Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Malawi ameshtakiwa kwa kupanga njama ya kumuua Rais wa nchi hiyo, Lazarus Chakwera.
Patricia Kaliati, Katibu Mkuu wa chama cha UTM, alikamatwa wiki iliyopita kwa tuhuma za “kula njama na wengine kutenda kosa kubwa”.
Alipofikishwa Jumatatu katika mahakama katika mji mkuu wa Malawi, Lilongwe, ,mwanamama huyo mwenye umri wa miaka 57 hakuzungumza.
Lakini wakili wake alidai kuwa mwanasiasa huyo alisisitiza kuwa hana hatia, ripoti ya vyombo vya habari vya ndani zinaeleza.
Maelezo machache ya madai ya njama hiyo yametolewa na viongozi mbalimbali wa upinzani wanadai kuwa mashtaka dhidi ya Kaliati yamechochewa kisiasa.
Wafuasi wa UTM walikusanyika nje ya mahakama na kuimba nyimbo za kuipinga serikali kabla ya kusikilizwa kwa kesi, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.
Ndani ya mahakama hiyo, mahakama iliambiwa kwamba Kaliati alikuwa na washiriki wawili, waliosemekana kuwa walikimbia.
Hatimaye hakimu aliamua kwamba Kaliati anaweza kuachiliwa kwa dhamana huku uchunguzi ukiendelea.
Mwendesha mashtaka wa serikali alikuwa ameomba azuiliwe kwa wiki nyingine.
Polisi nchini Malawi walisema wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kwamba haki za Kaliati zitaheshimiwa.