Mwaka 2008 nilisoma makala aliyoandika Samson Mwigamba. Nilipoisoma makala hayo nilibaini kuwa Mwigamba ni bomu linalosubiri wakati, lakini watu waliokuwa wamepofushwa na mapenzi dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliishangilia makala ile.
Mwigamba aliibuka ghafla kupitia gazeti la Tanzania Daima. Ni gazeti nililolianzisha na kulijenga likawa na heshima katika jamii.
Nikiwa masomoni nje ya nchi, niliona makala zenye kupungukiwa na viwango kutoka kwa Mwigamba zikichapishwa kwa kasi ya kutisha. Hapa alikuwa anafanya kazi ya kuchafua kila aliyepita mbele yake au aliyekuwa na hasira naye — awe mbunge, kiongozi wa Serikali au wa chama cha upinzani — isipokuwa wale tu wa Chadema. Alikuwa anatoa tuhuma za hovyo kabisa bila ushahidi wowote.
Kwa miaka karibu mitano aliyoandika makala katika gazeti la Tanzania Daima amefanya kazi kubwa ya kuchafua majina ya watu, kujenga misingi ya uchochezi na kimsingi ilifikia hatua nikawaambia wamiliki wa Tanzania Daima kuwa inavyoelekea hawasomi makala za Mwigamba au Mhariri anayezipitisha ni dhaifu na kwamba makala hizo zina hatari kubwa kwa jamii.
Sitanii, viongozi hawa niliwaeleza kuwa uandishi wa habari ni taaluma sawa na taaluma nyingine. Unahitaji kusomewa, kwani uandishi hauishii katika kujua kusoma na kuandika tu, bali kufahamu dhima unayobeba kwa Taifa unapofanya kazi hii. Nimesema mara kwa mara kuwa si kila mtu anaweza kuwa mwandishi, ingawa baadhi ya watu wamekuwa wakinipinga.
Nakubaliana na wanaosema kuwa uandishi ni kipaji, ila kipaji bila kuendelezwa ni hatari. Pengine nitumie mfano wa ndugu zetu Wamaasai wa hapa Tanzania maana Kenya pia wapo Wamaasai. Hawa wanashinda mbio za kimataifa na kuzoa medali. Wamaasai wa Tanzania wa sasa ukiacha akina Juma Ikangaa na Filbert Bayi wenye asili ya Arusha pekee waliofanikiwa kuleta medali kwa kuwa walipata mafundisho.
Wamaasai wa Kenya na wa Tanzania wa sasa wote wanakimbiza swala porini na kumkamata bila kumchoma kwa mkuki. Niliuliza nikaambiwa kuwa swala akifukuzwa hadi akachoka na kusimama akakamatwa nyama yake inakuwa laini kutokana na uchovu wa kutimua mbio. Hili wanalifanya Wamaasai wa Kenya na Wamaasai wa Tanzania.
Sitanii, kinachotokea Wamaasai wa Kenya wamepata mafunzo ya kukimbia. Hata wanapokwenda kwenye mashindano ya kimataifa ikipigwa bastola juu, wanajua hicho ni kiashiria cha mbio kuanza hivyo wanatimka bila kuchelewa. Wamaasai wa Tanzania kwa kuwa hawana mafunzo, ikipigwa juu bastola wanatafuta pa kujificha wakijua ni Wamang’ati na Wakurya wamewaingilia kuiba ng’ombe wao!
Sasa nasema Mwigamba katika uandishi wa habari hana tofauti na Wamaasai wa Tanzania. Ikiwa ana kipaji, basi alistahili kwenda shule akakikuze kipaji hicho. Hata hivyo, ninachoshuhudia Mwigamba katika makala zake nyingi amekuwa bingwa wa kutunga uongo, kuchochea jamii na kusambaza chuki kwa watu mbalimbali.
Bukoba kuna msemo mzuri tu. Wanasema ‘embwa ekalya ako omuzana basheka, elyo yalile aka mukama wayo, bati yashela’ (mbwa alikula [tonge] la kijakazi wakacheka, alipokula la mmiliki wakamuua). Haya ndiyo yaliyowakumba Chadema. Mwigamba amekula matonge ya vijakazi wengi, wao wakicheka, lakini alipogeukia lao wanasema atoswe.
Siasa za Tanzania zinanipa shida kidogo. Huko serikalini hawataki msema ukweli, kwenye vyama vya upinzani hawataki msema ukweli. Jambo moja tu ninalolifahamu fika ni kuwa serikalini ukiwa msema ukweli utapigwa fitina hadi utakoma. Milele hutakaa upande cheo. Watatoka nyuma watoto watakuwa wakurugenzi na hadi makamishna tena unaowazidi hata kiwango cha elimu, alimradi unasema ukweli utajuta tu.
Kwenye upinzani sasa nako kumenichanganya. Mwigamba anasema amewakumbusha Chadema kuwa fedha hazipelekwi mikoani, wameondoa kinyemela kifungu cha ukomo wa uongozi, lakini akatembeza na hukumu kuwa Zitto Kabwe asingekwaruzana na Freeman Mbowe iwapo tu kifungu cha ukomo wa kugombea uenyekiti ndani ya Chadema kisingeondolewa kinyemela mwaka huu au mwakani Mbowe asingegombea uenyekiti mara ya tatu.
Kilichofuata baada ya hapo ni sarakasi, kutembezeana ngumi na hata kufikishana polisi. Polisi nao walipoliangalia, wakasema hili limalizwe ndani ya chama kwani hakuna kesi. Chadema nao ukiwasikiliza wana hoja. Wanasema Mwigamba alikuwa akiwasasambua viongozi wa chama kwenye mitandao ya kijamii akitumia jina bandia la “Mkulima Masikini.”
