DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu   

Mapendekezo ya kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa huenda yakafanikisha kuleta mwelekeo mpya wa mwenendo wa siasa za hapa nchini.

Baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kupokea taarifa ya awali ya Kikosi Kazi hicho Ikulu, Dar es Salaam wiki iliyopita amesema: “Kwa hiyo niseme kikosi kazi hiki madhumuni ya kukiunda ni kama utangulizi wa ripoti yenu ulivyoonyesha. Kuyabaini na kuyachambua yale yote ambayo hayatuletei siasa zenye tija ndani ya nchi yetu, yale yanayokwaza demokrasia ndani ya nchi yetu, yale yote ambayo yanafanya siasa zetu hapa nchini ni za chuki na tunatokaje huko na tunakwenda katika laini iliyonyooka.

“Kama mfano wetu kule Zanzibar tulivyo, tulianza hivi, chokochoko ndogondogo, ukawa ugomvi mkubwa, malumbano yakakua, lakini tukafika mahali tukasema kwanini? Kwanini twende hivi? Sisi wote Wazanzibari, wote wa visiwa hivi, kwanini twende hivyo? Tukakaa, tukazungumza mambo yakanyooka, sasa hivi tunakwenda vizuri. Lakini kama nilivyosema, lengo letu ni kuwa na siasa zenye tija.”

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa, wameitafsiri kauli hii kuwa Rais Samia anataka kuona mwelekeo mpya wa siasa, zikiwamo siasa shirikishi badala ya utaratibu wa sasa ambapo mshindi anachukua kila kitu.

“Mfano mzuri ni uchaguzi wa mwaka 2015. CCM ilipata chini ya asilimia 60. Chadema walizoa karibu asilimia 40, lakini katika kuunda Serikali, huwaoni Chadema hata kwenye halmashauri za wilaya. Hii si sawa.

“Tuna mifano hai mingi. Nchi kama Israel, Italia, Japan, Ujerumani na nyingine nyingi duniani ziliondoa siasa za ubabe na visasi kwa kutumia mfumo wa uwiano katika ushindani.

“Kila chama cha siasa kinapata uwakilishi serikalini kulingana na idadi ya kura kilozopata. Hii inaondoa malalamiko, inafungua milango ya kuaminiana na namshukuru Rais Samia kuliona na kuliwaza hilo.

“Zanzibar kwa sasa imetulia, amani na upendo vimetamalaki chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Kama imewezekana Zanzibar, Tanzania Bara inashindikanaje?,” amehoji mchambuzi wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) aliyeomba asitajwe jina gazetini.

Profesa Mukandala

Awali, akiwasilisha mapendekezo hayo, Mwenyekiti wa Kikosi Kazi hicho chenye wajumbe 25 kutoka vyama vya siasa, asasi za kiraia, wanazuoni na watumishi wa umma, Prof. Rwekaza Mukandala, amesema kuna mambo yanayotakiwa kutekelezwa ndani ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu.

“Baada ya kikao hicho, kazi iliyofuata ilikuwa ni kuboresha taarifa ya awali iliyowasilishwa kwako kwa kuzingatia maelekezo yako na pili ilikuwa kuandaa taarifa ya awali na mpango kazi na kuiwasilisha kwako,” amesema na kuongeza:

“Kikosi kazi kimeandaa mpango kazi kwa kuzingatia muda wa kukamilisha kazi, kalenda ya uchaguzi wa mwaka 2025, mchakato wa kuandika Dira ya Taifa ya Maendeleo na maslahi mapana ya ya Taifa. Mpango kazi huu utazingatia muda.

“Yaani masuala ya muda mfupi ni yale yatakayofanyiwa kazi na kukamilishwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu tangu kikosi kuanza kazi, masuala ya muda wa kati ni yale yatakayofanyiwa kazi na kukamilika tangu sasa hadi muda wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Masuala ya muda mrefu ni yale yatayoanza kufanyiwa kazi baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.” 

Ametaja miongoni mwa mambo ya kutekelezwa katika muda mfupi kuwa ni mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa,huku muda wa kati ukiwa kuwapo kwa mfumo bora wa usimamizi wa uchaguzi na muda mrefu ukiwa ni mchakato wa kupata Katiba mpya baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Kuhusu Katiba mpya, amesema kuna watu wanadai mchakato wa kupata Katiba Inayopendekezwa haukuwashirikisha kwa sababu kuna wajumbe wa Bunge Maalumu walisusia na kuna wanaosema kuipata Katiba Mpya ni muhimu, lakini haina haraka kwa kuwa ya sasa inafanya kazi vizuri.

“Hapa suala la kufanyiwa kazi ni kupendekeza utaratibu wa kuipata na muda wa kufanyiwa kazi. Kikosi kinapendekeza uanze mchakato wa kupata Katiba mpya baada ya Uchaguzi wa mwaka 2025.

“Pendekezo hili linatokana na sababu kuu nne; moja, kuna haja ya kuainisha dira mpya ya maendeleo ya miaka ijayo, itakayotoa mwelekeo wa Katiba mpya… Pia kuna suala la kukosekana kwa muda wa kutosha kuanza kutumia Katiba mpya ndani ya kalenda ya uchaguzi 2025,” amesema.

