Rais wetu sasa ni Dk. John Magufuli. Tuna wajibu wa kumsaidia ili aweze kutimiza ahadi zake nzuri alizowaahidi Watanzania wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.

Kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu”, hatuna budi kuitekeleza kwa vitendo. Hatuna muda wa kupoteza. Uzoefu umeonyesha kuwa miaka mitano ni muda mfupi mno endapo wapiga na wapigiwa kura tutaamua kuutumia kwa malumbano.

Endapo tutaamua kuanza kazi mara moja, miaka mitano ni muda mrefu. Unatosha kuifanya Tanzania walau ionakane tofauti kimaendeleo.

Miongoni mwa ahadi kubwa za Rais Magufuli, ni ajira kwa mamilioni ya vijana. Amebainisha maeneo mawili makubwa ya kuwasaidia vijana kujikwamua-Kilimo na Viwanda. Viongozi wenye maono kama yeye, ndiyo wanaozungumzia maeneo ya aina hii, na si kwenye bodaboda. Siamini kama bodaboda zinaweza kuboresha maisha ya vijana wa Taifa letu.

Akiwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, miongoni mwa mambo ninayodhani alikosea ni lile la kutengua msimamo wa mtangulizi wake, Mama Zakia Meghji, kwa kufuta ushuru kwenye mafuta ya kula yanayotoka ughaibuni.

Mama Meghji, kwa kutambua azma ya kuimarisha, kuboresha kilimo na kuibua ajira kwa vijana nchini, alisimama kidete kuhakikisha kuwa mafuta ya kula kutoka nje yanalipiwa ushuru wa asilimia 10.

Mafuta ya mawese kutoka nje yanaingizwa nchini kwa kivuli cha “mafuta ghafi,” lakini ukweli si ghafi! Ni mafuta yaliyosindikwa na kufikia kiwango cha kutumiwa!

 Mkulo alifuta ushuru ukawa sifuri kutoka asilimia 10 kwa kisingizio kwamba kwa kufanya hivyo wafanyabiashara na viwanda vyetu vingeweza kushindana na nchi wanachama katika Jumuiya ya Afrika Mashariki! Uamuzi huo wa Mkulo ukawa kifo kwa wakulima wetu wa alizeti, mawese, karanga, pamba na mazao mengine yanayozalisha mafuta ya kula hapa nchini.

Suala hili la “mafuta ghafi” nimelifuatilia kwa miaka mingi. Hakuna mafuta ghafi. Genge la wafanyabiashara wameweka nguvu na kuhakikisha wanaighilibu Serikali ili ikubaliane na matakwa yao.

Kwa kuwa viongozi wetu kadhaa walikuwa si watu wenye kuzingatia maslahi ya wananchi, wakakubali; ama kwa umbumbumbu, au kwa malipo maalumu, kufuta ushuru kwenye mafuta hayo kutoka Asia.

Ndani ya hicho kinachoitwa mafuta ghafi, yakishafikishwa Dar es Salaam, viwanda vinaondoa mafuta na kuyaongeza thamani kwa kuyaweka kwenye vyombo na kuyapamba kwa majina mazuri.

Kinachobaki kutoka kwenye mafuta hayo, ni malighafi kwa ajili ya kutengeneza vifaa vya plastiki kama vile ndoo, viti, meza, vyombo vya ndani na kadhalika.

Malighafi nyingine inayobaki inatumika kutengeneza sabuni na kuziuza kwenye soko la ndani.

Kwa ufupi ni kwamba kile kinachoonekana kuwa ni “mafuta ghafi”, si mafuta ghafi, isipokuwa ni mafuta ya kula na malighafi nyingine za kutengeneza vitu hivyo nilivyovitaja na vingine vingi.

Kwa hiyo kufuta ushuru kwenye mafuta ghafi hayo, maana yake ni kuwaambia wenye kuyaingiza nchini waendelee kuneemeka kwa kuondolewa ushuru/kodi; na wakati huo huo wazidi kuwabana wenye viwanda vya mafuta yanayotokana na malighafi za ndani ili wafe. Watengeneza sabuni wanapohitaji malighafi, huwafuata hao hao waagizaji wakubwa na kuuziwa malighafi kwa bei kubwa kwa makusudi. Matokeo yake wenye viwanda vya sabuni vya ndani, hasa vile vidogo na vya kati vimejikuta vikifungwa kutokana na kushindwa kumudu ushindani na bei za soko.

