Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Karim Khan, amewasili katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa lengo la kuimarisha juhudi za kuchunguza uhalifu unaoripotiwa kufanyika katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo.

Ziara yake inafanyika wakati ambapo hali ya usalama inazidi kuzorota, huku mamia ya watu wakiripotiwa kuuawa na maelfu kujeruhiwa kutokana na ghasia zinazoendelea.

Akiwa nchini humo, Khan anatarajiwa kukutana na maafisa wa serikali, wawakilishi wa MONUSCO, waathirika wa machafuko, pamoja na mashirika ya kiraia ili kujadili hatua zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya wahusika wa uhalifu huo.

“Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu kuendelea kwa machafuko katika eneo hili,” alisema Khan. “Hakuna kundi lenye silaha wala jeshi lolote linaloshirikiana nao litakaloweza kukwepa uwajibikaji. Ni muhimu kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu.”

Alisisitiza kuwa Mkataba wa Roma lazima utekelezwe kwa ufanisi ili kuhakikisha wahusika wa uhalifu wanawajibishwa ipasavyo.

“Hakuna mtu anayepaswa kujeruhi au kushambulia raia na kisha kubaki bila kuchukuliwa hatua,” aliongeza. “Huu ni wakati wa kuona kama ICC itaweza kuwaletea wananchi wa DRC haki wanayostahili.”

Aidha, alilinganisha hali ya DRC na mizozo mingine duniani kama vile Palestina, Ukraine, na Israel, akisisitiza kuwa raia wa DRC wanapaswa kupata haki sawa na watu wengine duniani.

Katika ziara hiyo, Khan atakutana na Rais FĂ©lix Tshisekedi pamoja na maafisa wa serikali ili kujadili hatua zitakazofuata. Pia atafanya mazungumzo na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hapo kesho, Jumanne.

Ziara hii inadhihirisha jitihada za ICC katika kuhakikisha haki inapatikana na kuwachukulia hatua wale wanaohusika na uhalifu katika maeneo ya mashariki mwa Congo.

Tangu Oktoba 2024, ofisi ya mwendesha mashtaka huyo imekuwa ikichunguza madai ya uhalifu wa kivita yanayodaiwa kufanyika katika jimbo la Kivu Kaskazini mnamo Januari 2022.

Mnamo Mei 2023, Rais Tshisekedi aliwasilisha rufaa kwa ICC akitaka uchunguzi ufanyike kuhusu vitendo vya uhalifu vinavyodaiwa kufanywa na vikundi vya waasi tangu Januari 2022.

Mahakama ya ICC ina mamlaka ya kushughulikia makosa yaliyofanyika baada ya tarehe 1 Julai 2002, wakati Mkataba wa Roma ulipoanza kutumika.

Tayari DRC imeshuhudia baadhi ya wahalifu wa kivita wakifikishwa mbele ya ICC na kuhukumiwa, wakiwemo Jean Pierre Bemba, Thomas Lubanga, na Bosco Ntaganda.