Kuhusu umuhimu wa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, amesema kumekuwa na malalamiko ya kisheria na kimuundo kwamba Tume zote mbili za uchaguzi si huru.Pia kuna madai kwamba baadhi ya watendaji wake wanakiuka sheria na kanuni za kusimamia uchaguzi.

Katika hatua nyingine, amesema kuna malalamiko ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kusimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wakati si jukumu lake.Amesema hatua hiyo inasababisha ugumu wa ofisi hiyo kutekeleza majukumu yake.

“Kikosi Kazi kimebainisha masuala yanayotakiwa kufanyiwa kazi ikiwamo kutathmini mifumo ya uchaguzi, kubainisha na kupendekeza mfumo mzuri zaidi katika taifa,” amesema na kuongeza:

“Pia kubainisha maana ya Tume Huru ya Uchaguzi na kupendekeza hatua za kuimarisha uhuru wa Tume hizo mbili na tunapendekeza maboresho yanayotakiwa kufanyiwa kazi katika sheria na kanuni za uchaguzi.”

Rais Samia

Akijibu hoja za Kikosi Kazi, hicho kilichoundwa baada ya kumalizika kwa mkutano wa siku tatu wa wadau wa demokrasia ya vyama vya siasa uliofanyika Dodoma mwaka jana, Rais Samia amemtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Dk. Pindi Chana, kukaa pamoja na Waziri wa TAMISEMI, Innocent Bashungwa na baadhi ya wajumbe kuangalia namna bora ya mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

“Uchaguzi TAMISEMI usimamiaji wake ukoje? Waziri huko hapa, kaeni na Waziri wa TAMISEMI na baadhi ya wajumbe hapa chaguaneni muone how best tunaweza kufanya huo uchaguzi, nani asimamie uchaguzi wa TAMISEMI na kwanini?

“Na kwanini si chombo cha sasa hivi na kwanini na tuitoe hiyo taarifa vizuri, kwa sababu uchaguzi wa Serikali za Mitaa nadhani ni mwaka 2024 na tuwe tumefanya huo uchambuzi na tujue tunaelekea wapi, huyu kwanini?Nani huyu?

“Asiwe huyu kwanini?Kitu fulani kwanini? Hadi kieleweke, tuelewe vizuri, hadi wote waelewe halafu tuone njia ya kupita, tunaweza kupita katikati kama si TAMISEMI au TAMISEMI nusu na nani mwingine wasimamie pamoja” amesema.

Kuhusu kanuni za mikutano ya hadhara, amesema ana matumaini limeshaanza kufanyiwa kazi na muda si mrefu Waziri mwenye dhamanaatawasilisha mpango wa namna zitakavyokuwa.

“Yameelezwa mambo mengi na mwenyekiti, mambo ya kanuni za mikutano ya hadhara ambalo ndilo jambo letu la muda mfupi, ni matumaini yangu hii kazi mmeshaianza na inaendelea vema na muda si mrefu mtatuwakilishia draft ya kanuni ili ziende katika channel zinazohusika na ziweze kupitishwa ili demokraia ichukue mkondo wake.

“Lakini si tu kanuni ya kusema sasa tuanze, lakini anayekiuka kanuni afanyweje pia nalo liende huko. Kwa hiyo tunategemea muda si mrefu, suala zima la kanuni za maadili za vyama vya siasa, ni kweli tuna vyama vya siasa, vingine vile vikubwa vina kanuni zao vimejiwekea, vidogo vina kanuni zao vimejiwekea, lakini nadhani kungekuwa na kanuni za ujumla na vyama vyote vya siasa vingefuata kitaifa, halafu kuna zile ndogondogo za wenyewe, uko ndani wakajiwekea wenyewe,” amesema.

Katika hatua nyingine, amesema kuna baadhi ya vyama vya siasa havigusi uwiano wa kijinsia na vingine vinajitahidi kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini vingine bado havijafikia na kikosi hicho kitaona jinsi ya kuelekeza na amewataka wanawake waingie katika uongozi katika vyama vya siasa wakitambua wajibu na majukumu yao na wawe na ajenda.

“Hizo kanuni kwa vyama vya siasa ilimradi tu zisiwe za kukandamiza na vizuri mtakuwa wenyewe, mnazitunga na kelele zinapokuwa kali ni nyinyi mtaangalia, zisikandamize, zisiue vyama vya siasa na zilete siasa zenye tija ndani ya nchi.

“Lakini si kila siku tuko CNN na BBC, ukifungua huko Tanzania imefanya hivi, si ustaarabu kwa kweli, kwa hiyo twende na siasa ambazo zitakuwa zenye tija.Siasa zinakwenda, maendeleo yanakwenda na nchi inakwenda,” amesema.

Pia amesema elimu ya sheria za vyama vya siasa na mambo yake iunganishwe na elimu ya uraia.

Amesema Kikosi Kazi hicho kikijipanga na kushirikiana na baadhi ya wajumbe wake wanaweza kutoa elimu ya sheria ya vyama vya siasa na kanuni zake zitakazotungwa.

