*Ajibu maswali magumu ya waandishi, afanya uamuzi mgumu kwa ujasiri
*Afafanua uchumi wa bluu, awatoa wasiwasi wakaazi nyumba za maendeleo
*Akabidhi visiwa 10 kwa wawekezaji, wanaoatamia ardhi kunyang’anywa
*Asema mawaziri wanaoogopa waandishi inaashiria hawajafanya lolote
Na Deodatus Balile, Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, amefanya mabadiliko makubwa ya uendeshaji wa taifa la Zanzibar, mabadiliko ambayo yameanza kubadili sura ya Zanzibar, ukiwamo mwelekeo mpya wa uchumi wa bluu, JAMHURI limebaini.
Katika hali isiyo ya kawaida, Rais Mwinyi amejibu maswali ya waandishi wa habari bila kuyachuja na kama kawaida yake, kwenye mkutano na waandishi wa habari alifika yeye mwenyewe bila kuambatana na msururu wa mawaziri au watendaji wakuu wa serikali kama ilivyoanza kujengeka kwa watangulizi wake miaka iliyopita.
JAMHURI lilikuwa la kwanza kupewa fursa ya kuuliza maswali, ambapo Mwandishi wa Habari hii aliuliza maswali manane ya utangulizi, kisha Rais Mwinyi akayajibu yote kwa ufasaha. Maswali hayo yalikuwa hivi:-
1. Kuna taarifa kuwa Kampuni ya DNATA imepewa kuendesha Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume. Hii ni kampuni ya kigeni. Ni sifa zipi inazo zilizofanya ipewe jukumu hili?
2. Kuna taarifa kuwa vipimo vya Covid Test vinafanywa na kampuni binafsi badala ya serikali? Je, kwa nini vipimo vinafanywa na sekta binafsi na si serikali?
3. Kuna taarifa kuwa barabara za ndani ujenzi wake umetolewa kwa mkandarasi bila ya zabuni/tenda. Je, hili imekuwaje likatokea?
4. Kuna taarifa kuwa visiwa viwili vidogo vidogo vya Zanzibar vimetolewa kwa wawekezaji. Unalizungumziaje hili?
5. Kuna taarifa kuwa nyumba za Mji Mkongwe zitahamishwa umiliki na kutolewa kwa wawekezaji. Unawaambia nini Wazanzibari kuhusu taarifa hizi zilizozagaa?
6. Tumepata taarifa kuwa viwanja ambavyo havijaendelezwa utawanyang’anya watu na kuwapa wawekezaji. Hili limekaaje?
7. Nyumba za Maendeleo Michenzani na Kilimani, kuna taarifa kuwa zitavunjwa na wakaazi sasa wataanza kulipishwa kodi. Hili limekaaje?
8. Karibuni Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetangaza kuwa itaanza kuchimba mafuta. Je, imejiandaaje kuhakikisha ina-process mafuta hadi kupata finished product (petroli, mafuta ya taa na dizeli) badala ya kupeleka nje mafuta ghafi hivyo kupoteza ajira na fedha nyingi?
Rais Mwinyi amejibu maswali haya moja baada ya jingine, kama ifuatavyo:
Kampuni ya DNATA
“Huduma za uwanja wa ndege ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi kama yetu ambayo inategemea utalii. Unapokuwa na uwanja wa ndege ambao mtalii akifika anakuta kwenye uwaja wa ndege kuna kero nyingi, basi mtalii huyo kumpata tena si rahisi. Mtalii anakuta kuna foleni, kupata visa. Mtu wa visa anampa namba anamwambia akalipe benki, akimaliza aende kwenye kipimo cha Covid, akutane na foleni, arudi kwenye mizigo, anakaa anasubiri mzigo.
