomjua.
Lakini mengi ya yanayotajwa kwa Nyerere ni yale ambayo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara kupitia kwenye vyombo vya habari, magazeti, luninga na redio.
Katika kulikwepa jambo hilo nimemtafuta mtu aliyekuwa karibu sana na Mwalimu Nyerere kwa muda mrefu, ili naye ajaribu kunieleza alivyomjua Mwalimu na pia kunieleza yale ambayo walau ni tofauti na niliyoyazoea kuyasikia. Naye huyo si mwingine bali ni Mzee Abdallah Chasamba.
Mzee Abdallah ni mtu mzima mwenye umri wa miaka 79 kwa sasa, ambaye kwake ni Tabata karibu na Hai Bar, Dar es Salaam.
Nimepanga naye miadi ili akanieleze kuhusu alivyoishi na Baba wa Taifa wakati tunatimiza miaka 16 ya kifo chake, akanikubalia bila matatizo yoyote. Nimeenda na kumkuta nyumbani kwake akiwa amejaa furaha ya kusimulia anavyomwelewa Nyerere.
Katika masimulizi yake, ameanza kwa kunieleza historia kidogo juu ya maisha yake. Anasema alizaliwa mwaka 1936 katika Kijiji cha Mungugo, Mikese, mkoani Morogoro.
Anasema yeye alikuwa mtu wa 305 kupata kadi ya TANU mkoani Morogoro, mwaka 1955. Kwa hiyo, anajitambulisha kuwa yeye ni kati ya waasisi wa chama hicho kilichopigania uhuru wa nchi yetu. Anaongeza kuwa kadi yake ya TANU alitafutiwa na baba yake mzazi, marehemu Mwinjuma Chasamba.
Mwaka 1958 alitoka Morogoro kwenda Dar es Salaam kufanya kazi za kujitolea katika Umoja wa Vijana wa TANU, uliokuwa ukijulikana kama TANU Youth League. Lakini kwa vile ile ilikuwa kazi ya kujitolea, ilibidi atafute kibarua alichokipata kwenye duka moja la Mzungu, Smith McKenzie, lililouza vitenge katika Mtaa wa Samora ukijulikana kama Acacia Street wakati huo.
Baada ya uhuru, mwaka 1962 Mzee Abdallah aliachana na Smith McKenzie aliyehamia Nairobi, Kenya, wakati yeye akigoma kuambatana naye kule. Ndipo alipoungana na vijana wengine kwenda ‘Labour’ sehemu ya kutafuta ajira, kwa ajili ya kutafuta kazi.
Wakiwa pale, Mzee Abdallah akamuonesha Mnikulu wa kwanza wa Ikulu, Ramadhani Kingo, barua yake aliyoandikiwa na mwajiri wake, Smith McKenzie, kuhusu utendaji wake wa kazi. Kingo akaipenda akamwambia apande gari waende Ikulu.
Baada ya mahojiano ya muda mfupi wakiwa ofisini kwa Kingo, Ikulu, Mzee Abdallah akapewa kazi siku hiyohiyo pale Ikulu. Majukumu yake ya kwanza aliyokabidhiwa yalikuwa ni ya kukiangalia na kukitunza chumba namba 7 ambacho kilikuwa ni kwa ajili ya wageni.
Mzee Abdallah anaeleza kwamba baada ya muda mfupi alipelekwa pale babu yake Rais Kikwete, Mzee Ramia, kutoka Bagamoyo, aliyekuwa anaumwa. Eti alikaa naye kwa wiki mbili akimhudumia kwenye chumba hicho.
Eti wakati akimuangalia Mzee Ramia kwenye chumba hicho, kila siku Mwalimu Nyerere alikuwa akienda kumjulia hali mzee huyo kabla ya kuingia ofisini na baada ya kutoka ofisini. Eti huo ukawa ndiyo mwanzo wa Nyerere kumfahamu na kumzoea Mzee Abdallah.
Anasema kwamba kipindi hicho walichukuliwa vijana wengi waliokuwa wameajiriwa serikalini kwenda kwenye mafunzo ya JKT kwa miezi mitatu naye akiwa mmoja wao. Walipelekwa kwenye Kambi ya Ruvu.
