Uhusiano kati ya Mwekezaji wa Shamba la Kapunga (Kapunga Rice Company) lililopo Wilaya ya Mbarali mkoani hapa na wananchi umezidi kufifia kutokana na matukio yanayozidi kumwandama.
Baadhi ya matukio yanayomfanya mwekezaji huyo kuwa na uhusiano mbovu na wanakijiji wanaozunguka shamba lake ni pamoja tukio la hivi karibuni amabpo mwekezaji anadaiwa kupulizia sumu mashamba ya wenyeji na kuunguza mazao yao.
Kutokana na hali hiyo mwekezaji alifikishwa mahakamani ambapo kesi inaendelea huku baadhi ya wahanga wa sumu ile wakiiomba mahakama kumfukuza kabisa mwekezaji huyo.
Mashtaka ya awali yalisomwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya Mjini, Girbet Ndeuluo, na Mwendesha Mashtaka, Achiles Murisa ambaye alidai kosa hilo lilitokea January 12, 2012.
Achiles aliwataja watuhumiwa kuwa ni Walder Veemad, Segeer Backer na Andress Dafee ambapo wote ni wafanyakazi wa kampuni ya Kapunga.
Alisema, watuhumiwa wamefanya kosa hilo wakati wakipiga dawa katika mashamba yao kwa kutumia chombo cha usafiri wa angani (ndege).
Alisema, dawa hiyo inasemekana ilipitiliza hadi kwenye mashamba jirani na kufanya uharibifu kwenye mazao yaliyokuwa shambani.
Wakati hilo likiendelea mahakamani, mwekezaji huyo juzi aliingia katika tatizo jinguine baada ya gari lake aina ya Scania Na T 398 BSE kupinduka na kusababisha vifo vya watu sita na kujeruhi wengine 129.
Katika gari hilo inasemekana lilibeba watu zaidi ya 200 ambao walikuwa wanaenda kufanya vibarua katika shamba la mwekezaji huyo.