Sitanii, hapa nasema ndipo tulipokwama. Kwanza ifahamike kuwa Mwigamba kwa kila hali amewakosea Chadema. Yeye ni mwanachama halali wa Chadema na anaingia katika vikao vinavyomhusu. Hayo aliyoyaandika kwenye mitandao ya kijamii alishindwa nini kuyasema kwenye vikao halali? Kama alishindwa kwenye vikao halali nini kilimzuia kuyachapisha kwa jina lake hadi ajiite “Mkulima Masikini?”
Tabia hii chafu ya kuuma na kupuliza kama panya imetapakaa kila mahala katika nchi hii. Kwa kiasi kikubwa inakwamisha maendeleo. Viongozi wanafanya uamuzi kwenye vikao, watu kama Mwigamba wanashiriki kupiga makofi, lakini kumbe wakiwa humo humo ndani ya vikao wanatuma nje ujumbe wa kupingana na uamuzi walioshiriki kuufanya.
Kimsingi niseme hii inapoteza muda wa vyama au Serikali katika kuharakisha maendeleo. Mtu kama hutaki jambo ni bora useme hapana mbele ya mtu badala ya kusema ndiyooooo… kumbe moyoni unamaanisha hapana. Na hii watu kama sisi imetugharimu mara nyingi tu. Mimi leo siwezi kuelekezwa rafiki yangu awe nani na nimchukie nani.
Na wote wenye mitafaruku yao nimekuwa nikiwaambia ukweli na wanajua nasimamia nini. Wanapoparurana nawaambia migogoro yenu isinifikishe mahala pa kupandikizwa mawazo. Hili nimekuwa nikilisema wazi ingawa haliwafurahishi baadhi ya watu na wako tayari kuhakikisha wanasimama njiani inakoelekea kupitia riziki yangu. Binafsi nawaambia nawafahamu na nawashukuru.
Sitanii, kwa kila kiwango Mwigamba kitendo cha kuwa kwenye vikao vya Chadema na akashindwa kuyasema hayo aliyoyaandika kwenye mitandao ya kijamii tena kwa jina bandia, ni usaliti. Ina maana kama tungekuwa tumempeleka Mwigamba DRC tunapigana na M23, ina angekuwa anavujisha mbinu zetu kwa waasi kupitia majina bandia.
Mtu kama huyu ni hatari kuliko ukoma. Kama kuna kitu kimekwamisha maendeleo serikalini ni fitina. Nchi hii imegombana kwa mambo yasiyo na kichwa wala miguu ikabaki vipande.
Niguse mioyo ya Watanzania kwa mitambo ya Richmond, ambayo baadaye iligeuka Dowans na sasa Symbion. Zilitumika fitina kama hizi za Mwigamba serikalini kuliingiza Taifa katika mgogoro na hasara kubwa.
Watu wa aina ya Mwigamba walifikia hatua wakaliaminisha Taifa kuwa Edward Lowassa aliwapatia Richmond/Dowans mkataba wa kufua umeme na nchi ikawa inalipa Sh milioni 152 kila siku bure, wakati si kweli. Hawakusema ukweli kuwa Dowans ilikuwa inazalisha megawati 100 za umeme na hakuna Mtanzania aliyepata kutangaziwa na Tanesco atumie bure umeme kwa sababu unazalishwa na Dowans.
Mitambo hii ilikuwa tuuziwe kama Taifa kwa Sh bilioni 55, lakini ikatembezwa fitina ya ‘kufa mtu’, leo tumekwishawalipa Symbion kwa mitambo ile ile si chini ya Sh bilioni 150 na mitambo si yetu. Watanzania tuwafahamu hawa vizabizabina wanaoshiriki vikao kisha wakajifanya wao ni malaika waliofika duniani leo. Mwigamba alikosea.
Sitanii, nikirejea upande wa Chadema nao walikosea. Hata kama Mwigamba alikosea hawakuwa na haki ya kumpa kipigo. Chini ya Marekebisho ya Sheria ya Mwaka 1989 adhabu ya viboko ilirejeshwa nchini, lakini haitolewi na kila mtu. Adhabu hii inatolewa kwa amri ya Mahakama, baada ya pande zote mbili kusikilizwa.
Kilichotokea Arusha ni wazi Chadema walichukua sheria mkononi. Kwa binadamu yeyote aliyestaarabika si busara kuchukua sheria mkononi. Hata kama Mwigamba angewakosea Chadema namna gani hawakupaswa kumpa kipigo. Walipaswa kuwaita polisi, wamkamate — wakachukua kompyuta mkato (laptop) yake na kuifanyia uchunguzi, kisha akafikishwa mahakamani kwa kuvujisha siri kutoka katika vikao alivyoaminiwa.
Kimsingi ukiacha kachumbari za hapa na pale, nimeandika makala haya kueleza jinsi Mwigamba alivyo hatari. Sitazungumzia makala aliyoiandika dhidi ya Jeshi la Polisi ambayo iko mahakamani, lakini mtu akipata fursa aisome, kisha alinganishe mahudhui ya makala hayo na mlolongo wa aliyoyaandika dhidi ya Chadema, kisha ajipe jibu. Nasema makala aliyoandika Mwigamba dhidi ya Chadema alilenga kuwachochea wanachama wauasi uongozi.
Sitanii, nasema kama nchi yetu itaendekeza utaratibu wa viongozi kuasi uamuzi halali wa vikao na tukaendelea kuwashangilia, hatimaye nchi hii itakuwa haipigi hatua — iwe ni kwenye vyama vya siasa au serikalini — ni lazima uamuzi wa pamoja uendelee kutekelezwa kwa pamoja, kwani bila hivyo ni kuzalisha migogoro kama tunayoishuhudia kwenye chama tawala isiyo na tija kwa Taifa hili.