Imeelezwa kuwa mwendelezo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kutunukiwa shahada za heshima za falsafa na vyuo vyenye hadhi ya juu duniani ni kiashiria cha kutambua kazi kubwa inayofanywa na Mwanadiplomasia huyo namba moja nchini.
Katika mwendelezo huo Juni 03, 2024, Chuo Kikuu cha Anga nchini Korea kilimtunukia Rais Samia shahada ya heshima ya falsafa ya masuala ya usafiri wa anga katika hafla iliyofanyika chuoni hapo na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa chuo hicho.
Wakati anamtunuku shahada hiyo, Rais wa chuo hicho, Prof. Hee-Young Hurr alimtaja Rais Samia kama kiongozi mwenye maono aliyofanya mabadiliko makubwa kwa ajili ya ustawi wa wananchi wake na amekua mstari wa mbele kuibua na kusimamia utekelezaji wa agenda zenye manufaa duniani.
Rais Samia alitukunikiwa shahada hiyo ya heshima kutokana na jitihada kubwa anazofanya za kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na ununuzi wa ndege, ujenzi wa viwanja vya ndege, ukarabati wa viwanja vya ndege na ununuzi wa vifaa vya kuongozea ndege kama rada, n.k.