*Kituo kuhamishwa, polisi wanaoishi hapo kuondolewa
*Kunajengwa maduka, hoteli, hospitali, kumbi za starehe
*Wizara ya Mambo ya Ndani: Ardhi inaendelea kuwa yetu
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeingia mkataba na kampuni ya Mara Capital, kampuni tanzu ya Mara Group, unaoipa mamlaka kampuni hiyo kuchukua eneo lote la Polisi Oysterbay, Dar es Salaam, kwa ajili ya ujenzi wa duka kubwa la kisasa (shopping mall), hoteli mbili na huduma nyingine za kibiashara.
Kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa Mara Group, ukubwa wa eneo hilo ni futi za mraba milioni 3.5. Thamani ya vitegauchumi vitakavyojengwa hapo ni dola milioni 300. Kwa sasa dola moja ni wastani wa Sh 1,590.
Mradi huo unaelezwa kwamba utakuwa wa duka kubwa na la kipekee katika ukanda wa Afrika Mashariki, hoteli mbili za hadi ya nyota tano, kituo cha mikutano, hospitali ya kisasa, makazi na kituo cha kisasa cha polisi.
Polisi wanaoishi eneo hilo wanatakiwa wawe wameondoka ifikapo Mei mwakani. Mwekezaji huyo amepanga kujenga nyumba 300 kwa ajili ya polisi hao. Habari za awali zinasema nyumba hizo zitajengwa nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Mkataba huo ulitiwa saini kwenye Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam na kuwahusisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Mbarak Abdulwakil, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Saidi Mwema, na wakurugenzi wawili wa Mara Group, Ashish Thakkar na Prashant Manek.
Eneo linalohusishwa kwenye mradi huu linaanzia Namanga Shopping Centre hadi Morocco. Mwekezaji huyo ametoa fedha kwa ajili ya kuwalipa polisi watakaohamishwa hapo.
Kuna habari kwamba askari wa vyeo vya juu watajengewa nyumba za kuishi eneo la Mikocheni na askari wa vyeo vya chini watajengewa Kunduchi Mtongani.
Aidha, kuna habari kwamba kila polisi wa cheo cha chini anayeishi hapo Oysterbay amepangiwa malipo ya Sh milioni tatu, ilhali wale wa vyeo vya juu, kila mmoja atalipwa Sh milioni saba. Fedha hizo ni kwa ajili ya kusafirisha mizigo pamoja na usumbufu.
Kwa sasa Kituo cha Oysterbay ndicho Kituo Kikuu cha Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni. Kwa mabadiliko hayo, inapendekezwa kuwa Kituo cha Mkoa huo kitahamishiwa Kijitonyama Mabatini!
Mara Group inajinasibu kuwa inajishughulisha na masuala mbalimbali yakiwamo ya ujenzi wa vitegauchumi, teknolojia ya mawasiliano, miundombinu, habari na mawasiliano, na kadhalika. Ipo katika mataifa 18 barani Afrika ikiwa imeajiri watu zaidi ya 4,000.
Akizungumza wakati wa utiaji saini makubaliano hayo, Manek alisema mradi huo mkubwa utaifanya Dar es Salaam kuwa ya kisasa na kuitangaza Tanzania duniani kote.
“Mradi utaanza miezi 11 kuanzia leo (siku ya utiaji saini), na ardhi itabaki kuwa mali ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi la Tanzania ,” alisema Mkuu wa Ununuzi katika Jeshi la Polisi aliyetajwa kwa jina la Gregory.
Hii si mara ya kwanza kwa Serikali kuchukua uamuzi wa kuhamisha shughuli za kijeshi kwa ajili ya kuwapisha wawekezaji.
Ilikwishafanya hivyo kwa kuhamisha Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Buhemba, Butiama mkoani Mara ili kuwapisha wachimba dhahabu wa Meremeta kutoka Afrika Kusini.
Pia, kuna habari kwamba Kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kyabakari, iliyopo Butiama mkoani humo, huenda nayo ikaondolewa ili kuwapisha wawekezaji baada ya kubainika kuwapo dhahabu nyingi.
Eneo hilo lilikuwa likichimbwa dhahabu wakati wa ukoloni, lakini shughuli hizo zilisimamishwa baada ya Uhuru ambako Serikali iliweka kambi hiyo ya Jeshi.
Kutoka mkoani Mbeya, zipo taarifa kuwa Gereza Kuu la Mkoa wa Mbeya, Isanga, nalo lipo mbioni kuhamishwa baada ya kugundulika lipo juu ya madini yenye thamani kubwa.
Vyanzo vya habari kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa, vinasema mipango yote imekwishakamilishwa, hivyo kinachosubiriwa ni mkataba na harakati za gereza hilo kuvunjwa na uchimbaji kuanza mara moja.
Hata hivyo, askari aliyezungumza na JAMHURI kwa sharti la kutotajwa jina, alisikitishwa na hatua ya Serikali kuingia tamaa ya kupata fedha na kusahau kwa nini kituo kama Oysterbay kilianzishwa na kuwekwa hapo kilipo.
“Jamani tumeanza kuchezea usalama wa nchi hii. Hivi leo wanataka kusema Oysterbay Police imepoteza umuhimu wa kuendelea kuwapo hapo ilipo? Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, zamani Barabara ya Bagamoyo, katika nchi zote duniani barabara kama hii inayotoka katikati ya jiji lazima iwe na kituo kikubwa cha polisi kando kando ya barabara.
Ndiyo maana utaona kuna kituo hiki, kuna kituo cha Urafiki karibu na Shekilango, kuna Kituo cha Buguruni, Mabatini kule Banana, Kuna kituo cha Ufundi na Temeke, angalia maana yake nini.
“Maana yake ni kwamba ukitokea uhalifu katikati ya Jiji, basi polisi wanatanda na kuziba barabara kuu za kutokea. Sasa huko Mabatini wanakotaka kukihamishia, hivi ujambazi ukitokea katikati ya Jiji hadi polisi watoke vichochoroni kukusanywa kuja kuziba barabara ni lini?
“Kwa ufupi, hapa tunajenga mtandao wa majambazi kufanikisha shughuli zao kiulaini tu. Eti polisi watajengewa nyumba Goba, mpaka utoke Goba kuja mjini, majambazi watakuwa wamefika Morogoro. Acha tuchezee usalama tu, ila ipo siku tutajuta,” alisema askari huyo.
Askari mwingine alisema tatizo linalolalamikiwa la foleni halitakaa liishe kwani kinachoonekana sasa ni miradi kuendeleza kujazwa katikati ya Jiji. Hivi wanashindwa kujenga mradi kama huo Mbezi Beach, Mbagala, Kibaha na kwingineko nje ya jiji wakazalisha ajira na kupunguza msongamano katikati ya Jiji?” alihoji askari huyo.
Askari mwingine alisema kinachoendelea sasa ni udhalilishaji. “Fedha imeonekana ina nguvu kuliko Serikali. Kwa mwekeleo huu, hatari kubwa inalinyemelea taifa hili… tunauza kituo cha polisi kwa mtu binafsi?” Alihoji.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, hakupatikana kuzungumzia kadhia hii kutokana na harakati za uchaguzi zinazoendelea mjini Dodoma, kwani wakati wote hakuwapo ofisini kwake na simu yake ilikuwa haipokewi.