“Watalii walikuwa wanakaa kwenye uwanja wa ndege zaidi ya saa tatu. Tukaona hii si sawa, tukasema huduma zitolewe na kampuni zenye uwezo na uzoefu. Kampuni hii inaendesha Dubai Airport na wapo katika nchi nyingine 26,” amesema na kuongeza kuwa Kampuni ya Emirates wameungana nayo kuendesha biashara ya duty free.
“Kwa nini DNATA, kwa sababu ya uwezo wao,” amesema na kuongeza kuwa kwa sasa kampuni zinazotoa huduma katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar zinatoa asilimia 5 serikalini, ilhali Kampuni hii ya DNATA imekubali kutoa asilimia 12. “Ni moja ya kampuni za kimataifa,” amesisitiza. Amesema mchakato umechukua zaidi ya miezi sita kuipata kampuni hii kupitia kwenye Kamati ya Majadiliano ya Serikali (Government Negotiating Team), hivyo si kweli kuwa imepatikana bila kufuata utaratibu. Anaongeza kuwa waliamua wachukue kampuni inayotambulika kuepusha watu kushuku iwapo wangechukua kampuni zisizofahamika vizuri.
COVID kampuni binafsi
Akijibu swali la Uviko-19 kupimwa na kampuni binafsi, Rais Mwinyi amesema: “Kuna wakati ilichukua hadi siku nne mtu hajapata taarifa za kipimo cha COVID. Kwa sasa kila mgeni anatoa sifa. Majibu yanatoka ndani ya saa 24. Kutoka siku 4 hadi saa 24. Ukitaka ufuatwe hotelini unafuatwa huko huko. Wapo waliotaka kuifanya kazi hii wakasema tutaipa serikali dola 10, wao wachukue 70. Kampuni hii inaipa serikali dola 50, wao wanachukua 30. Ufanisi upo ndani ya saa 24. Tukasema dola 50 hii ikaimarishe huduma za afya. Tunanunua dawa kutokana na fedha hizi. Tunanunua vifaa kwa fedha hizi.”
Barabara
Amesema wanaolalamika anataka waelewe kuwa kuna barabara za aina tatu; ambazo ni:- Barabara kubwa, Barabara za Vijijini na Barabara za Ndani (Feeder Roads). Amesema kwa hizi feeder roads, kuna kampuni ambazo zimegundua utaalamu wa kisasa unaowezesha kujenga barabara kwa gharama ndogo zikadumu kwa muda mrefu. Anasema badala ya kila mwaka kujenga barabara kwa kifusi na kisha kikasombwa na mvua, ni bora kujenga barabara za lami kwa teknolojia mpya ya bei nafuu inayodumu muda mrefu.
“Matokeo yake ni kama unapoteza fedha. Unaweka kifusi leo, msimu ukiisha mvua inaosha. Barabara ya lami ya kawaida, kilomita moja USD 1m, hizi za ndani kilomita moja inajengwa kwa dola 300,000. Kwenye tenda tumetumia mfumo wa EPC + Finance. Hii maana yake ni Engineering, Procurement and Construction + Finance. Mtu akileta fedha zake, utampeleka kwenye tenda? Mjenzi akija na fedha zake unafanya naye negotiation juu ya mkopo, interest rate, tutalipa kwa muda gani. Hatimaye, wamepewa barabara. Tunajenga feeder roads za lami kwa mara ya kwanza [hapa Zanzibar].
Visiwa kwa wawekezaji
“Zanzibar ni nchi ya uwekezaji. Kuna hoteli 600, si wote wanaokaa kwenye fukwe. Lazima tuendelee kujenga hoteli. Tuna visiwa 52. Tutaendelea kuviacha tu kwa faida ya nani? Tumeamua vitolewe kwa wawekezaji wenye uwezo. Na wala si bure, wanavilipia. Visiwa tumepata dola milioni 3 mwanzo, mtu anaweka hoteli anaweka watalii. Vikae bure kwa miaka yote kwa faida ya nani?
