*Adaiwa kuchota 270,000, yeye ajibu hoja zote
Halmashauri Wilaya ya Karagwe imeingia katika mgogoro mpya, baada ya madiwani na watendaji wengine kuanzisha harakati za kumg’oa Mwenyekiti wa Halmashauri, Kashunju Singsbert Runyogote, ambaye naye amejibu mapigo kwa kuzima harakati hizo.
Tarehe 30/5/2012 mdiwani 29 walijiorodhesha majina yao na kutia saini kumtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kuitisha kikao maalum kujadili tuhuma zinazomkabili Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Runyogote.
Barua hiyo iliwasilishwa ofisi ya Mkurugenzi tarehe 4/6/2012 na ilipokelewa na Katibu Mhitasi wa Mkurugenzi, Selestina Seif.
Moja ya tuhuma dhidi ya Mwenyekiti ni madai ya ndugu Kashunju kushinikiza kulipwa safari ya kwenda Bukoba kisha akalipwa fedha Sh 270,000 za kukagua miradi wakati akijua kwamba wakati wa ukaguzi wa miradi na safari ya Bukoba atakuwa Rwanda kikazi, safari ambayo pia alilipwa posho na Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe; hivyo alipokea posho tatu kwa wakati mmoja kutoka Halmashauri. Inasemekana hata huko Rwanda Kashunju alilipiwa kila kitu na Serikali ya Rwanda.
Ili kuepusha tafrani, tarehe 6 Juni, yaani siku mbili baada ya madiwani kuwasilisha barua kwa Mkurugenzi, Runyogote alimwagiza Ashura Kajuna (mtumishi wa Halmashauri) amrejeshee kwenye halmashauri Sh 270,000.
Fedha hizo zilipokewa tarehe 6/6/2012 na ndugu Jackson wa ofisi ya malipo ya Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe na zikakatiwa stakabadhi namba 143133 ya Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.
Baada ya kurejesha fedha hizo, ndugu Runyogote ametumia viongozi wa mkoa (CCM na wakuu wa wilaya za Karagwe, Kyerwa na Misenyi) kuwaziba midomo madiwani ili tuhuma dhidi yake zisichunguzwe na kikao kisiitishwe.
Jamhuri ilipowasiliana na Runyogote, alisema: “Ni kweli nililipwa hiyo Sh 270,000 lakini baada ya kuzipokea nilipokwenda kijijini kwetu nikafiwa hivyo sikufanya kazi niliyokuwa nimepewa fedha kufanya ikabidi nizirejeshe na nilipewa risiti.”
Tarehe 7/6/2012 madiwani wote wa CCM katika Wilaya ya Karagwe waliitwa na kutishwa na vigogo hao wasiendelee na azma yao ya kushirikiana na wapinzani kumjadili Runyogote. Katika kikao hicho cha madiwani wa CCM Runyogote alikiri kurejesha halmashauri Sh 270,000. Hata hivyo, ilishinikizwa asamehewe.
Kwa mujibu wa kanuni, Mkurugenzi alitakiwa kuitisha kikao hicho ndani ya siku saba baada ya kupokea barua ya madiwani; hata hivyo, siku hizo saba zimepita bila kikao kufanyika.
“Kinachotusikitisha ni kwamba wapo watumishi wa halmashauri ya wilaya ambao walipokea posho mara mbili kama alivyofanya Kashunju na kesi zao zinaendelea mahakamani chini ya PCCB. Mbaya zaidi juzijuzi mtumishi Florian Buberwa, mganga katika Kituo cha Afya Murongo, imeshinikizwa apelekwe mahakamani kwa kuisababishia halmashauri hasara ya shilingi 112,000; vyombo vya dola vilishauri mganga huyo arejeshe lakini Kashunju akakataa.
