Wenye nyumba hawako salama ikiwa wapangaji wao ni wahusika wa dawa za kulevya. Ni muhimu kulijua hili ili kujihadhari na kile kinachoweza kukuletea madhara. Sheria mpya ya kupambana na kuzuia dawa za kulevya – ‘The Drug Control and Enforcement Act, No 5 of 2015 – imeeleza kwa mapana uhusika wa watu wa kada mbalimbali katika dawa za kulevya.
Tunachotakiwa kujua ni kuwa uhusika haumlengi tu yule mwenyewe mhusika halisi, bali umeelekezwa mbali na hata kufika kwa wenye nyumba au wamiliki wa nyumba/eneo.
Pia uhusiano katika sheria hii haumlengi tu mwenye nyumba na mpangaji wake, bali pia mwenye nyumba na wale walio katika nyumba yake wawe watoto, mke, ndugu, rafiki na kadhalika, madhali ni watu wako katika nyumba yako au eneo unalomiliki basi watakuhusu katika hili.
Hata hivyo, kabla ya kuona hatia ya mwenye nyumba/eneo, tutazame kwanza ni vitu gani vinaitwa dawa za kulevya ili kama unajihadhari ujue lipi la kujihadhari nalo.
1. Ni vitu gani vinaitwa dawa za kulevya
Sheria ya kupambana na dawa za kulevya inataja aina nyingi mno ya vitu ambavyo imeviita dawa za kulevya. Vipo jamii ya kimiminika, jamii ya unga, jamii ya miti, majani, mbegu n.k.
Kifungu cha 2 cha sheria hiyo kinachosomwa sambamba na ‘schedule’ ya 1 ya sheria hiyo hiyo, kimeorodhesha zaidi ya sampuli 100 za vitu ambavyo vinahesabika kuwa ni dawa za kulevya hapa Tanzania. Humo imo pia bangi, mirungi, cocaine, heroin, mandrax, morphine, cannabis resin au opium, coca leaf, alphaprodine, etorphine n.k.
Ni vigumu kuzitaja kwa Kiswahili lakini pia ni vigumu kuzitaja zote kwa kuwa ziko zaidi ya mia. Muhimu ni kuwa jihadhari na mienendo ya wapangaji au wale uliowaweka katika nyumba/eneo lako.
Pia ujue kuwa mirungi nayo ni dawa za kulevya tofauti na wengi wanavyodhani kuwa ni kiburudisho cha starehe halali kama ilivyo sigara au vingine.
2. Hatia ya mwenye nyumba ikiwa mpangaji anahusika na dawa za kulevya
Kifungu cha 19(1) cha sheria hiyo kinakataza mmiliki wa muda au wa kudumu kuruhusu eneo lake kutumika kwa namna yoyote katika shughuli yoyote ya dawa za kulevya.
Mmiliki wa muda anaweza kuwa mwangalizi wa nyumba labda ameachiwa jukumu hilo na mmiliki halisi, au anaweza kuwa mpangaji aliyempangisha mpangaji mwingine (sub-lease). Wote hawa wanaweza kuwa na hatia katika kifungu hiki.
Mmiliki wa kudumu ndiye mmiliki halisi wa nyumba/eneo. Huyu naye anawajibika katika kifungu hiki.
3. Vitu gani usiruhusu vifanyike katika nyumba/eneo lako
Kifungu hicho cha 19 kimeeleza vitu hivyo. Kinasema maandalizi yoyote ya shughuli za dawa za kulevya yasifanyike kwenye nyumba/eneo lako, matumizi yoyote kwa mfano kuvuta bangi, kujidunga, kunusa, kulamba, au kula, kuuza au kununua. Kutumika kama eneo la kutengenezea dawa, kutumia nyumba kama kituo cha kufukishia dawa na aina nyingine yoyote ya shughuli hiyo.
4. Adhabu kwa wenye maeneo/nyumba
Kifungu cha 19(2) kimeainisha adhabu ya faini ya shilingi zisizopungua milioni tano au kifungo kisichopungua miaka mitatu jela, au vyote viwili.
Kwa makala hii ni vema sana kwa wenye nyumba kujihadhari na shughuli zinazofanywa na wapangaji, au yeyote anayekaa katika nyumba/maeneo yao. Usiseme simo na hali unajua kinachoendelea, kwa mujibu wa sheria hii umo.
Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.