Dodoma. Mahakama ya hakimu mkazi Mkoa wa Dodoma imemwachia mwenyekiti wa zamani wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamis baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha maombi ya kuifuta kesi iliyokuwa ikimkabili.
Uamuzi huo umetolewa leo Februari 15, 2018 na hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, Emmanuel Fovo baada kuridhia ombi la wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Biswalo Biswalo kuiomba mahakama kuifuta kesi hiyo.
Desemba 9, 2017, Sadifa alikamatwa na Takukuru akiwa nyumbani kwake Mailimbili mjini hapa akituhumiwa kugawa rushwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa umoja huo.
Mbunge huyo wa Donge na mjumbe wa kamati kuu ya CCM aliyemaliza muda wake, baada ya kukamatwa alilala mahabusu kwa siku tatu baada ya kukosa dhamana.
Katika shtaka la kwanza, Sadifa alidaiwa aliwahonga wanachama ili wamchague Rashid Mohamed Rashid ambaye alikuwa akiwania umakamu mwenyekiti katika uchaguzi mkuu wa umoja huo.
Shtaka la pili, alidaiwa kuwaahidi kuwalipia gharama za usafiri wanachama wa umoja huo kwa kuwasafirisha kutoka Dodoma hadi Kagera kama zawadi ili wamchague Rashid.