Mashabiki wa soka wa Tanzania ni wasahaulifu sana. Ukiwasikiliza mashabiki wa Yanga leo, unaweza usiamini kile wanachokidai.
Msimu uliopita tu mashabiki hao walikuwa wakimhusudu Kocha wao, Mwinyi Zahera, ambaye licha ya kufundisha kikosi cha mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu nchini katika hali mbaya, alifanikiwa kuiwezesha timu hiyo kumaliza kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu.
Wakati huo mashabiki wa Yanga usingewaambia chochote dhidi ya Zahera wakakubali kukusikiliza.
Lakini wiki iliyopita wakiwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, mashabiki hao hao walikuwa wakiimba kwa nguvu wakimkataa Zahera na kutaka aondolewe haraka! Kisa, timu yao kufungwa 2-1 na Pyramids ya Misri katika mchezo wa kwanza wa kuwania nafasi ya kucheza kwenye makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ukisikia jinsi wanachama hao walivyokuwa wanaimba kumkataa Zahera na ukiwaangalia jinsi walivyokuwa wakirusha chupa za maji kwa hasira, ni vigumu kuamini kuwa ni Zahera huyo huyo ambaye mwaka jana walimtetea kwa nguvu zao zote.
Na kauli alizozitoa Zahera baada ya mechi hiyo ndizo zimezidi kuchochea moto wa mashabiki wa Yanga. Zahera alitaka wachezaji na yeye wasilaumiwe kutokana na kufungwa na Wamisri hao kwa sababu timu hiyo haikufanya usajili kwa ajili ya kushiriki michuano ya kimataifa mwaka huu.
Hilo linaweza kuwa na ukweli kwa kiasi fulani kwa sababu baada ya kumaliza washindi wa pili katika ligi na kushindwa kuchukua Kombe la Shirikisho, Yanga haikuwa na nafasi ya kushiriki mashindano ya CAF mwaka huu.
Lakini mambo yalibadilika baada ya Tanzania kupata nafasi ya kuingiza timu nne kwenye mashindano ya CAF – mbili kwenye kinyang’anyiro cha Klabu Bingwa Afrika na mbili kwenye Kombe la Shirikisho.
Ghafla, Yanga ikajikuta ikidondokewa na bahati ya mtende kwa kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kushika nafasi ya pili kwenye ligi.
Wakati Yanga ikipata nafasi hiyo, usajili ulikuwa umeshafanyika kwa kiasi kikubwa. Mbaya zaidi, hata ratiba ya michuano hiyo ilibadilishwa na kuifanya Yanga na timu nyingine zilizoshiriki zishindwe kufanya maandalizi ya kutosha.
Hata hivyo, mashabiki wanahoji kama Zahera aliiandaa timu kwa ligi ya ndani kwanini bado haijaonyesha ushindani mkubwa katika ligi hiyo?
Katika mechi nne ambazo Yanga imecheza katika Ligi Kuu hadi hivi sasa imefungwa mechi moja, kutoka sare mechi moja na kushinda mechi mbili, hivyo kujikusanyia jumla ya pointi saba ikiwa pointi 11 nyuma ya vinara wa ligi hiyo na mahasimu wao wakubwa, Simba.
Mashabiki wa Yanga wanahemuka pia kutokana na rekodi ya mahasimu wao hao ambao katika mechi saba, wameshinda mechi sita na kufungwa mechi moja.
Kuondoka kwa Zahera Yanga hivi sasa ni jambo linalotarajiwa na watu wengi, hasa ukizingatia kuwa klabu nyingi nchini hazina utaratibu wa kuwavumilia makocha timu zao zinapofanya vibaya hata kama sababu si makocha hao.
Wakati makocha wanahitaji si chini ya misimu minne kuijenga timu, huu ni msimu wa pili tu kwa Zahera kuwa Yanga lakini tayari mashabiki wa timu hiyo wameonyesha kumchoka.
Ukiacha Yanga, timu nyingine za Ligi Kuu ambazo zimeonyesha dalili ya kuwachoka makocha wao ni Ndanda, ambayo siku kadhaa zilizopita ilimpa kocha wao mechi tatu kumpima kama anastahili kubakia katika timu hiyo.
Azam yenyewe tayari imekwisha kubadilisha kocha. Ingawa sababu kubwa inatajwa kuwa Kocha huyo, Etiene Ndayiragije, kupata kibarua cha kuifundisha Taifa Stars, lakini baadhi ya wachambuzi wanabainisha kuwa tayari timu hiyo ilikwisha kumchoka kocha huyo kutokana na matokeo mabaya katika michezo ya kimataifa.