Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Simiyu
Familia ya marehemu Juma Jumapili (60), wameishukuru Serikali baada ya kuruhusu kuuchukua mwili wa marehemu huyo uliozuiliwa kutolewa katika Hospitali ya Rufaa Bugando iliyoko jijini Mwanza kutokana na kudaiwa gharama za matibabu sh.milioni 18.
Akizungumza kwa niaba ya familia Mwali Jumapili, amesema kuwa wameshindwa kulipia gharama za matibabu ya ndugu yao kutokana na kutokuwa na uwezo huo.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuturuhusu kuchukua mwili wa marehemu ndugu yetu ambaye alifariki Aprili Mosi mwaka huu lakini tulishindwa kuzika kutokana na kudaiwa sh.milioni 18 ambazo licha ya ndugu kuchangishana lakini hatukuweza kufikisha hata milioni 1” amesema.
Amesema kuwa marehemu Jumapili alipata ajali ya pikipiki Desemba 2023 na alifikishwa kupatiwa matibabu kwa mara ya kwanza Hospitali ya Wilaya ya Bariadi iliyoko Somanda na baadae kuhamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Simiyu iliyoko Nyaumata na pia kupewa Rufaa ya kwenda Hospitali ya Bugando kutokana na hali yake kuzidi kuwa mbaya.
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa marehemu anapata matibabu walilazimika kuuza ng’ombe, mashamba na baadhi ya vitu vya thamani ikiwa ni pamoja na ndugu kuchangishana ili kupata fedha za kugharamia matibabu yake lakini bado walikwama.
Amesema kuwa mazishi ya marehemu ndugu yao yalifanyika juzi katika makaburi ya familia yaliyoko eneo la Sakwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu.
Amesemma kuwa kutokana na kushindwa kuzipata gharama hizo walifikisha kilio chao kwa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Simon Simalenga, wakiomba msaada wa serikali kuwezesha kupewa mwili huo.
Naye kaka wa marehemu Elias Jumapili, amesema kuwa wamehangaika kupata mwili wa ndugu yao lakini ilishindikana kutokana na uwezo wao mdogo wa kifedha.
“Ndugu yangu alikwenda Bariadi kutafuta maisha ambapo akiwa huko alikuwa akijishughulisha na ufundi wa baiskeli hadi ajali ilipomkuta” amesema.
Mkuu huyo wa wilaya alifanya mawasiliano na Hospitali ya Rufaa ya Bugando ambapo mazungumzo yao yalizaa matunda baada ya hospitali hiyo kuruhusu mwili huo uchukuliwe bila familia hiyo kulipa gharama zilizotakiwa.
Simalenga amesema maelekezo ya Rais Samia ni kuwa mwananchi akishindwa kuchukua mwili kwa sababu ya gharama asitozwe bali apewe nafasi ya kuuchukua iwapo suala la malipo limeshindikana.