Na Mwandishi Maalum

Mwanariadha wa Jeshi la Polisi Konstebo Transfora Mussa ameibuka mshindi wa kwanza kwa upande wa wanawake kupitia mbio za kilometa 10 katika mbio za Fulham 10k zilizofanyika Nchini Uingereza Novemba 17, 2024 huku akifanikiwa kuvunja rekodi iliyokuwa inashikiliwa kwa kukimbia muda mfupi zaidi.

Mwanariadha huyo ambaye alipewa medali ya dhahabu, alivunja rekodi hiyo kwa kutumia muda wa dakika 31:53 tofauti na rekodi ya mwaka jana ambapo mwanariadha kutoka Nchini Kenya alishinda kwa kutumia muda wa dakika 33:11 katika mashindano hayo.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya mwanariadha huyo katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege KIA, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Alphonce Bandya kwa niaba ya Kamanda wa Polisi pamoja na kumpongeza Mwanariadha huyo kwa kuliletea sifa Jeshi hilo, amesema wataendelea kutoa ushirikiano wakati wote kwa timu hiyo ili ipate mafanikio zaidi.

Kwa upande wake Konstebo Transfora mara baada ya kuwasili katika Uwanja huo wa ndege leo Novemba 19, 2024 na kupokelewa na Maafisa, Wakaguzi na Askari amesema nidhamu pamoja maandalizi mazuri aliyoyafanya ndio msingi wa mafanikio hayo ambapo ameahidi kufanya vizuri zaidi katika mashindano mengine.

Kocha Msaidizi wa Timu hiyo Sajenti Oswald amesema usikivu na nidhamu wakati wa maandalizi katika kambi yao sambamba na kupata ushirikiano wa karibu kutoka kw0a Uongozi mzima wa Jeshi la Polisi pindi wanapohitaji ndio chachu ya mafanikio yao.