*Asema wanataka kuipeleka Zanzibar vichakani
Mchakato wa kuandika Katiba Mpya umepata hamasa kubwa hasa visiwani Zanzibar. Huko kuna kundi la dini lijulikanalo kama Uamsho. Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Othman Masoud Othman, ameamua kuweka mambo sawa kwa kile anachoona jinsi kikundi cha Uamsho kinavyoipotosha jamii. Endelea…
Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Serikali: (anaendelea) Mwisho Mhe. Spika, mimi naomba nizungumzie kidogo tu suala la hoja ya Katiba Mpya. Na hili mimi naomba niizungumzie kwa sababu waheshimiwa wengi wamelizungumza tena vizuri, kwa ufasaha, kwa busara ya hali ya juu; anayetaka kufahamu kama hakuwafahamu waheshimiwa walivyozungumza, basi huyu atakuwa na tatizo la kufahamu, lakini nadhani limeelezwa vizuri kabisa.
Nasema haya ninayoyasema machache ni kwa sababu tu ya kusaidia kuwatanabaisha wenzetu wananchi. Kwa sababu wakati mwingine mtu anaweza Mwenyezi Mungu akampa uwezo au nafasi na pengine akaitumia vibaya. Na nafasi moja ambayo wenzetu pengine wanaitumia vibaya ni hii ya kuwa kiongozi wa dini – wa taasisi ya dini.
Kwa sababu ukishakusema dini watu wanakutegemea na wanakuheshimu, sasa unapoitumia vibaya, kwa kweli unakuwa watu hukuwatendea haki.
Mimi hiki kikundi wenyewe wanaosema cha Uamsho waliniomba kuja kukutana na mimi ofisini kwangu, na nikawaambia sawa siku fulani njooni na nikakaa nao kwa muda wa saa tatu nzima. Walieleza hoja zao. Moja ya hoja walizoeleza kwamba ‘sisi bwana Muungano’ na hili ndilo ambalo wamekwenda kuwapotosha watu kwa bahati mbaya sana, kwamba ‘sisi baada ya kujadili Katiba Mpya tujadili kwanza huu Muungano wenyewe si halali’.
Wakasema kwa mujibu wa ‘Fiqhi-l-Usul’ jambo likishakuwa haramu haliwezi kuhalalika, nikawasilikiza vizuri na mimi nikawauliza, lakini tutakapokuja kuamua huo uhalali wa Muungano tutatumia Fiqhi-l-Usul au Fiqhi-l-dunia. Hii sheria yetu ya nchi ndiyo itakayotumika?
Sasa kama ni hoja hiyo, hiyo hoja haina msingi na kwa nini haina msingi? Haina msingi kwa sababu kama unahoji suala la uhalali wa Muungano suala la uhalali itabidi ufuate sheria tulizonazo za nchi. Lakini tujaaliwe ukubaliwe huo Muungano au tuseme upige hiyo kura ya maoni useme huu Muungano basi watu wote hatuutaki kwa Zanzibar.
Kwanza suala la msingi la kujiuliza, sasa nani watakaopitisha hilo azimio si Baraza hili, ndio hapa ambapo waheshimiwa wamesema aah, hii tumekubaliana sisi hii ni Representative Democracy. Bara hili ndilo lililopewa mamlaka hayo ya kupitisha hilo azimio lenyewe. Kwa sababu sasa hivi badala ya kuwa-engage hawa Wajumbe wa Baraza wenyewe badala ya kuwa unakaa huko na kuanza kuwatukana unataka nani aje apitishe hilo azimio. Wao wanahubiri amani, Wajumbe wa Baraza wewe unahubiri fujo sasa mwisho wa siku nani apitishe hilo azimio.
Lakini kwa utaratibu huo hata azimio Baraza hili likipitisha kwa mujibu wa ibara ya 1998 ya Katiba ya Muungano, inabidi suala liende bungeni na wakubali wabunge wa Bara two third majority – wakubali wabunge wa Zanzibar two third majority. Sasa hawa wabunge wa Zanzibar hujawa-engage unafanyia fujo wao wanahubiri amani kwanza watapitishaje? Wakikataa wale wenzetu two third majority huo Muungano unaosema uishe utakwishaje? Sasa unawapeleka watu katika njia ambayo mwisho wake almost hauwezekani.
Lakini leo imekuja njia hii ambayo hilo unalolitaka, maana yake kumetengenezwa barabara ya lami unaweza ukapita kama alivyosema Mwenyekiti wa Tume wewe peleka. Uzuri wa Sheria hii ya Marekebisho ya Katiba imeeleza kwamba watu watachukuliwa maoni, halafu zitakuwa forum kujadili je, maoni yao yamechukuliwa? Halafu litaundwa Bunge la Katiba ambapo wawakilishi wote hao watakuwamo kwenye Bunge hilo na maamuzi itakuwa Zanzibar pia ina maamuzi na baada ya hapo watakachoamua hao Wabunge wa Bunge la Katiba litarudi kwa wananchi.
