Katibu Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Walimu, Winifrida Rutaindurwa ametoa onyo kwa Walimu wanaowaadhibu wanafunzi bila kuzingatia Sheria Kanuni na Taratibu zinazotoa mwongozo wa aina, kiwango na namna adhabu inavyotakiwa kutolewa kwa wanafunzi.
Amesema kuwa kutoa adhabu ya viboko kwa wanafunzi bila kuzingatia taratibu zinazohusika sio tu kwamba inaleta athari kwa wanafunzi wanaoadhibiwa, bali inaweza kusababisha chuki kati ya wazazi na walimu.
Ameeleza kuwa Tume ya Utumishi wa Walimu imesikitishwa na tukio la hivi karibuni lililoripotiwa kwenye vyombo vya habari juu ya Mwalimu Respecious Patrick wa Shule ya Msingi Kibeta, Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera anayedaiwa kumwadhibu mwanafuzi Sperius Eradius, ambapo mwanafunzi huyo amefariki dunia.
“Mwalimu ni mlezi na kwa mujibu wa kuu tano za maadili ya ualimu, mwalimu ana wajibu wa kumlea mwanafunzi kimwili, kiakili na kiroho. Sasa mwalimu anapogeuka na kuwa tishio kwa wanafunzi ni jambo la kusikitisha ambalo hatuwezi kulifumbia macho wala kulivumilia hata kidogo” alisema.
Amefafanua kuwa, uongozi wa shule una jukumu la kusimamia nidhamu ya Walimu pale shuleni kwani Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu inamtambua Mwalimu Mkuu/Mkuu wa Shule kuwa ni mamlaka ya kwanza ya nidhamu kwa mwalimu.
“Kwanza nimejiuliza, hadi huyu mwalimu anafikia huko kuna uwezekano mkubwa amekuwa na tabia ya kuwaadhibu wanafunzi kupita kiasi na alipaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu huko nyuma kabla ya kusababisha madhara makubwa hivi,” amesema.
Ameongeza, “Nimeshindwa kuelewa inawezekanaje mwalimu anafanya tukio la kumpiga mwanafunzi kiasi hicho na walimu wengine wapo na hakuna jitihada wanazofanya kumsaidia mwanafunzi.”
Amemwagiza Kaimu Katibu Msaidizi wa Wilaya ya Bukoba kuangalia taratibu za kufuata kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Na. 25 ya mwaka 2015 ili kama yatabainika masuala yanayohitaji kuchukuliwa hatua za kidnidhamu kwa walimu wa shule hiyo sheria ichukue mkondo wake.
Mwongozo wa kutoa adhabu mashuleni umetoalewa chini ya kifungu cha 61 (1) (v) cha Sheria ya Elimu sura ya 353 marejeo ya mwaka 2002 ambapo kinampa Mamlaka Waziri wa Elimu kutunga kanuni za Masuala mbalimbali zitakazokidhi utekelezaji wa utekelezaji wa masuala ya Sheria hiyo.
Miongoni mwa kanuni zilizotungwa ni The Education (corporal Punishment) Regulation G. N. 294 ya mwaka 2002. Kanuni hizi zinatoa mwongongozo ni wakati gani adhabu ya viboko inatakiwa kutolewa na kwa kiwango gani.
“Kanuni ya 3 (1) inasema adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhamu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima. Kanuni ndogo ya (2) inasema adhabu ya Viboko itatolewa kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi na isizidi viboko vinne (4) kwa tukio lolote,” alisema.
Sheria inamtaka mwalimu mkuu au mkuu wa shule kutoa adhabu ya viboko au kukasimisha mamlaka yake kwa mwalimu yeyote kutekeleza adhabu hiyo.
Kwa mujibu wa kanuni hiyo, kila adhabu ya viboko inapotolewa kwa mwanafunzi ni lazima mwalimu aweke kumbukumbu kwenye kitabu ikitaja jina la mwanafunzi, kosa alilolifanya, idadi ya viboko pamoja na jina la mwalimu aliyetoa adhabu na kumbukumbu hizo zinatakiwa kusainiwa na mwalimu mkuu au mkuu wa shule.
Ni wajibu wa walimu kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za utumishi wao ili kuleta ustawi mzuri kwa wanafunzi wanaowafundisha.
Adili Mhina,
Afisa Mawasiliano,
Tume ya Utumishi wa Walimu.
30/08/2018.