Moja ya matatizo yanayowakabili wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ni ukosefu wa maji. Jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa na Serikali, lakini bado tatizo hili limeonekana kuwa kubwa.
Mtaa wa Kwembe uko katika Wilaya ya Kinondoni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Wakazi wa eneo hili ni miongoni mwa wananchi wa jiji hilo ambao kwa namna moja ama nyingine wameonja adha ya ukosefu wa maji.
Mtaa huu huko katika Kata ya Kwembe yenye takriban wakazi 30,000. Kwembe ni kati ya maeneo yanayokua kila siku kutokana na ongezeko la makazi mapya ya watu.
Ili kutatua tatizo la maji, katika miaka 1980 wananchi wa Kwembe waliamua kuanzisha mradi wa maji uliofahamika kwa jina la Jumuiya ya Watumia Maji Kwembe. Mradi huo ilikuwa chini ya ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Japan (JICA) wenye thamani ya Sh milioni 94.
Chini ya ufadhili huo, wananchi wa Kwembe waliweza kujenga kisima chenye ujazo wa lita 20,000 kilichokuwa kinapokea maji kutoka bomba kuu la Dawasco katika eneo la Kibamba kwa Mangi.
Hali kadhalika, wananchi waliweza pia kujenga kisima kingine eneo la Kwembe chenye ujazo wa lita 45,000. Jitihada za wananchi ziliishia hapo na hivyo mradi haukuweza kufanikiwa kama yalivyokuwa matarajio ya wengi.
Kazi kubwa ya kisima cha Kibamba kwa Mangi ilikuwa ni kupokea maji na kilitakiwa kuyasambaza katika maeneo mbalimbali ya Kwembe kupitia kisima cha lita 45,000 kilichokuwa kimejengwa eneo la Kwembe. Hilo halikufanikiwa ipasavyo kutokana na miundombinu kuwa hafifu.
Baada ya kuona tatizo la maji linazidi kuwa sugu, mwaka 2010 wananchi wa Kwembe walikutana na kutengua uongozi wa zamani uliokuwa unasimamia mradi huo na kupata uongozi mpya.
“Baada ya kupatikana kwa uongozi mpya tukajaribu kutumia miundombinu tuliyoikuta, lakini ikaonekana kuwa tayari ilikuwa mibovu na kwa hiyo isingeweza kusaidia lolote katika suala zima la kurahisisha upatikanaji wa maji,” anasema Joyce Manyerere, Mratibu wa mradi huo kwa sasa.
Chini ya uratibu wa Joyce, mradi huo ukafanikiwa kupata wafadhili kutoka mashirika mbalimbali ya kimataifa kama vile EU na BTC, ambayo yalishirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Ufadhili huo ulituwezesha kupata mabomba 79 ya inchi sita. Baada ya uboreshaji wa miundombinu ikaonekana kuwa kuna umuhimu wa kuwa na transfoma ambayo itaweza kusukuma maji ili kuendana na miundombinu mipya. Hili lilikuwa gumu kidogo tukarudi kwa wafadhili kuwaeleza, wakakubali na wakatoa ahadi ya kutupatia transfoma,” anaeleza Joyce.
Wakati wakisubiri kupata transfoma kutoka kwa wafadhili, uongozi wa mradi huo ukabuni mbinu mbadala ambayo ingesaidia kuwapatia maji kwa wakati ule wananchi wa Kwembe.
Kupitia mbinu mbadala kamati iliamua kuwa maji yasambazwe kwa gari kutoka Kibamba kwa Mangi hadi kwa wananchi wa Kwembe, ambapo kila mwananchi alinunua ndoo ya lita 20 kwa bei ya Sh 250 na dumu la lita 1,000 liliuzwa Sh 9,000.
“Kwa utaratibu, huu tulipata magari kama 20 ambayo tuliyasajili kwa makubaliano ili kusambaza maji, hali kadhalika kwa kuzingatia bei elekezi iliyopangwa na uongozi ambayo ndiyo hiyo niliyokutajia hapo awali,” anasema Joyce.