“Inasikitisha kuona Kashunju anaachiwa huru kwa tuhuma ya 270,000, kwa kosa lilelile linalowaangamiza wengine. Hali hii imeleta hali ya kutokuelewana na chuki baina ya madiwani wa Karagwe. Ikumbukwe kuwa Kashunju ni diwani kwa tiketi ya CCM. Imani za CCM zimejengwa chini ya misingi ya USAWA kwani binadamu wote ni sawa, sasa iweje Kashunju alindwe na wakubwa kwa kosa lilelile lililowaangamiza wengine?” alihoji mmoja wa watumishi aliyeshuhudia madudu hayo. Runyogote aliliambia Jamhuri kuwa si kazi yake kuwafikisha mahakamani waliotuhumiwa kwani zipo mamlaka zinazohusika.
Tuhuma nyingine zinazomkabili Runyogote ni pamoja na kupewa mafuta na gari la Halmashauri kumpeleka nyumbani kwake Rukuraijo (km 45 kutoka Kayanga) na kumrudisha makao makuu ya wilaya, Kayanga, wakati vikao vya Baraza vikiendelea. Baraza la Madiwani halijawahi kuidhinisha mafuta ya Mwenyekiti ya kumsafirisha wakati vikao vikiendelea isipokuwa posho ya kujikimu tu. Hali hii inaisababishia Halmashauri hasara kubwa kwani hata posho za kujikimu analipwa. Runyogote alisema: “Katika hilo ndugu Mwandishi, ebu fuatilia ujue stahiki za Meya na Mwenyekiti wa Halmashauri na utaona sina la kujibu.”
Ndugu Runyogote anatuhumiwa pia kutumia raslimali za Halmashauri kwa kazi binafsi, mfano mwaka 2008 alihudhuria sherehe za kusimikwa na kuwekwa wakfu Askofu Rugambwa katika Jimbo Katoliki la Kigoma kwa kutumia gari la TASAF (STK 2098). Runyogote alisema: “Huyu askofu ni mzaliwa wa Karagwe, hivi kama ningealikwa ningekataa kwenda kweli? Kwanza tulikwenda wengi, sijui kwa nini mimi tu ndo iwe nongwa.”
Posho yake, dereva pamoja na mafuta viligharimiwa na Halmashauri. Pia Amekuwa akipokea fedha za posho kwa siku nyingi zaidi ya zile zilizotajwa kwenye mwaliko wa safari za kikazi. Mfano, katika safari ya kuhudhuria LVRLAC Kisumu (KENYA), barua ya mwaliko ilitaja siku 3 yeye akadai posho za siku 7 mbali na siku za njiani. Hapa Runyogote alisema ni kweli alizipokea kwani siku moja alilala Kampala wakati wa kwenda, na nyingine wakati wa kurudi na baada ya mkutano alilala Kisumu, hivyo zikichanganywa na siku tatu za mkutano zinatimia saba.
Zipo pia tuhuma ya kushinikiza uanzishaji wa miradi mbalimbali kwa maslahi binafsi na kwa kukiuka taratibu za vikao vya halmashauri huku akijua. Mfano Uanzishaji wa Mradi wa Kitega Uchumi katika stendi ya Kayanga ambapo mradi huu haukufuata taratibu za kupitisha kwenye ngazi za kamati ya wataalamu (CMT), Kamati ya Ujenzi, Uchumi na Mazingira na badala yake alilazimisha kupitisha kwenye Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, Baraza la Madiwani na radi Radio FADECO chombo ambacho hakitoi Maamuzi.
“Kitendo hiki alikifanya kwa makusudi kwani hata alifikia kushinikiza kughushi Muhtasari wa Kikao cha Baraza kuonyesha kuwa suala hilo lilishaafikiwa wakati sio kweli,” aliongeza mtoa habari wetu.
