Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro

Rai imetolewa kwa Watumishi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na weledi wa hali ya juu wanapotekeleza majukumu yao.

Rai hiyo imetolewa na Kamshina wa Maadili Jaji (Mst.) Sivangilwa Mwangesi wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi cha Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Cate mjini Morogoro.

‘’Hauwezi kuwa mwangalizi wa maadili ya wengine wakati wewe mwenyewe hauna maadili, hivyo kama mfanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma unatakiwa kuwa mfano wa kuigwa na watumishi wengine wa Umma katika nyanja ya uadilifu,’’alisema Mwangesi.

Jaji Mwangesi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo la Wafanyakazi wa ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ameongeza kuwa uadilifu unajengwa kwa nguzo kuu tatu.

Alizitaja nguzo hizo kuwa ni utaalamu, uaminifu na uwajibikaji na kuongeza kuwa ni wajibu kwa kila mtumishi wa Sekretarieti kuzingatia nguzo hizo.

‘’Ninawaasa kuzingatia nidhamu na kujituma katika kutekeleza majukumu yenu na yeyote atakayeenda kinyume na hayo, atakua si miongoni mwetu na hatutasita kumchukulia hatua kutokana na mwenendo wake,’’alisema.

Katika hatua nyingine, Kamishna huyo wa Maadili, amezungumzia umuhimu wa watumishi kutunza na kulinda rasilimali za Taasisi na kuacha uzembe katika matumizi ya mali na vitendea kazi vya ofisi kutokana na upatikanaji wake kuwa wa gharama.

‘’Niwaombe kuacha uzembe na kuwa makini katika matumizi ya vitendea kazi na kuvitunza kwa hali na mali kwani vitendea kazi tulivyonavyo ni vichache na upatikanaji wake ni washida sana,’’amesisitiza.

Kuhusu kuufanyaji kazi kwa ushirikaiano, Mwenyekiti huyo wa Baraza la Wafanya kazi, aliwapongeza watumishi wa Sekretarieti ya Maadili kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kuomba hali hiyo iwe endelevu na amesisitiza kuwa kwake milango ipo wazi kwa yeyote mwenye jambo kumuona na kujadili kwa pamoja.

‘’Niwapongeza kwa ushirikiano wenu katika utendaji kazi na ninawaomba ushirikiano huo mnaonionyesha mimi pia uwe endelevu miongoni mwenu ili tuweze kuifikisha mbali Taasisi yetu,’’ alisisitiza.

Please follow and like us:
Pin Share