DAR ES SALAAM

NA AZIZA NANGWA

Kampuni inayoendesha mradi wa mabasi ya mwendokasi jijini Dar es Salaam, UDART, imekiri kuzidiwa wingi wa
abiria kutokana na uchache wa mabasi inayoyamiliki.
Kampuni hiyo imekiri kuwa msongamano wa abiria katika mabasi na abiria kukaa muda mrefu vituoni wakisubiri
usafiri kunatokana na uchache wa mabasi.
Ofisa Habari wa UDART, George Ntevi, anasema hali ni mbaya zaidi katika kipindi hiki cha mvua, hasa pale
wanapolazimika kusitisha huduma kutokana na eneo la Jangwani kujaa maji, hivyo kutopitika.
Anasema hivi sasa kampuni hiyo ina mabasi 140 tu wakati yanahitajika mabasi kama 300 ili kutoa huduma nzuri
kwa Jiji la Dar es Salaam.
“Tena katika hayo mabasi 140 tuliyonayo, yapo mengine ambayo ni mabovu, hivyo hayafanyi kazi,” anafafanua Ntevi.
Anasema kujaa maji eneo ya Jangwani kuliathiri sana mabasi yao, kwani mengi yaliharibika wakati makao makuu ya kampuni yakiwa katika eneo hilo. Hivi sasa UDART imehamishia ofisi zake katika eneo la Ubungo Maji.
Ntevi anasema ili kukabiliana na tatizo hilo, serikali imo katika mchakato wa kuagiza mabasi mengine kutoka nje ili
kukidhi mahitaji yaliyopo.
“Utafiti umefanyika na kubaini kuwa kuna watu milioni moja wanatembea kwa miguu kila siku kutokana na
upungufu wa magari, hivyo kuja kwa mabasi hayo kutapunguzza tatizo hilo,” anafafanua.
Kuhusu malalamiko ya nauli kwa abiria wanaodai kulipishwa mara mbili kutokana na kulazimika kushukia Jangwani
wakati wa mafuriko, Ntevi anasema kwa kawaida inapotokea eneo la Jangwani kufungwa, kampuni hiyo imekuwa ikitoa matangazo na taarifa kwa abiria.
“Huwa tunawatangazia kabisa kuwa mabasi yanayotoka Kimara yataishia Magomeni, na yale yanayotoka Posta na
Kariakoo yataishia Faya. Hivyo abiria anapaswa kulifahamu hilo,” anasema.
Anasema kuwa abiria wengi wanashauriwa kushuka Magomeni na kupanda mabasi ya Morocco, ili iwe rahisi
kupata usafiri wa mabasi ya kawaida yanayokwenda mjini kwa haraka.
Wiki iliyopita maelfu ya wakazi wanaotumia usafiri wa mwendo kasi walikumbwa na matatizo makubwa baada ya
eneo la Jwngwani kujaa maji, hivyo kutopitika kwa magari ya aina yoyote.
Akizungumza kwa niaba ya abiria wenzake, Maulid Khalifan, mkazi wa Kimara Korogwe, anasema kuwa wamiliki hao wa mabasi wamewafanya wao kuwa kitega uchumi kwani kila unapofikia msimu wa mvua wamekuwa wakiwalipisha nauli
mara mbili kwa safari za kwenda Kivukoni na Gerezani.
Khalifan anasema matope yaliyokuwepo katika eneo hilo si matope ya kukosa kuzolewa na vyombo husika ili
magari yaweze kupita kwa urahisi na kuwaondolea adha abiria wanaotumia barabara hiyo.
“Ndugu mwandishi, abiria tunasumbuka sana hasa kipindi hiki, kwani tunalazimika kulipa nauli mara mbilimbili kisha
tunaogelea mitope ya kuvuka au kukodisha pikipiki kwa gharama zetu. Halafu tukifika katika kituo cha Faya tunalipa
tena nauli, hivyo jumla ninakuwa nimelipa Sh 1,300 kwa safari moja. Kwa nini sasa wasipunguze nauli kipindi cha
mvua iwe Sh 400 tu kwa safari?” anahoji.
Naye Nusura John, mkazi wa Mkwajuni anasema kuwa utaratibu wa mabasi hayo umekuwa mbovu kwa kipindi
kirefu kwani hata siku za kawaida yamekuwa ni kero kwao kutokana na mabasi hayo kujaza watu kupita kiasi, kitu
ambacho kinaweza kusababisha magonjwa kwa abiria wanaotumia mabasi hayo.