Na Charles Ndagulla, Moshi

Mfanyabiashara Bosco Kyara na mwenzake
Gabriel Mombuli, wanaotuhumiwa
kujihusisha na mtandao wa wizi wa magari
katika nchi za Kenya na Tanzania
wamesafirishwa kwenda nchini Kenya
kujibu mashtaka ya wizi wa gari.
Kyara ni mkazi wa Makuyuni katika Mji
Mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi Vijijini,
wakati Mombuli ambaye anafanya shughuli
za udereva, anaishi eneo la Majengo Shauri
Moyo katika Manispaa ya Moshi, mkoani
Kilimanjaro.
Kabla ya kusafirishwa kwenda nchini
Kenya, watuhumiwa hao walifikishwa katika
Mahakama ya Wilaya ya Hai na kusomewa

mashtaka mawili likiwamo la unyang’anyi
wa kutumia silaha na kupatikana na mali
inayoaminika kuwa ni ya wizi.
Katika shtaka la kwanza, ilidaiwa kuwa siku
na muda usiojulikana mwaka huu huko
Nairobi nchini Kenya, washtakiwa waliiba
gari aina ya Nissan V8 lenye namba za
usajili KCP 184R mali ya Kampuni ya Nisk
Capital Limited.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka
iliyosomwa mahakamani hapo na
Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi wa Polisi,
Hawa Hamis, washtakiwa hao kabla na
baada ya kuiba gari hilo walimtishia kwa
bastola Luke Indechi Abboo.
Shtaka la pili ni washtakiwa hao kupatikana
na mali inayoaminika kuwa ya wizi, ambapo
Agosti 19, mwaka huu saa 1:30 usiku katika
kizuizi cha Polisi eneo la Kwa Msomali,
Wilaya ya Hai walikutwa na gari aina ya
Nissan Patrol V8 lenye thamani ya Sh
milioni 200 mali ya Kampuni ya Nisk Capital
Limited ya Kenya.
JAMHURI limebaini kuwa washtakiwa hao
walichukuliwa na polisi wiki iliyopita kutoka

Gereza Kuu la Mkoa wa Kilimanjaro,
Karanga na kupelekwa mahakamani
ambako walifutiwa mashtaka na
kusafirishwa kwenda nchini Kenya kupitia
mpaka wa Tarakea.
Wakili Julius Semali aliyekuwa akimtetea
mfanyabiashara Bosco Kyara, amelalamikia
hatua iliyochukuliwa na polisi ya
kuwasafirisha washtakiwa hao kwenda
nchini Kenya bila kufuata taratibu za
kisheria.
“Nilipata taarifa kutoka kwa mke wake
(Haika), aliniambia wamenyakuliwa na
kupelekwa Kenya, walipelekwa
mahakamani polisi wakafuta jalada na
kuwapeleka pale Tarakea na kuwakabidhi
kwa askari wa Kenya,

” amesema Wakili

Semali.
Amesema yeye kama wakili aliyekuwa
akimwakilisha mshtakiwa hakushirikishwa
kwa namna yoyote na kwamba tayari
amewasilisha barua ya malalamiko ofisi ya
Wakili wa Serikali mjini Moshi kwa kile
alichodai taratibu za kisheria hazikufuatwa.
Kwa mujibu wa wakili huyo, katika

kubadilishana wahalifu wa makosa ya jinai
kati ya nchi na nchi, Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali ingeshirikishwa pamoja na
yeye kama wakili anayemwakilisha
mshtakiwa huyo lakini hilo halikufanyika.
Amesema tukio la mteja wake kupelekwa
Kenya bila tararibu za kisheria kufuatwa
limemuumiza, huku akidai hawezi
kulisemea kwa kuwa tayari jambo hilo
limeshafanyika na sasa wanachosubiri ni
kauli kutoka ofisi ya Wakili wa Serikali.
Tangu kufikishwa mahakamani hapo kwa
washtakiwa hao, upande wa mashtaka
ulikuwa ukisisitiza kuwa zipo taratibu za
kisheria zinazopaswa kufanyika washtakiwa
wasafirishwe kwenda nchi nyingine kujibu
mashtaka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro,
Hamis Issah, amethibitisha kusafirishwa
kwa watuhumiwa hao kwenda nchini Kenya
huku akiwataka wanaohoji mazingira ya
kusafirishwa kwao wawasiliane na Mkuu wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO)
kupewa ufafanuzi.
Kamanda Issah amesema mbali na

watuhumiwa hao kukabidhiwa kwa polisi wa
Kenya, gari aina ya Nissan Patrol V8 lenye
namba za usajili KCP 184R ambalo
lilikamatwa mikononi mwa watuhumiwa hao
nalo limerejeshwa nchini Kenya.

MWISHO…