Gwaride la kufunga mafunzo yao lilikaguliwa na Amiri Jeshi Mkuu, Mwalimu Nyerere. Wakati Nyerere anakagua gwaride hilo akamuona Mzee Abdallah, akaamua kumuita “Abdallah kumbe na wewe uko huku! Hujambo?”
Eti Mzee Abdallah akaangalia mbele mita 100 bila kumjibu lolote Nyerere, kama walivyofundishwa kwenye mafunzo hayo ya kijeshi.
Baada ya hapo ndipo Nyerere akasema kweli kijana huyu kaiva. Hiyo ilikuwa mwaka 1963. Baada ya Nyerere kurudi Ikulu akamwambia mnikulu kwamba “Kijana yule aliyekuwa anamwangalia Mzee Ramia akirudi kutoka JKT nataka niwe naye Msasani.” Huo ukawa ndiyo mwanzo wa Mzee Abdallah kuwa na Mwalimu muda wote wa utumishi wake serikalini.
Mzee Abdallah anasema majukumu yake yalikuwa ni kuangalia na kukagua mazingira ambayo alikuwa Nyerere anafikia – hapa nchini na nje ya nchi – kuanzia vyumba vya kulala ikiwa ni pamoja na chakula alichopaswa kula Nyerere.
Anasema watu wengi waliamini kwamba yeye alikuwa ni mpishi wa Nyerere, lakini ukweli ni kwamba haikuwa hivyo, yeye hakuwa mpishi ila kukagua wapishi wametayarisha nini kwa ajili ya Mwalimu.
“Nilikagua pia kinywaji alichokitumia Mwalimu hata na malazi yake pia,” anaongea Mzee Abdallah.
Mzee huyo anasema kwamba alikuwa akiambatana na Nyerere kila mahali alipotembelea, ndani na je ya nchi.
Zaidi anachokikumbuka Mzee Abdallah ni kwamba kwa muda wote aliokaa na Nyerere hakuwahi kumuona akipata msukosuko wa kiafya wa kumfanya alazwe hospitalini, anasema alikuwa akipata homa za kawaida tu na kupatiwa vidonge na baadaye kuwa katika hali yake ya kawaida.
Ila anasema kwamba tukio pekee la kiafya lililompata Mwalimu ni la mwaka 1977, ambako walikwenda Arusha kwa ajili ya sherehe za kitaifa na kesho yake, Februari 5 ndiyo uliokuwa uzinduzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika Zanzibar.
Anaelezea kwamba kama ilivyokuwa kawaida, katika Hoteli ya Mount Meru, Arusha, alikagua chakula akagundua kwamba kulikuwa na kitoweo aina ya kamba ambao alipowaonja, hakuipenda ladha yake.
Hivyo, akamtahadharisha Mwalimu kuwa kamba hao asiwaguse. Lakini eti katika kupakua chakula, aliyekuwa Rais wa Zambia, Kenneth Kaunda, alikuwa amemtangulia Nyerere, akawaona kamba na kupakua kisha akamsogezea Nyerere naye apakue, eti Nyerere akashindwa kukataa ikambidi naye apakue wale kamba.
Mzee Abdallah anasema baada ya kufika Zanzibar siku hiyo jioni tumbo lilimsumbua sana Mwalimu kiasi kwamba alishindwa hata kusimama. Ndipo yeye Mzee Abdallah akawaambia watu wa usalama wakamwambie rafiki yake, Rais Kaunda, aliyekuwa ghorofa ya juu ya pale walipokuwa wao, kwenye hoteli moja.
Rais Kaunda akaenda na daktari wake aliyeweza kumsaidia Nyerere, baada ya daktari wa Nyerere kuwa amehangaika sana bila nafuu yoyote kujitokeza.
Kuhusu uvaaji wa Nyerere, Mzee Abdallah anasema kwamba Mwalimu alikuwa na jozi sita za viatu, suti tatu za kimao, au vazi la kitaifa, za mikono mirefu ambazo alipendelea kuzivaa kwenye shughuli maalum au kwenye safari za nje ya nchi, na nyingine tatu za mikono mifupi ambazo alikuwa anapendelea kuzivaa kwa shughuli za ndani ya nchi.
