Na Joe Beda Rupia

Usipokuwa makini unaweza kudhani mambo ni shwari katika kampuni ya mabasi yaendayo haraka, UDART, ya jijini Dar es Salaam. 

Hakuna anayesema ukweli. Hakuna anayewasemea. Hakuna anayewajali. Wadau wamekaa kimya. Wamewatelekeza na wao wenyewe ni kama wameamua kufa na tai shingoni.

Ukiyaona mabasi yanavyopita kwenye barabara zake maalumu kati ya Kimara – Kivukoni – Gerezani  na Morocco, utadhani mambo ni shwari.

Takwimu zinazotolewa nazo zinavutia. Kwamba idadi ya abiria wanaosafirishwa kwa siku inaongezeka. Takwimu. Ni makaratasi tu. Makabrasha. Kuna ukweli?

Majuzi wahariri tukaambiwa kuwa mradi huu ambao bado upo katika kipindi cha mpito kilichorefushwa kutoka miaka miwili hadi kuwa cha kudumu sasa, una mabasi 210. Takwimu tu hizi. Nazo ni za uongo.

Kwamba ili mradi ufanye kazi kwa ufanisi unapaswa kuwa na mabasi 305 (hii ni kweli). Kwa hiyo kuna upungufu wa mabasi 95. Inawezekana kuwa ni kweli pia. Ni tafiti ingawa ni za zamani sana sasa. Zaidi ya muongo mmoja.

Ukiwa kwenye vituo vya mwendokasi kwa sasa huioni hadhi na heshima ya mradi huu, wala huoni uendelevu wake, mradi umechakaa kabla ya kuanzia huduma kamili. 

Mabasi hayatoshi. Yake 70 mapya nayo hayatumiwi kimkakati ili kuyaokoa ya zamani yaliyokuwa yameelemewa. Kuna vituo watu wanakaa kwa muda mrefu mabasi hayasimami. 

Mfano ni Kituo cha Usalama. Lakini kweli wanayo mabasi 210? Jibu ni hapana. Kuna mabasi kadhaa hayana uwezo wa kutembea tena barabarani. Written off.

Hili halisemwi. Lakini kulisema si dhambi! Muda unakwenda, mabasi yanachakaa kwa kuwa yanafanya kazi kila siku. Haiwezekani kabisa kuwa yale mabasi 140 ya awali yaliyoanza kazi Mei 2016 leo hii yote ni mazima! Hapana.

Kuna moja liliteketea kabisa kwa moto Kimara. Mengine kadhaa yalikumbwa na mafuriko mfululizo yaliyowahi kutokea Jangwani. Mengine vipuri vyake vilihamishiwa katika mabasi mengine.

Hivyo kama mpango wa awali ulihitaji mabasi 305 na sasa yapo 210 huku mengine yakiwa written off, maana yake ni kwamba mradi haufanyi kazi kwa ufanisi uliokusudiwa! Hili halisemwi.

Ikiwa korido asilia; Kimara – Kivukoni – Gerezani na Morocco (pamoja na barabara zake za mlisho) ilihitaji mabasi 305 lakini yanayofanya kazi ni kama 120 au 140, basi hakuna ufanisi. Tuwe wakweli.

Sawa, hebu tuseme kuna mabasi 210, hakuna lililoteketea kwa moto wala yaliyokumbwa na mafuriko, siku hizi kuna mabasi yanakwenda Mwenge, Kibaha, Mloganzila na kwa Magufuli!

Ruti hizi mpya zinapunguza mabasi kwenye korido asilia iliyokuwa ikihitaji mabasi 305! 

Kwa hiyo ruti asilia imebaki na ‘business as usual’. Bora liende. Hakuna jipya. Hakuna ustaarabu. Matarajio ya wananchi yamefifia hadi yamekufa kabisa.

Mradi huu kwa sasa si wa mfano tena. Wageni hawaji au hata kama wanakuja hawatangazwi, kwa kuwa hawavutiwi tena.

Benki ya Dunia imebaki mdomo wazi. Mradi uliovuma na kupigiwa mfano kila kona ya dunia, upo upo tu kwa sasa. Wenye dhamana nao wanatazamana tu na kutoa takwimu feki.

Mficha uchi hazai. Hivi kwa nini wahusika wananyamaza badala ya kuwaambia ukweli wakubwa kuwa mradi huu unakwenda kwa kudra za Mwenyezi Mungu?

Covid – 19 iliupiga mradi huu na sote tu mashahidi, sasa kwa nini haujapata fedha zilizotolewa na serikali kuchechemua uchumi?

Zile Sh trilioni 1.3 zilizoelekezwa kujenga madarasa na maeneo mengine, kama Mwendokasi wangekuwa wa kweli, wangemwambia Rais Samia Suluhu Hassan ambaye mradi upo chini yake (TAMISEMI) angewatengea bilioni kadhaa kuuokoa mradi.

Mawazo ya DART kwa sasa yapo kwenye awamu nyingine za mradi (Mbagala na Gongo la Mboto), lakini je, wamefanikiwa vipi katika awamu ya kwanza? Kwa kweli hawajafanikiwa.

Kuna fedha kiasi gani zimetengwa kwa ajili ya kununua mabasi mapya? Life span ya mabasi yale 140 ni miaka minane. Maana yake yanakaribia kufika mwisho. Je, serikali italazimika kununua mabasi mengine mapya kwa kuwa mradi haujaweka ajiba? Inasikitisha sana.

Mradi unaendeshwa kienyeji tu. Ni kama kampuni kubwa ya daladala. Tangu ulipozinduliwa na Rais Magufuli Januari 25, 2017, hakuna kitu chochote kipya kilichoongezeka.

Lau kama wangepata fedha za COVID (ambazo wanastahili) huenda kungefanyika uboreshaji wa aina fulani ndani ya mradi.

Hivi kwa nini imeshindikana kuwa na tiketi za kielektroniki? Kwa nini vituo vingi vimefunguliwa mlango mmoja tu? 

Mradi huu utakufa na ili kuukoa kuna mambo mawili yanayopaswa kufanywa; serikali kuupa ruzuku au kuongeza nauli.

0679 336 491