Wananchi wameitikia mwito wa ulipaji kodi kwa mujibu wa sheria.

Kwa namna ya pekee, mamia kwa mamia ya wananchi wameonekana katika ofisi za Serikali za Mitaa na Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) nchini kote wakiwa kwenye misururu kwa lengo la kulipa kodi mbalimbali.

Hii ni ishara nzuri yenye kuonesha namna Watanzania wanavyoanza kujenga utamaduni wa kulipa kodi bila shuruti.

Pamoja na mwitikio kuwa mkubwa, bado imeonekana mamlaka zinazohusika ni kama hazikutarajia au hazikujipanga kuhudumia wingi huu wa walipa kodi.

Katika hali ya kusikitisha, baadhi wameonekana wakiwa, ama wameketi kwenye mawe, au wamesimama katika jua mithili ya hali inavyokuwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wakisubiri zamu ya kulipa kodi.

Sisi tunaamini kuwa huu si utaratibu mzuri. Mlipa kodi ni mtu muhimu kwa maendeleo ya Taifa, kwa hiyo ni vema mamlaka zinazohusika zikajiandaa kuwawekea mazingira mazuri ili wanapoamua kwenda kulipa kodi wasikwazwe na adha za kusimama juani au kukosa sehemu za kuketi.

Walipa kodi sharti wapokewe kwa bashasha na wanyenyekewe kwa sababu kitendo wanachofanya ni cha kizalendo na chenye kuibadili nchi yetu kutoka kwenye maendeleo duni. Waandaliwe mazingira mazuri ya kuwafanya wajione fahari kwenda kulipa kodi ikiwa ni pamoja na kupokewa kwa ukarimu.

Hata hivyo, tunaamini kuwa mafanikio haya ya ulipaji kodi yatakuwa na maana tu pale ambako matumizi ye fedha hizi za umma yatakaposimamiwa vizuri na kuleta tija iliyokusudiwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Kwa miaka mingi wananchi wamevunjika moyo kwenye ulipaji kodi kwa sababu wamekuwa hawaridhishwi na matumizi na thamani ya kile kinachotokana na hizo kodi.

Kwa mfano, miaka michache iliyopita fedha za umma zilitumika kujenga barabara nyingi wilayani Kinondoni, lakini ajabu ni kwamba kabla hata ya uzinduzi, barabara hizo zikawa na mashimo makubwa mno. Nyakati za mvua hazipitiki. Haya ndiyo yanayowatia hasira wananchi hata kuwafanya wasite kulipa kodi.

Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kodi zinatumiwa kuwaletea maendeleo ya kweli badala ya kutumiwa na wezi na mafisadi wachache kujinufaisha.

Endapo wananchi wataanza kuona matunda, tunaamini kasi ya wananchi kujitokeza kulipa kodi itakuwa kubwa zaidi na bila shaka yoyote nchi yetu itaingia kwenye orodha ya kupigiwa mfano mzuri.

Pia Serikali ione njia nzuri ya kupunguza utitiri wa kodi na viwango vyake kwani navyo vimekuwa kero kubwa.

Hongereni wananchi kwa kuitikia ulipaji kodi, lakini pia ni wajibu wa Serikali kuhakikisha fedha zinazokusanywa zitatumika kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wote.