Mzee Abdallah anakumbuka kwamba mwaka 1977 Mwalimu alikuwa na ziara nchini Uingereza, wakati yeye amepumzika hotelini walikofikia, yeye Mzee Abdallah na Mzee Joseph Butiku wakaenda madukani.
Kule akaona suti nzuri aina ya Kaunda, akamwambia Mzee Butiku kwamba hii tukimchukulia Mwalimu anaweza kuipenda. Mzee Butiku akamwambia ‘mchukulie wewe maana mnaelewana zaidi’.
Akainunua suti hiyo rangi ya maziwa, akampelekea Mwalimu na kumuomba aijaribu. Eti alipompa suti hiuyo, Mwalimu Nyerere akasema “Abdallah bwana, ngoja nijaribu”.
Baada ya kuivaa ikawa imemkaa vizuri sana, ndipo Mwalimu akamwambia akamchukulie nyingine. Na huo ukawa mwanzo wa Mwalimu kuvaa Kaunda Suti akichanganya na vazi la kitaifa.
Hicho ni kitu ambacho Mzee Abdallah anajivunia kuwa mwanzilishi wa vazi hilo ambalo Mwalimu alilipenda sana.
Mzee Abdallah anasema kwamba Mwalimu aliishi maisha ya kawaida sana nyumbani kwake, anasema mbali na wanafamilia wake, yeye kwake kila Mtanzania alimuona kama mwanafamilia.
Anasema yeye Mzee Abdallah hakutokana na ukoo wa Nyerere, lakini Nyerere alimuingiza kwenye ukoo huo na kumfanya mmoja wa watoto wake wa kuwazaa!
Pia Nyerere alimfanya mama yake mzazi, Bibi Mugaya Nyang’ombe, amchukulie Mzee Abdallah kama mjukuu wake. Pia dada zake Nyerere, Nyangeta, Nyakiki na wengineo walimuona Mzee Abdallah kama mwana wao sawa na walivyowaona kina Makongoro na wengine.
Anakumbuka kwamba wakati fulani alimshauri Mwalimu awapeleke baadhi ya watoto wake nje ya nchi, hasa China, ili wakawe katika mazingira tofauti na ya hapa nyumbani katika kuwafanya wajikite kwenye masomo.
Mwalimu aliukubali ushauri huo na baadaye akawa anamshukuru kwa wazo hilo sababu waliopelekwa kule walifanya vizuri katika fani ya kurusha ndege za kijeshi.
Jambo ambalo Mzee Abdallah anasema hawezi kulisahau ni la Nyerere kumsaidia kupaka makazi yake. Anasema kiwanja alikojenga nyumba yake alikipata kwa msaada wa Bi Bernadeta Kunambi, aliyekuwa mkuu wa Wilaya wa Ilala.
Yeye alinunua mifuko 25 tu ya saruji, alipomwambia Mwalimu kuhusu hatua hiyo, Mwalimu akamueleza kwamba aishie hapo alipofika, kazi iliyobaki ni ya kwake (Mwalimu). Mzee Abdallah anasema, “Ndiyo nyumba hii unayoiona.”
Kuhusu mabadiliko yanayoendelea nchini, Mzee Abdallah anasema hilo Mwalimu alilipenda. Kwa mfano, Nyerere alianza akiwa mpenzi wa suti za Kiingereza, baadaye akabadilika na kuwa mpenzi wa vazi la kitaifa, baadaye Kaunda suti. Hiyo yote ni kuonesha jinsi Nyerere alivyokuwa mpenzi wa mabadiliko. Ila Mzee Abdallah anasema mabadiliko hayo yawe ya heri.
Eti, ili mabadiliko yawe ya heri, hapana budi yawepo mazingira ya kuyakubali mabadiliko husika sawa na mazingira yaliyotengenezwa wakati tunadai uhuru wetu na kutufanya kuupata uhuru huo bila kumwaga damu.
0784 989 512