Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mwanza

Ni zama za sayansi na teknoojia. Ndio, teknolojia inapaswa kutumika katika kila eneo ilimradi tu kuleta ufanisi na kuboresha amaisha.

Ni ukweli huu ndio umeifanya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwa mara ya kwanza nchini, kuanzisha rasmi mapambano dhidi ya uvuvi haramu kwa mbinu za kisasa.

Sasa ‘ndege nyuki’, kwa Kiingereza ‘drone’ itaanza kutumika kuwasaka wavuvi haramu popote walipo ndani ya Ziwa Viktoria katika harakati za kukomesha vitendo hivi hatari kwa mustakabali wa taifa.

Naibu Waziri (Uvuvi), Alexander Mnyeti, anasema hiyo ni moja kati ya hatua madhubuti na za kisasa zinazochukuliwa na serikali kudhibiti uvuvi haramu.

“Wizara imetumia Sh milioni 259 kwa ununuzi wa ndege nyuki, mafunzo kwa waendeshaji, vituo vya udhibiti, usajili na kuanzisha mfumo wa kuhifadhi na kuchambua taarifa zinazopatikana kutoka kwenye (picha) ‘drone’.

“Ndege hii itaimarisha usimamizi wa shughuli za uvuvi Ziwa Victoria. Ina spidi ya kilometa 108 kwa saa na uwezo wa kuchukua picha kutoka umbali mita 350,” anasema Mnyeti kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Ashatu Kijaji.


Ndege hiyo mali ya serikali, ina uwezo wa kwenda umbali wa Kilometa 400 (kutoka kituo iliporushwa) na kukaa angani kwa muda wa saa mbili.

Kana kwamba haitoshi, Mnyeti anasema matumizi ya ndege nyuki hayataishia Ziwa Victoria pekee, bali yatasambaa hadi Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na pwani ya Bahari ya Hindi.


“Kila pembe ya nchi itaonja matunda ya teknolojia hii ya kisasa katika usimamizi wa rasilimali za taifa,” anawahakikishia maofisa wa Idara ya Uvuvi na wananchi waliohudhuria hafla ya uzinduzi jijini Mwanza mwishoni mwa wiki.

Iwavyo vyovyote vile, kuanza kwa matumzi ya ndege nyuki katika mapambano dhidi ya uvuvi haramu kutapunguza vitendo vitendo hivyo sambamba na gharama za doria.

Lakini pia itatumika katika uokoaji pindi majanga yanapotolea majini.

“Wizara itaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi nyingine kuimarisha ulinzi na usalama Ziwa Victoria,” anasema.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dk. Edwin Mhede, anasema matumzi ya ndege nyuki ni utekelezaji wa matakwa ya kimataifa yanaoelekeza matumizi ya teknolojia rafiki kwa kimazingira.

Awali, katika mapambano dhidi ya uvuvi haramu, serikali ilikuwa ikitumia boti na magari; nyenzo ambazo hutumia dizeli, miongoni mwa nishati zinazozalisha hewa ukaa.

“Ndege nyuki hii itakuwa ikienda eneo mahsusi lenye viashiria vya uvuvi haramu hivyo kupunguza matumizi ya boti na magari kuwasaka wavuvi haramu,” anasema Dk. Mhede.

Amemuahidi Naibu Waziri, Mnyeti, kwamba Idara anayoisimamia itatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na serikali.

Miongoni mwa maelekezo hay oni kufuatilia tuhuma zinazotolewa na wananchi zikiwatuhumu baadhi ya maofisa uvuvi kushiriki katika vitendo vya uvuvi haramu.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.
Jitihada za serikali za kubadili mbinu ya kupambana na uvuvi haramu zimwafurahisha wakazi kadhaa wa Jiji la Mwanza, wakisema hatua ya kujivunia kwa Watanzania wote.

Serikali imeahidi kutenga fedha za kutosja katika Bajeti ya 2025/26 kwa ajili ya ununuzi wa ndege nyuki zaidi ili kuongeza wigo wa kudhibiti uvuvi haramu nchini.