Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Moshi, James Silas, amekataliwa kuendelea kusikiliza shauri la ardhi namba 175/2017 lililopo mbele yake.

Oktoba 6, mwaka huu, Donald Kimambo na David Kimambo waliandika barua wakimtaka Silas kujitoa kusikiliza shauri lao.

Barua hiyo imeeleza kuwa wamechukua uamuzi huo baada ya Silas kufuta shauri lao bila kusikiliza pande zote, hivyo kutotenda haki. 

Sehemu ya barua hiyo inasem: “Tuna taarifa kwamba ukoo wako na ukoo wa Mbowe mna mafungamano ya kindugu, kutokana na mahusiano hayo ya kindugu tunaona haki haitendeki ukiwa unasikiliza kesi. Ili haki itendeke, tunakuomba ujitoe na shauri hili liendelee.”

Awali shauri hilo lilifutwa Januari 17, mwaka huu bila kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, lakini Kimambo na mdogo wake walipinga uamuzi huo Mahakama Kuu Kanda ya Moshi mbele ya aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Aishael Sumari. 

Oktoba mwaka huu, Jaji Sumari baada ya kupitia rufaa hiyo, alitoa uamuzi wa shauri hilo kusikilizwa upya na Baraza la Ardhi na Nyumba baada ya kubaini kuwapo upungufu kadhaa katika uamuzi huo.

Walalamikaji wanadai kupokea vitisho na kejeli kutoka kwa Silas, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

“Kutokana na sababu tulizozitaja hapo juu, zikiwamo kauli za vitisho, kutufokea na kejeli, tunaona wazi kwamba umeshatoa hukumu kwa kumpa ushindi mlalamikiwa ambaye amepora ardhi yetu, tunaomba ujitoe kusikiliza shauri hili ili haki ionekane ikitendeka,” inahitimisha barua hiyo. 

Silas alipozungumza na JAMHURI kuhusu sakata hilo amesema kwamba huo ni uongo na uzushi, kwani madai hayo hayana ukweli wowote.

Amekiri kupokea barua ya malalamiko kutoka kwa walalamikaji katika shauri hilo, lakini akasema kwamba hawawezi kuruhusu mahakama ziendeshwe kwa hisia na kusisitiza kuwa kwa kufanya hivyo hakuna kesi zitakazosikilizwa na kufikia uamuzi sahihi.

“Baada ya kuandika barua walikwenda kumuona bosi wangu ambaye ni msajili wa mabaraza ya ardhi na nyumba wa kanda na aliwaeleza utaratibu wa kufuata, ikiwamo kufika mahakamani siku ya kesi na kunyoosha mkono na kutoa hoja zao ili ziwekwe kwenye kumbukumbu za mahakama.

“Bosi wangu aliwaeleza kuwa hata majaji wanalalamikiwa, lakini unapoona hauna imani na jaji unafika mahakamani, unamwambia mheshimiwa jaji nashukuru kusikiliza shauri hili lakini tulipofikia nina hisia au nina ushahidi kwamba mwenendo wa kesi haunifurahishi jinsi unavyoendesha hilo shauri,” amesema Silas.

Amesema kuwa anayelalamikia kutotendewa haki sharti atoe ushahidi wa kile anachokilalamikia, lakini amesisitiza kuwa wanaomtuhumu hawana ushahidi wowote wa kuweza kuthibitisha tuhuma dhidi yake.

Kuhusu kuwa na uhusiano wa kindugu na mlalamikiwa, mwenyekiti huyo amekana madai hayo na kueleza kuwa huo ni uzushi. 

Kuhusu kufuta shauri hilo bila kulisikiliza, amesema alifikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa liliwahi kusikilizwa huko nyuma na ikaonekana walalamikaji hao walikuwa wakiisumbua mahakama.

Amesema shauri hilo limekuwepo mahakamani hapo kwa miaka sita na limekuwa likifunguliwa na watu tofauti tofauti huku wakishindwa kufika mahakamani.

“Baada ya uamuzi wangu walikata rufaa Mahakama Kuu, jalada limerudi likiwa na maelekezo asikilize mwenyekiti huyo huyo ambaye ni mimi, shauri halijaanza kusikilizwa wanaanza kukimbilia kwenye magazeti,” amesema Silas.

Donald Kimambo na David Kimambo walifungua shauri namba 175 mwaka 2017 kutokana na mgogoro wa ardhi baina yao na Clement Mbowe. 

Shauri hilo lilifungwa mwanzoni mwa mwaka huu kabla halijakatiwa rufaa Oktoba mwaka huu.