Dhana ya kupambana na ufisadi inahitaji jicho la ziada kutokana na watumishi wa umma kutumia fursa wanazopata kujineemesha nje ya utaratibu rasmi wa kiserikali, uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI, umebaini.

Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe imeingia katika mgogoro mkubwa, baada ya kubainika kuwa aliyekuwa Mwenyekiti Halmashauri hiyo, Joseph Mkundi amedai na kulipwa posho hadi za mwaka 2011, wakati waraka wa kulipa posho wenyeviti wa halmashauri umetoka mwaka 2015.

Kabla ya waraka huo wa Serikali, halmashauri hazikufahamu ni kiasi gani wenyeviti wa halmashauri au meya anapaswa kulipwa na kwa siku ngapi anapofanya kazi za wananchi ofisini.

Aprili 21, mwaka 2015 Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), iliandika barua yenye kichwa cha habari kisemacho; “Ufafanuzi kuhusu posho inayolipwa kwa Mwenyekiti wa Halmashauri au Meya kwa Siku mbii anazoruhusiwa kuja ofisini,” ilirejea Sheria ya Serikali za Mitaa Sura ya 287 na Mamlaka za Miji Sura 288 zikisomwa pamoja na Kanuni za Halmashauri.

M. A. Pawaga, aliyekuwa Kaimu Katibu Mkuu TAMISEMI, anasema katika barua hiyo kuwa wenyeviti wa halmashauri au mameya wanawajibika kufika ofisini mara mbili kwa wiki “kushughulikia masuala ya mbalimbali ya Halmashauri ikiwa ni pamoja na kutia saini nyaraka mbalimbali za Halmashauri zinazohitaji sainii yake, kusikiliza shida za wananchi na kukutana na viongozi mbalimbali wa kiserikali.

“Kutokana na shughuli hizi, Mwenyekiti wa Halmashauri au Meya anastahili kulipwa posho ya kujikimu inayolipwa anapokuwa safarini endapo Mwenyekiti au Meya atalala nje ya makazi yake. Endapo Mwenyekiti au Meya atafanya kazi zake au kurudi nyumbani atastahili kulipwa nusu ya kiwango cha posho ya kujikimu ili imuwezesha kujikimu anapokuwa anatekeleza majukumu hayo,” ulisema ufafanuzi huo wa Serikali. Hata hivyo, inasisitizwa kuwa posho hizo zinapaswa kutokana na mapato yaliyoainishwa kwenye bajeti.

Mwenyekiti wa sasa wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, George Machela Nyamaha ameliambia JAMHURI kuwa baada ya kuingia ofisini amekuta madai makubwa kutoka kwa Mwenyekiti aliyemtangulia Mkundi, na alipohoji akaambiwa ni malimbikizo ya posho alizostahili kulipwa, kutokana na kufanya kazi tangu mwaka 2011 bila kulipwa posho hizo.

Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI, unaonyesha kuwa Aprili 10, 2014 Mkundi alilipwa wastani wa Sh milioni 2.5, Juni 6, 2015 akalipwa Sh milioni 8.0 na Novemba 3, 2015 ikiwa ni wiki moja baada ya uchaguzi, alilipwa Sh milioni 10.

Malipo haya yalifanyika baada ya Mkundi kuwa amemwandikia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Agosti 28, 2014 barua iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho: “Madai ya Posho ya Kujikimu Tokea Januari, 2011 hadi Agosti 29, 2014.” Katika barua hiyo, alipiga hesabu ya madai yake na kuonyesha kuwa anadai jumla ya siku 352 katika kipindi hicho kwa wastani wa Sh 65,000 kila siku kati ya hizo.

“Sasa najiuliza waraka wa ufafanuzi umetoka 2015, yeye anadai fidia tangu mwaka 2011. Tayari amelipwa fedha hizo unazosema. Mimi naona hii si sahihi hata kidogo. Kama ni posho alistahili kupata hizo za kuanzia waraka ulipotoka. Mimi nasema tutamdai posho zetu,” anasema Nyamaha.

Nyamaha, anasema hata maofisa wote wa halmashauri waliohusika na kutoa malipo hayo atahakikisha wanachukuliwa hatua za kisheria kwani waraka uko wazi na haukustahili ‘kuchakachuliwa’ kwa kumlipa posho asizostahili Mwenyekiti huyo ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Ukerewe kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

JAMHURI lilipowasiliana na Mkundi juu ya tuhuma hizo, akasema: “Kuna watu wanatafuta umaarufu kwa kuchafua jina langu na kuchafua rekodi yangu nikiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ukerewe.

“Nimekuwa kiongozi tangu mwaka 2011, na kwa mujibu wa Kanuni Mwenyekiti wa Halmashauri anapaswa awe na siku mbili za kusikiliza matatizo ya wananchi. Kama kiongozi huyo anatoka nje ya eneo iliko taasisi, taasisi ina wajibu wa kum-accommodate kwa siku mbili atakazokuwapo katika eneo hilo.

“Tokea mwaka 2010 mwishoni nilipoanza kutumika, kimsingi sikuwa ninalipwa. Nimekuja kulipwa baadaye baada ya kuwa nimefuatilia, pamoja na kuonyesha kwamba natakiwa nilipwe. Kama kiongozi natakiwa kuwa nalipwa kwa mazingira ya Ukerewe, 65,000. Baada ya kusikia kauli ya waziri, ikaonekana kuwa kuna baadhi ya maeneo wakurugenzi wanakosa kuwa na uhakika walipe nini, ndipo ukatolewa waraka,” anasema Mkundi.

Ameliambia JAMHURI kuwa kazi hii ilimuumiza kwa kiasi kikubwa kwani aliifanya kwa miaka zaidi ya minne bila malipo, na fursa hiyo ya waraka ilipotokea akaona ni vyema adai haki yake yote tangu alipoingia ofisini rasmi mwaka 2011.

Hata hivyo, anasema yeye anakumbuka kuwa hadi sasa amelipwa Sh milioni 10,500, kwa maana ya Sh milioni 2.5 na Sh milioni 8.0: “Hiyo milioni 10 sikumbuki kuipokea hata kidogo. Nitadai hizo fedha ni haki yangu kwani kazi niliifanya na hivyo nastahili malipo kwa kazi niliyofanya,” anasema Mkundi.

Alipoulizwa kwa nini alidai fedha na kulipwa wakati hazikuwa kwenye bajeti zikatolewa kwenye vyanzo vya ndani, Mkundi amesema yeye anachojua ni kwamba anadai haki yake, na mlipaji anapaswa kujua kama anazitoa kwenye bajeti au vyanzo vingine ambavyo navyo ni sehemu ya bajeti.

Taarifa zinaonyesha kuwa nyumbani kwa Mkundi ni Ukara, ambako asingeweza kuja Nansio Ukerewe akafanya kazi na kuondoka akarejea nyumbani kwake.

Hata hivyo, Mkundi alishindwa kujibu swali alikuwa anapata wapi fedha za kusafiri na kujikimu kwa miaka minne kabla ya waraka wa waziri kutoka uliompa fursa ya kudai wastani wa Sh milioni 37,500, ambazo kati yake amekwishalilpwa Sh milioni 20,500 na bado anadai Sh milioni 17.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI, umebaini kuwa wenyeviti na mameya wengi baada ya kutoka kwa waraka huu karibu nchi nzima wamedai malipo hayo, ingawa awali walikuwa wakiwezeshwa na halmashauri zao kufanya kazi kabla ya waraka, kitu ambacho kinatafsiriwa kuwa ni udanganyifu kwa njia ya kupokea malipo mara mbili kwa kazi moja waliyokwishaifanya.