Juma lililopita nikiwa nafuatilia Kikao cha Pili cha Mkutano wa Bunge, nilimshuhudia na kumsikia Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba, akieleza matukio ya vifo vya raia katika maeneo kadhaa nchini, vilivyotokea kwenye shughuli za kisiasa na akahoji nafasi ya kisheria kuwashughulikia wahusika na waratibu wa matukio hayo badala ya wale wanaoshiriki katika maelezo yake.

Alisema kuwa kama waratibu wa matukio hayo wangechukuliwa hatua stahiki, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, pamoja na Katibu Mkuu wake, Dk. Wilbroad Slaa, walipaswa kuwa gerezani wakitumikia vifungo.

 

Mwigulu bila shaka alikuwa akitimiza wajibu wake kama mbunge kuyasema yale anayoona yanafaa kusemwa kuimarisha afya ya amani, utulivu na maendeleo kwenye Taifa letu, lakini hoja, haja na mantiki si kusema tu bali alikuwa anasema nini na chenye mashiko kiasi gani kwenye masikio na macho ya watu makini wanaojua kuchambua, kukusanya na kuunganisha nukta.

 

Lakini pia kimantiki, kauli yake imebeba ushahidi na hukumu kuwa Mbowe pamoja na Dk. Slaa ndiyo wamekuwa wanapanga au kuratibu na kusababisha mauaji ya raia wasiokuwa na hatia kwenye mikutano ya Chadema ambayo baadhi ya vifo vimehusisha wanachama, makada, na viongozi wa chama hicho. Hii maana yake ni kwamba Mbowe na Dk. Slaa walipanga au kuratibu kuua wanachama, makada na viongozi wao.

Akili ya kawaida inakataa kukubaliana na Mwigulu kuwa viongozi hao wamekuwa wanapanga mauaji ya wanachama, viongozi na hata makada wake kutokana na baadhi ya ripoti za tume za Serikali zilizopata kuchunguza matukio ya vifo vilivyotokeo kwenye mikutano ya kisiasa, hususan mikutano ya Chadema.

 

Lakini pia ombi la viongozi hao wa Chadema kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete kumuomba kuunda mahakama maalum ya kijaji kuchunguza vifo vyenye utata na vile vilivyotokea kwenye mikutano ya kisiasa.

 

Hapa mtu makini atajiuliza, hivi kama umepanga mauaji unaweza kumwomba Rais aunde tume ya kijaji ili ikuchunguze? Au majibu ya tume ya Serikali kutuhumu wateule wa Rais ndiyo kuhalalishe Mbowe na Dk. Slaa kwenda kutumikia vifungo kama Mwigulu anavyosema?

Mtakumbuka kuwa kwenye sakata la kesi ya ugaidi lililokuwa linamkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, Mwigulu akiwa bungeni kwenye moja ya michango yake aliuaminisha umma wa Watanzania kuwa anao ushahidi kuwa Chadema ni chama cha magaidi na ushahidi huo atautoa popote iwe polisi, mahakamani, na hata mbinguni.

 

Ushaidi huo hakuutoa popote na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilimfutia Lwakatare shitaka la ugaidi. Mwigulu huyo huyo hakutokea kutoa ushahidi kama shahidi muhimu kwenye kesi kule Singida baada ya vurugu za Ndago, ambazo ilisemekana kuwa 
alizifadhili na kuchukua vijana kutoka Dar es Salaam. Vurugu zile zilisababisha kifo cha mtoto wa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyekuwa mwanachama wa Chadema. Makada na viongozi wa Chadema wakashitakiwa na baadaye walishinda kesi hiyo.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani kule Arusha, Mwigulu alikuwa anatembea na kijana mmoja aliyeitwa Mussa Tesha. Kijana yule alifanywa kama bango la kuombea kura za huruma kwenye kampeni za CCM.

 

Mwigulu huyu huyu alikuwa akimnadi kuwa amefanyiwa ugaidi kwa kumwagiwa tindikali na makada wa Chadema kule Igunga wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge. Inasemekana kuwa alishawishi baadhi ya makada wa Chadema wakamatwe kwa kuwa ni magaidi.

 

Vijana watano wa Chadema wakakamatwa kwa makosa ya ugaidi na kudhuru mwili. Baadaye Mahakama iliwafutia kesi ya ugaidi vijana wale na kuonya kuwa masuala ya visingizo vya ugaidi yanaathiri taswira ya nchi na uchumi wake. Ikawa ni pigo jingine la kukwama kwa ugaidi.

Ripoti ya Tume ya Serikali ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyoundwa kufuatilia vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu, imemtaka aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, kuwajibishwa kutokana na kutuhumiwa kusimamia mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Runinga cha Channel Ten yaliyotokea kwenye ufunguzi wa tawi la Chadema kule Nyololo, Iringa.

 

Kilichotokea badala ya kamanda huyo kuchukuliwa hatua za kinidhamu, alisifiwa bungeni kwa kuchapa kazi na baadaye alipandishwa cheo na kuhamishiwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.

 

Utawala bora wa kisheria ungekuwa unafuata njia yake ya asili naamini bila shaka kuwa Mwigulu asingethubutu kutoa kauli aliyotoa bungeni.  Mwigulu ametoa kauli hiyo huku kumbukumbu ya tukio la Januari 5, 2011 ikiwa haijafutika bali kukolezewa wino na majibu ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii hivi karibuni.

 

Ripoti hiyo kwenye ukurasa wa 11 na 12 imelituhumu moja kwa moja Jeshi la Polisi kwa kuhusika na mauaji ya raia watatu na kujeruhi watu wengine zaidi ya 48. Majeruhi walikutwa na majeraha ya risasi za moto kwenye miili yao na tume imekiri kuwa askari walitumia nguvu za ziada zisizokuwa na ulazima kuzuia maandamano ya Chadema.

 

Hapa Mwigulu pia amesahau kuwa mwenyekiti wake wakati akiwahutubia wajumbe wa Kamati Kuu ya chama kule Dodoma, aliwaonya kutokutegemea Jeshi la Polisi kukabiliana na upinzani.

Mwigulu akiwa anachagiza viongozi wa Chadema wawe rumande, kumbukumbu zinaonesha kuwa makada wa CCM Samweli Mtinange na Shabani Limu waliotuhumiwa kumuua Msafri Mbwambo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Usa River, hawajakamatwa hadi leo baada ya kutoroka wakiwa mikononi mwa askari wenye silaha.

 

Mbwambo aliuawa kwa kukatwa shingo na msumeno wa kukatia mbao Aprili 27, 2012. Kada wa CCM aliyedaiwa kutenda mauaji hayo inasemekana kuwa alitoroshwa ili kuepusha kukichafua chama hicho na tope la mauaji dhidi ya kiongozi wa Chadema, tangu atoroke mikononi mwa polisi kwenye eneo la Mahakama kule Arusha.

Matukio haya machache kati ya mengi yenye ushahidi unaoonesha vitendo, yatoshe kumuonesha Mwigulu kuwa yeye kama kijana huu ni wakati wa kuhakikisha kuwa anakuwa mfano kwa kufanya siasa za kistaarabu  na kuhakikisha kuwa ushauri wa mwenyekiti wake kuwa CCM iache kutegemea Jeshi la Polisi kujibu mapigo ya upinzani unafuatwa, maana yakiorodheshwa matukio mabaya yatakuwa mengi na mazito kuliko wepesi wa kauli zake mbele ya vipaza sauti vya Bunge.

 

Lakini kubwa ajue kuwa wananchi wanajua kuchagua pumba na mchele na wanajua kutofautisha kati ya chepe na kijiko. Wakatabahu.