Sasa hii njia unayotaka kuwapitisha watu wewe ni pori tupu, hii njia ambayo imewekwa wazi you can see all the stairs kwa nini uwapitishe watu katika dead end wakati njia sahihi, nyeupe ipo imewekwa?
Mimi ndiyo maana nasema watu wetu, wenzetu wananchi ni vizuri wapime hiyo njia wanayotaka kupelekwa na hawa watu. Hawa wanataka kuwatia porini wakati njia nyeupe ipo tena imetandikwa vizuri kwenye sheria na hii sheria kwa bahati nzuri imeandikwa kwa Kiswahili na Kiingereza.
Labda kazi mimi niwaombe waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili watusaidie au tusaidiane katika kuwaelimisha wananchi kwamba njia nyeupe ipo, hii tunayohubiri ndiyo njia nyeupe lakini ukitaka njia hiyo njia nyingine labda kama umejitayarisha vita. Kwa sababu wakikataa wenzetu utakwenda kupigana vita? Ndiyo maana yake.
Sasa mimi ninachosema ni kwamba nawaomba sana watu waelewe kwamba vurugu na fujo haitosaidia, na mwisho itakuwa kichekesho kweli kweli Mheshimiwa Spika. Kwa sababu wewe kama unawatetea watu wa Zanzibar halafu watu wa Zanzibar ndio unaowafanyia fujo, maduka yanafungwa, nyumba zao zinaingia mabomu, sasa wewe wakili gani wa kwamba yule unayemtetea ndiye unayemuathiri, yule mgomvi wako kakaa bukheri hana wasiwasi.
Hizi nadhani kweli, mimi nadhani watu watafakari maana yake tatizo la hili jambo wala halihitaji darasa ukiangalia unaona hapa pana tatizo, halafu wakili anayekwambia mimi nitakutetea mpaka upate nchi yake yeye mwenyewe kushitakiwa kwa maandamano katafuta wakili, lakini huyu anasema anaweza kutengeneza hoja ya kisheria mpaka akakupatia wewe nchi yako. Jamani si jambo la ajabu?
Sasa mimi naomba watu wakae watanabahi, watafakari hili jambo wataona kwamba hapa wenzetu hawana nia ya kututetea, hawana nia ya maslahi ya nchi yetu isipokuwa labda wana ajenda yao ya siri (makofi).
Mheshimiwa Spika, mimi nilisema niseme hayo machache kwa sababu nadhani yatasaidia labda kufumbua macho kwa anayetaka kuyafumbua. Lakini baada ya kusema hayo na mimi niseme naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja ahsante sana. (Makofi kwa dakika tano)
Mheshimiwa Spika: Wahehsimiwa Wajumbe hapana shaka makofi hayo ya kumshukuru sana Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu kwa maelezo, kwa hotuba aliyotoa akiwa anasaidia hoja mbalimbali ambazo zimetolewa hapa, lakini pia hata hoja ambazo zinatoka kwa wananchi. Muda uliobaki ni dakika 25, hii ni shughuli kubwa muhimu ambayo ni vizuri tukaitafakari vizuri sana.
Sasa ni juu yetu Waheshimiwa Wajumbe tukiona kazi hii tuimalize sasa hivi nimwambie mheshimiwa hapa atoe hoja, la, kwamba mwafaka wetu na kwa vile jinsi tunavyoona inafaa ili shughuli hizi ziende vizuri tutafakari haya yaliyozungumzwa sasa hivi basi pengine shughuli hii tuifanye kesho. Niliona tufanye hivi kwa sababu haiwezekani Waheshimiwa Wajumbe waseme maneno mengi, wahoji mengi bila ya serikali kutoa majibu kuhusu hayo.
Kwa hivyo, mawaziri wote wale ambao waliomba na kuna jambo waliseme kumsaidia Mheshimiwa waziri. Nashukuru kunisikiliza kwa makini na nadhani inafaa sana kutafakari hayo pamoja na mheshimiwa waziri kwenda kujitayarisha vizuri zaidi.
Kwa sababu bajeti hii tukiipitisha vizuri muswada ule utaokuja baada ya kazi hii nao unakuwa ni mwepesi. Kwa mtazamo huu na kwa furaha hii basi naomba tusitishe shughuli zetu kuanzia sasa na kuahirisha kikao hiki hadi kesho.
(Saa 1:20 usiku Baraza liliahirishwa hadi tarehe 21/6/2012 saa 3:00 asubuhi)