Magari yanayosambaza maji
Inaelezwa kuwa wenye magari wakishasambaza maji kwa wakazi wa Kwembe na kuyauza kwa bei elekezi, wanapewa fursa ya kuuza nje ya Kata ya Kwembe kwa bei watakayojipangia wao.
“Huu ni utaratibu ambao tuliuweka kuhakikisha kuwa wananchi wetu wanapata maji kwanza kwa bei nafuu, na baada ya hapo mwenye gari akitaka kuuza maji nje ya Kata ya Kwembe anaruhusiwa pia, na hapo sasa sisi hatumpangii bei,” anasema Joyce.
Machi 2013 mahitaji ya maji yaliongezeka katika Mtaa wa Kwembe. Hivyo basi uongozi wa mradi huo ukaona umuhimu wa kujenga kisima kingine cha kupokelea maji.
Wananchi wa Kwembe walikaa mkutano wa pamoja na kuamua kuanzisha mfuko wa ujenzi. Chini ya mfuko huo ndoo yenye ujazo wa lita 20 iliuzwa kwa Sh 300 badala ya Sh 250 ya mwanzoni, Sh 50 ikiwa mchango wa ujenzi.
Vilevile dumu la ujazo wa lita 1,000 lililokuwa likiuzwa Sh 9,000 likawa linauzwa Sh 10,000, Elfu moja ikiwa mchango wa ujenzi.
“Chini ya utaratibu huu, mpaka kufikia mwezi Julai mwaka huu, tuliweza kujenga kisima chenye ujazo wa lita 160,000 kwa gharama ya shilingi milioni 40. Na kabla ya wafadhili kutekeleza azma yao ya kutupatia transfoma, Serikali yetu tayari imetupatia transfoma na hivi tunavyoongea uunganishaji umekamilika na maji yatawafikia wananchi wa Kwembe muda wowote kuanzia sasa,” anasema Joyce.
Utaratibu wa sasa
Baada ya maji kupokewa katika kisima kipya chenye ujazo wa lita 160,000 kikisaidiwa na kile cha zamani cha ujazo wa lita 20,000, yatasukumwa na transfoma katika visima viwili ambavyo viko katika maeneo tofauti ya Mtaa wa Kwembe.
Katika visima hivyo, kimoja kina uwezo wa kupokea ujazo wa lita 45,000. Visima hivyo vitasambaza katika vizimba vingine vitano ambavyo viko katika sehemu mbalimbali za Kwembe. Kutoka katika vizimba hivi, maji yatasambazwa katika vituo mbalimbali vya wananchi wenye matangi yao binafsi ambao wako 30, hawa nao wanawauzia wananchi.
“Sasa unaweza kuona kwa mtiririko huu kuwa maji yataweza kuwafikia wananchi wa Kwembe kwa urahisi zaidi kuliko ilivyokuwa mwanzo, lakini pia magari yataendelea kusambaza katika maeneo mbalimbali ya Kata ya Kwembe,” anasema Joyce.
Changamoto
Changamoto kubwa ni uhitaji wa maji ya kutosha kutokana na ongezeko la watu katika eneo la Kwembe. “Unajua, baada ya sisi kuwa na mradi huu, Dawasco walifunga visima vyote vya watu binafsi, kwa hiyo mahitaji yote ya maji yamehamia kwetu,” anasema Barnabas Asenga, Msimamizi Mkuu wa Huduma katika Kituo hicho.
Mafanikio ya mradi
Kwa mujibu wa Joyce, mradi huu pia umefanikiwa kufanya ukarabati wa baadhi ya barabara katika Mtaa wa Kwembe, hali ambayo imerahisisha usafirishaji wa maji katika maeneo mbalimbali.
“Hayo ni mafanikio, lakini pia tumefanikiwa kulipa bili zetu kwa wakati kule Dawasco, hatudaiwi na mtu yeyote, wale watumishi wetu wako vizuri na hata tukianza kulipa bili za Tanesco nazo nina imani kuwa tutafanya vizuri kwa sababu tumejipanga vizuri katika hili,” anasema mratibu huyo.
Matarajio ya baadaye ya mradi huo ni kuhakikisha kuwa kila mkazi wa Kwembe anapata huduma nzuri ya maji kutokana na mradi huu.