“Tumetoa visiwa 10 katika 52, na tutaendelea kuvitoa. Ukienda Thailand, huko Malta, watu wanajenga kwenye visiwa na utalii ni mkubwa,” amesema Rais Mwinyi na kuongeza kuwa Zanzibar itanufaika kwa kiasi kikubwa na ukodishaji wa visiwa hivi kwa wawekezaji. Amesisitiza kuwa fukwe zitaendelea kuwa mali ya umma na wananchi watakuwa huru kwenye fukwe za visiwa hivi kuogelea au kupita bila kuzuiwa na mwekezaji yeyote.
Majengo ya Mji Mkongwe
“Zile ni nyumba za zamani sana. Sisi tunajivunia urithi wa kale. Zanzibar ni tofauti, kuna utalii wa fukwe na utalii wa kihistoria. Wanaosema majengo ya Mji Mkongwe yasiguswe, wanataka yaendelee kuanguka? Serikali imeamua majengo haya yatunzwe kama sisi tulivyoyakuta… kuna majengo kadhaa yameanguka kabisa. Maamuzi ni kuyatoa kwa wawekezaji wayawekeze yaendelee kudumu zaidi. Na tunasema wale wanaokaa katika majengo yale, kama wana uwezo wayatengeneze waendelee kuyatumia.
“Wasioweza, tunasema wayatoe kwa mwekezaji. Tutahakikisha yule anayetoka anakwenda kupata makazi mazuri. Tunataka Mji Mkongwe barabara zitengenezwe, tuweke taa… Mji Mkongwe Majengo sasa yajengwe kuwe kuna hoteli, kuwe kuna makazi. Asiye na uwezo ahamishwe, nia ni njema kabisa,” amesema na kuongeza kuwa serikali inataka kuhakikisha historia ya majengo haya inatunzwa badala ya kuachwa yakaendelea kuanguka kama ilivyo sasa.
Viwanja
“Serikali imeamua. Kuna watu wengi waliopewa viwanja, wameviacha miaka na miaka. Tunawapa mwaka mmoja. Kama mtu alipewa hajawekeza, kinarudi serikalini. Siyo kushika watu wakasubiri. Kila siku tunapokea wageni wanataka kuwekeza kweye mahoteli, watu wameatamia ardhi. Waliopewa viwanja tunawapa miezi sita kama ni wageni, baada ya miezi sita, kama hajaendeleza tunavichukua.
“Serikali haina nia ya kuwanyang’anya wazawa. Wao ni Wazanzibari, kama hawana uwezo wa kujenga chochote, wanapewa mwaka mzima kujenga. Serikali iko tayari kuwaunganisha na wawekezaji, lengo na madhumuni watu wawe na fedha,” ameongeza kuwa serikali haiwezi kuacha viwanja vikaendelea kuwa vimezungukwa na kuta bila kuendelezwa. Amesisitiza ikipita miezi sita kwa wageni bila kuendelezwa vinachukuliwa na kwa wazawa ukipita mwaka mmoja bila kuviendeleza itabidi waione serikali iwaunganishe na wawekezaji viendelezwe.
Nyumba za Maendeleo
“Nyumba za maendeleo hizi, kuna wakaazi wa aina tatu. Wapo waliopewa apartment kama fidia, hawa hawatakiwi kulipa kodi, ni fidia. Wengine walipewa kwa sababu ya nyadhifa zao, yule aliyepewa ataendelea kukaa hadi akifariki, mke wake aendelee kukaa. Watoto wao kama wanataka kuendelea kukaa wakodishwe. Lakini si kabla ya mwisho wa maisha ya mke au mume.
“Aina ya tatu ni wapangaji wa Shirika la Nyumba. Majengo haya yanahitaji kukarabatiwa. Yanahitaji kujengwa yakae kwa miaka mingi. Wanaokaa kwa kupangishwa wahakikishe kodi zinalipwa.”