Hapa fomula yake ni nyepesi tu. Mwenye kiwanda kidogo au cha kati anapotaka malighafi kutengeneza sababu, huyu mwenye malighafi anachofanya ni kumkomoa kwa kumpangia bei ya juu. Matokeo yake, huyu mdogo anashindwa na kumwacha yule mkubwa aendelee kutengeneza sabuni kwenye kiwanda chake na kulikamata soko.

Wakulima na wafanyabiashara wetu wa ndani hawawezi kushindana na mafuta ya mawese yanayotolewa nje ambayo wakulima wake wanapewa ruzuku na Serikali zao. Sisi wakulima wetu hapa hawapewi ruzuku na kwa maana hiyo bei lazima ziwe juu.

Ndiyo maana mafuta ya nje yanaweza kuuzwa Sh 5,000 licha ya kuwa ni hatari (yana rehemu), na yale ya alizeti yanayozaliswa na wakulima wetu masikini yakiuzwa hadi Sh 15,000 kwa ujazo ule ule. Ukiweka na mlolongo wa kodi kuanzia kijiji, halmashauri hadi Serikali Kuu, wangapi watamudu kununua mafuta yanayosindikwa hapa nchini?

Maradhi ya shinikizo la damu (BP), kisukari na saratani yanaongezeka kwa kasi ya kustaajabisha. Ugonjwa wa shinikizo la damu ambao ulijulikana kuwa ni wa watu wazima na “matajiri”, unawapata hadi watoto wenye miaka 10. Ebu wataalamu wasaidie kubaini sababu za ongezeko la maradhi haya ni nini. Sitaki kupiga ramli, lakini kuna shaka kuwa huenda mafuta haya yenye rehemu nyingi yakawa yanachangia maradhi haya. Haya yanazungumzwa. Wataalamu wetu wathubutu kupata ukweli wake.

Wakati Mkulo akihalalisha kuondolewa kwa ushuru huo kwa kigezo kuwa kiwango cha mafuta kinachozaliwa nchini ni kidogo, alisema anaondoa ushuru kwa mafuta ya nje ili kuepusha uhaba wa bidhaa hiyo nchini.

Mimi si mchumi, lakini akiri ya kawaida ya kijasiriamali inanituma kuamini kuwa unapokuwa na upungufu wa bidhaa kama hiyo, huo ndiyo mwanzo wa kuhimiza kilimo.

Huo ndiyo mwanzo wa kuwafanya vijana wengi washiriki kilimo cha alizeti na mazao mengine ya mafuta kwa sababu kinakuwa tayari kina tija. Huo ndiyo mwanzo wa kuwaondoa kwenye adha hii ya kuendesha bodaboda ambayo tunajiadanganya kwa kuamini kuwa itawapa maisha mazuri.

 Ni Mkulo huyu huyu ambaye, ama kwa kutojua, au kwa makusudi, aliamua kushirikiana na wafanyabishara kuingiza nchini vileo kwa ushuru mdogo, huku wazalishaji wa ndani akiwakamua kodi. Mvinyo unaozalishwa nchini ukatozwa Sh 420 kwa chupa, ilhali unaotoka nje unalipiwa Sh 122 kwa chupa!

Kwa ushuru huo, ndugu zetu wanaolima zabibu katika mikoa kama Dodoma na Singida, hawawezi kupambana na waagizaji kutoka ng’ambo. Mvinyo unaotengezwa Tanzania ni mtamu, lakini tunashindwa kuupata kutokana na kodi kubwa. Sasa tunajikuta tukilazimika kunywa mvinyo kutoka Afrika Kusini ambao kwa kweli ubora wake si wa kuuzidi wa kwetu.

Rais Magufuli, ameahidi viwanda. Hili ni jambo jema sana. Viwanda na kilimo ni kama samaki na maji. Hatuwezi kuzungumza viwanda kama kilimo kitaendelea kuminywa au kuvizwa kwa mbinu zilizotumiwa na kina Mkulo.

