WAZIRI wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema hakuna utata au uchotaji wa Fedha katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa X Dk Mwigulu ameeleza kuwa BoT inasimamia kwa umakini sheria za nchi na miiko ya benki kuu zote duniani.

Dk Mwigulu aliandika hayo jana kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa iliyoandikwa na gazeti (si HabariLEO) iliyotokana na uchambuzi wa taasisi isiyo ya kiserikali iitwayo Wajibu inayoongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mstaafu, Ludovic Uttoh.

Alieleza kuwa kwa ujumla maelezo ya taarifa hiyo yanaeleweka na hayana utata hivyo hafahamu kwa nini mwandishi wa gazeti hilo ameeleza kuwa kuna utata BoT. “Inawezekana aliandika kwa nia ovu ya kuupotosha umma, kuidhalilisha BoT na kusababisha taharuki kwa jamii.

Aidha, inawezekana mwandishi ameandika kwa kutojua sheria suala ambalo angeuliza angepewa ufafanuzi unaotakiwa. Kutokana na maelezo hayo,”aliandika Dk Mwigulu.

Alieleza kuwa taarifa hiyo imeelezea suala ambalo hufanyika kila mwaka kwa kuwa sheria ya BoT inaruhusu kutoa mikopo ya muda mfupi kwa serikali kukidhi mahitaji ya matumizi ambayo yanakuwa hayajapata mapato. “Kwa mujibu wa kifungu cha 34 hadi 37 cha BoT Act, Serikali inaruhusiwa kukopa hadi asilimia 18 ya makusanyo halisi ya ndani ya mwaka uliopita,” alieleza Dk Mwigulu.

Aliongeza: “Hili limekuwa likidanganyika hivyo tangu BoT ianzishwe. BoT ni benki ya serikali, serikali huchukua advance kwa mujibu wa sheria badala ya kukopa kwa riba kubwa kutoka benki za kibiashara”.

Dk Mwigulu alieleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023, serikali ilikuwa inaweza kukopa BoT kiasi kinachofikia Sh trilioni 4.5. “Taarifa ya kuwapo kwa mkopo wa Shilingi trilioni ni suala ambalo liko ndani ya wigo unaokubalika kisheria. Kiasi hicho kilipofika mwisho wa mwaka kilijumuishwa kwenye Treasury Bonds za mwaka husika ambazo zinaendelea kulipia riba kama sehemu ya mikopo ya ndani,”alieleza.

Alisema kuwa utaratibu huo ni wa kawaida na hufanyika kwa benki kuu za nchi nyingi duniani wakati serikali inapohitaji fedha za kugharimia bajeti wakati ikiendelea kujipanga na kukusanya mapato kutoka katika vyanzo mbalimbali. “Ndiyo maana hata IMF waliridhika kuwa BoT na serikali wamezingatia sheria na taratibu za kimataifa kama inavyotakiwa,”aliandika Dk Mwigulu.

Alieleza kuwa kutokana na uzingatiwaji wa sheria hizo, bodi ya IMF waliridhia kutoa Dola za Marekani milioni 300 kwa mwaka 2023/2024 na Benki ya Dunia waliridhia kutoa Dola za Marekani milioni 750 kwa mwaka 2023/2024.

Alisema tathmini ya pili ya program ya IMF iliyofanyika Desemba 2023 iliangalia masuala mbalimbali yakiwamo ya mapato, matumizi, madeni, uzingatiwaji wa sheria ya BoT, ukuaji wa uchumi, mfumuko wa bei, urari wa biashara, thamani ya Shilingi na usimamizi wa masoko ya fedha nchini. “BoT itaandaa taarifa kwa umma na kukanusha na kutoa elimu kuwa hakuna utata wowote uliopo kutokana na taarifa hizo bali ni suala la kawaida ambalo serikali inaruhusiwa kukopa kwa kuzingatia ukomo wa asilimia 18 ya mapato halisi ya mwaka uliopita, kama ilivyo kwa sheria za nchi nyingine duniani. Hata ukomo huu upo kwenye viwango karibiana kati ya nchi zote za EAC,”aliandika.

Please follow and like us:
Pin Share