Majumba Michenzani
Amesema majumba ya Michezani hadi maji ya bahari yanaingia ndani. “Hatuna sababu ya kuvunja nyumba. Serikali ina mpango wa kujenga nyumba mpya. Pale ambapo nyumba za zamani hazikidhi, zijengwe upya. Aliyepewa fidia asilipe. Kwa waliopangishwa walipe kodi,” amesema.
Uchimbaji wa mafuta
“Zanzibar imegundulika kuwa na gesi ya kutosha kabisa. Tukipata mafuta ya kutosha tutajenga mtambo wa kusafirisha bila kuyauza ghafi, inategemea wingi wake. Uganda wanatengeneza bomba, ukiwa na mafuta kidogo, ukataka kuyasafisha mwenyewe itakuwa gharama kubwa. Kama hayatoshi tutayasafirisha, ila kama yakitosha tutasafisha wenyewe.
“Gesi tuliyoigundua, tuna uwezo wa kufanya mtambo wa LPG hapa. Uchumi wetu utabadilika sana. Gesi ni mali kubwa, duniani kote kuna gharama kubwa ya kuizalisha. Gesi na mafuta ni miradi ya muda mrefu. Ukigundua leo unaanza kuona matunda yake miaka minne au mitano ijayo. Gesi ilikuwa imegunduliwa trilioni 3.8, sasa hivi kuna figure (takwimu) tofauti kabisa, ni kama mara tatu ya hiyo. Mategemeo ni mazuri na tutahakikisha inafaidisha Wazanzibari,” amesema.
Mambo matano aliyotekeleza
Rais Mwinyi anasema wakati anagombea urais, aliahidi mambo matano:-
1. Kuimarisha amani, umoja na mshikamano
Katika hili anasema alifanya mazungumzo na wapinzani wakaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). “Tulizungumza, tukapata mwafaka na kufanya kazi pamoja. Watu ni wamoja kwa sasa. Hili linanitia faraja sana,” amesema.
2. Uwajibikaji kwa watu wote
Katika hili amesema amefanya mabadiliko katika ngazi mbalimbali kuanzia ngazi za juu kabisa hadi za chini. “Lengo ni kuwaletea wananchi maendeleo,” amesema.
3. Mazingira mazuri ya uwekezaji na kufanya biashara
Amesema wawekezaji wanakwenda katika nchi zenye mazingira mazuri. “Nchi ina mazingira mazuri sana ya kufanya biashara kwa sasa,” ameongeza na kusema amefanyia kazi eneo la Mamlaka ya Uwekezaji kufanya kazi kwa muda mfupi na bila urasimu ili kuruhusu wawekezaji wamiminike Zanzibar.
4. Kuimarisha huduma za jamii
Amesema ugonjwa wa corona umechelewesha kasi aliyopanga kwenda nayo, lakini kuanzia Januari, 2022 wananchi watashuhudia huduma ya maji, umeme, afya, elimu na mengine vikitolewa kwa kasi. Anasema kwa kujiamini kwa kuwa tayari Zanzibar imepata mkopo wa masharti nafuu kutoka IMF, hivyo itapiga hatua kubwa na za haraka.
5. Kuondoa kero mbalimbali ndani ya jamii
Suala la udhalilishaji kwa wanawake na watoto, amesema jambo hili ni kero ya muda mrefu ila wamechukua hatua madhubuti, ikiwamo kubadili sheria na kuanzisha mahakama maalumu.
Kuhusu dawa za kulevya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaunda Mamlaka Mpya ya Kudhibiti dawa za kulevya na dhuluma wanazofanyiwa wananchi, hasa ardhi, ameunda tume maalumu kuchunguza migogoro ya ardhi. “Ardhi ndiyo kero namba moja Zanzibar,” amesema.
Je, unajua anazungumziaje maisha ya kawaida ya wananchi na huduma nyingine za jamii? Usikose toleo la JAMHURI wiki ijayo.