Unaposafiri kwa gari- kuanzia Dodoma hadi Igunga, barabarani kuna mamia ya wananchi, hasa vijana wanaouza mafuta ya alizeti. Wapo wenye viwanda vidogo kwa ajili ya kusindika, lakini wapo wengine wanaosindika kwa kutumia maarifa ya kienyeji yasiyokuwa na tija.

Endapo Serikali itafanikiwa kuweka ushuru kwenye “mafuta ghafi” ya mawese na mengine kutoka nje, hiyo ina maana soko la mafuta yetu ya ndani litakuwa zuri. Lakini si uzuri tu, isipokuwa mahitaji ya mafuta yatakuwa makubwa na kwa sababu hiyo vijana wengi watajielekeza kwenye kilimo.

Wengi wakishageukia kilimo, ni lazima mahitaji ya viwanda vingi-vidogo, vya kati na vikubwa, yatapanuka. Kuwapo kwa viwanda vingi kutasaidia kuongeza ajira na hivyo kutimiza azma ya Rais Magufuli.

Kilimo cha alizeti, ufuta na mazao mengine ya aina hiyo kisilenge kulitazama soko la ndani pekee. Tutazame soko la nje. Mataifa mengi dunia yanapenda kutumia mafuta ya alizeti ambayo hayana madhara yanayosababishwa na rehemu nyingi kama ilivyo kwa mawese.

Soko la mafuta haya kwa mataifa mengi ya Afrika, Ulaya na Asia ni kubwa. Tanzania tunayo ardhi ya kutosha, nzuri na hali ya hewa inayofaa kwa kilimo cha aina hii.

Watanzania tunachopaswa kufanya ni kupanua kilimo chetu, lakini hatuwezi kufanya hivyo kama tutaendelea na fikra za wafanyabiashara wachache kuwatumia viongozi wetu kuondoa ushuru/kodi kwenye mazao na bidhaa nyingine zinazozalishwa ughaibuni.

Mafuta ya mawese kuingizwa nchini bila kulipiwa ushuru ni pigo kubwa mno kwa wakulima wa Tanzania, na kwa kweli hili ni eneo mojawapo ambalo Serikali ya Awamu ya Tano inapaswa kuanza nalo bila kuchelewa. Bajeti ya mwaka 2016/2017 tuhakikishe ushuru unarejeshwa kwenye mafuta ya mawese na mengine kama njia ya Serikali kuingiza mapato na pia kuwalinda wakulima wetu wa ndani.

Tufanye hivyo hadi kwenye maziwa ili tuwe na wafugaji wengi, viwanda vingi vya kusindika mazao ya maziwa na kwa maana hiyo vijana wengi zaidi wapate ajira. Ebu tuangalie mfano kama ule wa Asas pale Iringa, ameajiri watu wangapi kuanzia mashambani, kiwandani na katika maduka?

Jambo jingine ambalo Rais Magufuli, anapaswa kulifanya ni kukutana na wamiliki wa viwanda kwa kila mkoa. Tunatambua kuwa ameshaunda Kamati ya Wataalamu ili kubaini sababu za kufa kwa viwanda na kumshauri hatua za kunusuru hali hiyo.

Uamuzi huu ni mzuri, lakini ingekuwa vizuri zaidi kama Rais angehakikisha suala hili analifanya mkoa kwa mkoa kwani matatizo ya viwanda vya Tanga yanaweza yakawa tofauti na viwanda vya Tabora au Kigoma. Pia ni vizuri akawasikiliza wenye viwanda wenyewe moja kwa moja ili kusikia maoni yao kutoka kwao.

Viwanda vingine vimekufa kwa sababu kama hii ya kuingiza maelfu ya tani za mawese bila ushuru. Hili jambo nimeliandika kwa miaka 10. Nina hakika ushauri huu ukizingatiwa na Serikali kilimo na viwanda vitastawi katika Taifa letu. Yanayowezekana sasa Serikali yetu haina budi kuanza nayo mara moja. Hatuna muda wa kupoteza. Imani waliyonayo wananchi kwa Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwa itakuwa makini kusikiliza, kupokea na kufanyia kazi ushauri mbalimbali unaolenga kulijenga Taifa letu.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alituasa kwa kusema: “Inawezekana Kufanyika, Wafanya Wajibu Wako.”