“Sheria inatutaka ifikapo mwaka 2025 kila halmashauri nchini ijitegemee kwa asilimia 20. Leo Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe inajitegemea kwa asilimia 4.3. Kama tunataka kufika huko, ni lazima tufanye uwekezaji na hili naamini nilifanya jambo sahihi na kwa kufuata taratibu zote,” alisema Runyogote.
Mwenyekiti kwa manufaa binafsi alilazimisha vifaa vya mradi wa maji Rukuraijo vilivyonunuliwa na kusafirishwa moja kwa moja hadi kwenye kata yake bila kufuata taratibu za ununuzi, jambo hilo lilileta mtafaruku mkubwa na vifaa hivyo kurudishwa halmashauri kwa gari namba SM 3941 jambo ambalo liliisababishia halmashauri hasara.
“Hili lilipotokea nilimuuliza Mkuu wa Idara ya Maji kuwa ulitaka kunitega? Maana walitaka na vifaa wavihifadhi kwangu kwa kuwa nina ghala nilikataa. Hili halinihusu na miradi hii inafahamika taratibu zake,” alisema Runyogote.
Akiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, anadaiwa kusaini mikataba yenye utata. Mfano mkataba wa matengenezo ya madirisha ya chuma ya shule za sekondari na ule wa ununuzi wa saruji iliyoletwa ikiwa na kilo pungufu, pia anahusishwa na upungufu wa saruji kwani magari yake ndiyo yaliyosafirisha saruji hiyo. Haijulikani ni jinsi gani alipewa zabuni hiyo wakati akijua yeye ni Mwenyekiti wa Halmashauri. Tuhuma hizi alisema si za kweli na waliohusika akiwamo Mkurugenzi aliagiza wapewe onyo.
Runyogote anatuhumiwa pia kushindwa kusimamia uazimio halali wa vikao vya Baraza la Madiwani, kwa kukosa ushirikishaji na ushirikishwaji wa wajumbe wa Baraza la Madiwani.
Mfano azimio la kuwarudisha kazini watumishi waliosimamishwa kazi kuepuka gharama zinazoendelea kuikabili Halmashauri na migogoro isiyokuwa ya lazima.
Katika hili, alisema Mbunge wa Karagwe (CCM), Gosbert Blandes, kwa kushirikiana na baadhi ya madiwani walikuwa wakishinikiza watumishi hao warejeshwe kazini kwa kushushwa vyeo na kupewa onyo.
“Mimi nilikataa nikasema taratibu za kisheria zifuatwe. Hawa wangeweza kutushitaki wakalipwa hadi Sh milioni 200. Ikifikia hapo, watajitoa hawa na kusema ni la Mwenyekiti. Tumewapelekea tuhuma zao, wao hawajajibu,” alisema Runyogote. Hata hivyo, watumishi waliosimamishwa waliliambia Jamhuri kuwa tuhuma hizo wamezijibu siku nyingi.
Si hilo tu, pamoja na kulipwa gharama za safari na posho kwenda Dar es Salaam kushughulikia gari STK 4891 ambalo limekaa gereji muda mrefu, Mwenyekiti ameshindwa kutoa taarifa mbele ya Baraza la Madiwani juu ya hali/hatima ya gari hilo.
Aijibu tuhuma hizi, Runyogote alisema gari hilo sasa limetengenezwa na kutengamaa na si muda litarejea Karagwe. “Hivi litakaporejea waliokuwa wanasema aibu wataiweka wapi?” alihoji.
Tuhuma nyingine ni kuwa chanzo cha migogoro kati ya watumishi na Halmashauri, inayoitia hasara halmashauri.
Mfano hai ni kwamba Mwenyekiti huyo alikuwa mwanzilishi wa mgogoro kati Halmashauri na mtumishi aliyekuwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Nkwenda, Elizeus Baletwa. Mgogoro huu umeisababishia halmashauri hasara kubwa kwa kuendesha kesi ambayo halmashauri imeshindwa.
