Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Mwenge wa Uhuru,umepitia na kuridhishwa na mradi wa ujenzi wa Kongani ya viwanda ya KAMAKA ,Disunyara, Kibaha Vijijini Mkoani Pwani, ambapo hadi kukamilika itatumia gharama ya Trilioni 3.1 na kutoa ajira 200,000.
Akitembelea mradi huo, kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa, Abdallah Shaib alieleza Serikali inaendelea kushirikiana na wawekezaji ili kuinua sekta ya uwekezaji na viwanda.
“Nawapongeza wawekezaji wazalendo,huu ni mfano wa kuigwa, Serikali inatambua mchango wao,” amesema.
Shaib alieleza kongani hiyo inakwenda kuleta tija, kuongeza ajira na kukuza pato la Taifa.
Kiongozi huyo,ametoa wito kwa Watanzania wenye uwezo,wajenge uthubutu na kuwa wazalendo kujenga uwekezaji mkubwa kama huo.
Akitoa taarifa ya mradi huo Nelson Mollel,kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, alieleza kati ya fedha hizo Bilioni 122.4 itatumika katika miundombinu ndani ya miaka mitano hadi sasa Bilioni 31.7 zinatumika kwenye awamu ya kwanza ya miundombinu.
“Katika mradi huu viwanda zaidi ya 200 vitajengwa kati ya hivyo ni viwanda tisa vikubwa na vingine vitakuwa vidogo na vya kati, na eneo la ujenzi ni hekari 1,000″alibainisha Mollel.
Mollel alifafanua, lengo la ujenzi ni kutii wito wa Serikali kujenga viwanda na kukuza uchumi,kuongeza fursa za kiuchumi katika uzalishaji wa ajira.
Pia kulinda hifadhi ya mazingira kujenga viwanda vingi kwenye eneo moja badala ya kujenga viwanda vingi kwa maeneo mbalimbali.
Awali Akipokea Mwenge huo Vikuruti,Kibaha Vijijini ukitokea Bagamoyo,Mkuu wa Wilaya ya Kibaha,Nikkison Saimon ameeleza, Mwenge ukiwa wilayani humo unapitia miradi 26 yenye thamani ya trilioni 3.1 katika Halmashauri mbili ya Kibaha Vijijini miradi 14 na miradi 12 Kibaha Mjini .
Kati ya miradi mingine iliyopitiwa Kibaha Vijijini,ni pamoja na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara kutoka Bandari Kavu kwenda kongani ya viwanda ya Sinotan.
Kuweka jiwe la msingi jengo la wagonjwa wa nje (OPD) Zahanati ya Vikuruti,ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa shule ya Sekondari Disunyara ambao umezinduliwa.
Kufungua mradi wa ujenzi wa jengo la upasuaji na wadi kituo cha afya cha st.Michael, kuweka jiwe la msingi mradi wa maji Kijiji cha Ruvu Stesheni.