Shirika la Misaada la Uingereza (UKAID) kwa kushirikiana na Benki ya Dunia wamezindua kampeni ya matangazo ya mwezi mmoja kuhamasisha jamii mbinu za kukabili mafuriko.

Kampeni hiyo itakayohusisha mradi wa mabasi yaendayo haraka (UDART), imezinduliwa katika kituo cha mabasi yaendayo haraka cha Kivukoni. Imehusisha basi lililobandikwa matangazo yanayohamasisha utokomezaji taka, hasa za plastiki zinazosadikiwa kuwa miongoni mwa vyanzo vya mafuriko jijini Dar es Salaam.

Ingawa matangazo hayo yatadumu kwa mwezi mmoja, kampeni hiyo itadumu kwa miaka mitatu ikihusisha ujenzi wa miundombinu ya majitaka.

Itajikita katika kuelimisha umma madhara yanayotokana na mafuriko jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Kitengo cha Biashara na Masoko wa UDART, Tumaini Magila, amesema kampeni hiyo ni muhimu kwa kuwa inawafikia watu wengi haraka.

“Mabasi yetu yanabeba asilimia zaidi ya 40 ya wakazi wa Dar es Salaam,” amesema Magila.

Amewashukuru UKAID na Benki ya Dunia kwa kuyatumia mabasi yao, akisema UDART ni miongoni mwa waathirika wa mafuriko.

Amesema kupitia matanagazo hayo, wakazi wa Dar es Salaam pia wataelimika kuhusu madhara ya matumizi ya chupa za plastiki.

Naye Mwakilishi wa UKAID hapa nchini, Beth Arthy, amesema wameanzisha kampeni hiyo ili kusaidiana na serikali kufanikisha malengo ya kimaendeleo, yakiwamo ya uchumi wa viwanda.

Amesema kwa kushughulikia visababishi vya mafuriko ndani ya Jiji la Dar es Salaam, usalama wa ajira na afya za watu utaongezeka.

Kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, Serikali ya Uingereza inachangia dola zaidi ya milioni 100 za Marekani kutengeneza miundombinu ya majitaka na madaraja.

“Mradi huu utatekelezwa ndani ya miaka mitatu na utaokoa hasara za kiuchumi na upotevu wa maisha ya watu kunakosababishwa na mafuriko,” amesema.

Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini, Bella Bird, amesema kampeni hiyo itaongeza uelewa wa wananchi kuhusu madhara ya taka ngumu, hasa za plastiki.

Amesema utafiti wa mwaka 2016 unaonyesha tani zaidi ya milioni 240 za taka zilizalishwa duniani kote. Amesema miaka 30 ijayo hali ya taka zinazozalishwa itaongezeka kwa asilimia 17.

Kwa Dar es Salaam, amesema takriban tani 4,500 za chupa za plastiki huzalishwa kila mwaka. Robo ya taka hizo zinaishia kwenye mifereji ya maji.

“Na tunachoweza kuona kama matokeo ya taka hizi ni mafuriko. Sitaki kuwaambia wakazi wa Dar es Salaam kuhusu nini kinatokea mafuriko yanapokuja,” amesema Bella.

Ameipongeza serikali, UDART na washirika (UKAID) kwa kushirikiana na Benki ya Dunia katika kampeni ya kuhamasisha uelewa kuhusu taka ngumu kwa wakazi wa Dar es Salaam katika kutokomeza taka za plastiki.

“Nafikiri yote yanaanza na uelewa, sisi wote tunatumia plastiki, na tumeona kupitia kwenye hii kampeni na data zilizopo ni kwa kiasi gani tunatakiwa kuwa makini na matumizi ya plastiki katika kulinda mazingira yetu na dunia,” amesema Bella.

Tathmini inaonyesha kuwa tani milioni 8 za plastiki huingizwa nchini kwa mwaka; huku asilimia 75 ya taka katika Jiji la Dar es Salaam ni plastiki.

Chupa za plastiki milioni moja huzalishwa kila baada ya dakika moja ulimwenguni kote na ni asilimia 35 tu ya taka zote, zikiwemo chupa hupelekwa katika vituo vya taka.

Utafiti umebaini kuwa siku tatu za mafuriko ndani ya Jiji la Dar es Salaam husababisha hasara ya Sh bilioni 230.