Akiwa safari ndugu Kashunju huwa hakabidhi ofisi kwa Makamu wake, hivyo Ofisi ya Mwenyekiti huwa haitoi huduma asipokuwepo. Hali hii imeleta usumbufu mkubwa kwa wananchi wanaohitaji huduma katika ofisi hiyo.
Jambo linaloonekana kuwaudhi walio wengi ni pamoja na Mwenyekiti kuwashambulia madiwani kwa maneno yenye vitisho na matusi hasa wale wanaokuwa wametofautiana naye kwenye hoja za msingi katika vikao vya kawaida.
Anatuhumiwa kuwa na mwenendo mbaya na chanzo cha mahusiano mabaya baina ya Halmashauri na taasisi nyingine. Mfano uongozi wa ushirika, Karagwe District Cooperative Union (KDCU), uliomba kukutana na uongozi wa Halmashauri lakini Kashunju akawakatalia kwa makusudi, jambo ambalo limeonyesha dalili za mahusiano mabaya kati ya ushirika na Halmashauri ya wilaya ya Karagwe.
Jamhuri lilipomuuliza tuhuma kuwa yeye ni mkabila, alisema: “Mimi mke wangu ni wa kutoka Morogoro. Sasa kama ni hivyo, ukabila na mimi wapi na wapi? Hao wanaosema hivyo wana lao jambo.”
Alisema ichunguzwe popote akikutwa ametumia vibaya fedha za halmashauri achukuliwe hatua. “Wakati naingia kwenye uongozi mwaka 2006, halmashauri ilikuwa inakusanya Sh milioni 247, leo tunakusanya sh bilioni 3.8. Hivi lipo bora?” alihoji Runyogote.
Kutokana na vyanzo vyetu vya habari, zipo tetesi kuwa tuhuma hizi ziliwasilishwa kwenye kikao cha CCM Mkoa wa Kagera kilichofanyika tarehe Juni 6, 2012 ambacho kilihudhuriwa pia na Pius Msekwa, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Kashunju Runyogote na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Masawe walikuwa wajumbe wa kikao hicho. Haijajulikana kama Msekwa na Masawe walibariki tuhuma hizi zifumbiwe macho. Hata hivyo, ukaribu wa kikao hiki cha tarehe Juni 6, 2012 na cha tarehe Juni 7, 2012 huko Karagwe unaleta hisia za mahusiano kwani haiwezekani Mkuu wa Wilaya ya Misenyi kwenda kuhudhuria kikao Karagwe bila ridhaa ya Mkuu wa Mkoa.
“Tumeshuhudia mawaziri wakichunguzwa au kuwajibishwa. Sasa kwanini tuhuma dhidi ya Kashunju zisichunguzwe ili haki itendeke? Kwa kuzingatia haki za binadamu na utawala bora ni muhimu tuhuma zote zilizoelekezwa kwa Kashunju zichunguzwe ili ukweli ujulikane; Kashunju awe huru baada kuchunguzwa ili kuondoa hisia za kulindwa na kujenga imani kwa utawala wa sasa,” alisema mtoa habari mwingine.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa, alipozungumza na Jamhuri, alisema: “CCM mara nyingi tunamaliza mambo yetu kwa vikao. Kama amerejesha hizo fedha huyo ni mtu mzuri.
“Mimi niliwashauri halmashauri ya Mkoa wa Kagera nikamtuma Katibu kuwa madiwani wale (29) wazungumze waondoe hoja ya kumvua madaraka Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe. Maana si vizuri sana kufukuzana. Unaweza kumfukuza huyu ukakuta unapta mtu mbaya zaidi.
“Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera baada ya kufanya kikao huko Karagwe aliniletea taarifa kuwa mambo yamemalizwa na sasa hali iko shwari, nami namshukuru kwa hilo huyu Mwenyekiti amekuwa muungwana, maana kukiri na kuomba radhi ni uungwana. Hakuna kiongozi aliyekamilika,” alisema Msekwa.