“Kwa sababu sasa hivi wanasema sheria zipo za Jeshi la Polisi na vyama vya siasa na zinafanya vizuri, kwanini kanuni? Wanatafuta tu sababu ya kutoruhusu, sasa hapo ndipo pa kuanzia; elimu ya siasa inasemaje?Sheria ya vyama vya siasa inasemaje?Sheria ya Jeshi la Polisi inasemaje?” amesema na kuongeza:

“Kanuni mnazozitunga zinasemaje? Mnazichambua vizuri?Watu waelewe vizuri.Twende huko.Mkitoka hapo tunaingia yale makubwa sasa.

“Elimu ya uraia si peke yenu, kuna vyombo vingi ambavyo itabidi viingizwe kwenye elimu ya uraia, vikiwamo vyombo vya kidini na lazima wenyewe watusaidie elimu ya uraia kule kama ninavyosema siku zote, sisi viongozi wa kiserikali na siasa tukisema yanakwenda kichwani kwa wafuasi wetu.

“Lakini viongozi wa dini wakisema yanaingia ndani ya mioyo. Sasa viongozi wa dini mtusaidie kutafuta aya huko, kutafuta mistari huko inayoendana na haya tunayoyafanya na muyafafanue vizuri.”

Kuhusu suala la rushwa, amesema linataka elimu kubwa kwelikweli na Kikosi Kazi hicho kiende kikafanye kazi kisha kije na majibu ya namna ya kufanyiwa kazi, kupunguzwa na kuondolewa.

“Sisi viongozi tunasimama hapa kusema rushwa, rushwa, jamani rushwa, nataka niwaambie wajumbe, leo hii mkipewa majimbo kasimamieni mtazitoa kwa njia moja au nyingine, kwa sababu nyingi, kunakutoa na kuna wajumbe kuzitaka.

“Kwa hiyo hapo kuna kazi kubwa ya kufanya, tufunge mioyo ya wajumbe na mioyo ya watoaji na nini kiwepo hapo kuhusu hiyo rushwa, kwa kuwa kuna sababu za watu kunyoosha mikono ni zipi?Mnaziondoaje na tunazipunguza vipi?

“Kwa hiyo hili dude si kwa serikali, si kwa vyama vya siasa, yaani ni tatizo letu Tanzania. Bado kuna kazi kubwa ya kufanya.Kwa hiyo nendeni chemsheni kichwa, muonyeshe sababu kwanini na zinaondokaje na zinapunguzwaje ili mikono isikunjuke kwa kiasi hicho.Hili suala huwezi kumkuta mtu mmoja, ni letu sote,” amesema.

Kwa upande wa ruzuku za vyama vya siasa, amesema hataki kulitolea ufafanuzi na akakiagiza Kikosi Kazi hicho kikalifanyie kazi na waje na majibu, kwa sababu hata akisema fedha ataitoa wapi?

“Naitoa wapi fedha?Sina pa kuitoa, kwa hiyo twendeni tukachemshe vichwa wote, lakini wakati mwingine unaposema sawa, utaitoa wapi?Tukisema kila chama cha siasa kinapata ruzuku tutakuwa kama Lesotho, kila baada ya siku mbili chama cha siasa kitaundwa, watu wanataka ruzuku.

“Hiyo haitawezekana, unapoanzisha chama umejipangaje?Utakiendeshaje? Unategemea serikali ikuendeshee chama chako cha siasa?Ruzuku kweli ipo kwa wale wanaofanya kazi, wako bungeni wanafanya kazi.Wanasema hao unawapa ruzuku, lakini je, hivi vingine tuviue? Sasa hilo tunawaachia nyinyi kachemsheni kichwa tujue tunafanya nini,” amesema.

Kuhusu Tume Huru ya Uchaguzi amekipa kazi Kikosi Kazi, hicho na watapeleka mapendekezo ni nini na iweje na akakitaka kiangalie waliokuwa nazo je, hawana migogoro ya siasa?

“Kwa mfano majirani zetu, wanazo, lakini zinaendeshwaje? Hawana migogoro?Hawatangazi matokeo wakakimbia nchi kabisa? Nendeni katika nchi mbalimbali angalieni zinaendaje, lakini tunaposema huru tunafuata nini hasa huko?Kitu gani kinachotupa kiu tunahisi tutakipata katika Tume Huru na maana ya Tume Huru ni nini?

“Pengine inawezekana tukifanya maboresho wala zile kelele za Katiba mpya huko na mengine yote yakaisha kwa sababu zile kiu za watu kutaka Katiba ibadilishwe itakuwa imeshashughulikiwa, kwa hiyo twendeni tujipange, tuyachambue kwa undani,” amesema.

Baada ya kuwasilisha mapendekezo ya awali, Kikosi Kazi sasa kitakaa na kushirikisha wataalam katika nyanja mbalimbali kupata mapendekezo yao kisha kuwasilisha kwa Rais maoni ya wadau kwa nia ya kumaliza misuguano ya kisiasa nchini na kuendesha siasa za kistaarabu.